Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mijadala chanya kijinsia huimarisha jamii kiafya

6c2be1fd0131740ce59eac020b92c0e9 Mijadala chanya kijinsia huimarisha jamii kiafya

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KWA miaka zaidi ya kumi sasa, watendaji wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) wamekuwa wakiendesha vituo simulizi ili kuongeza uelewa juu ya masuala yanayohusiana na jinsia ili kufikia usawa katika muundo wa jamii.

Vituo hivi vya kusimulia hadithi, maarufu kwa Kiswahili kama 'vilinge' vina mbinu zinazowezesha mazungumzo na majadiliano kama kazi ya vikundi, utafiti, vikundi vya kijiweni, kujadiliana na kutazama video kwa pamoja.

Hivi vinalenga kuboresha maisha ya wanawake na vikundi vingine vilivyo katika mazingira magumu katika jamii sambamba kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia ukiwamo dhidi ya wanawake na watoto.

Baadhi ya mikoa iliyonufaika na vituo hivi vya kusimulia hadithi ni Kilimanjaro, Mbeya na Pwani, ambapo viongozi wa wanawake wamepongeza mikutano hiyo, ambayo imefungua kurasa mpya za kihistoria katika maisha yao.

Hadija Mwanahomboza kutoka Masaki wilayani Kisarawe katika Mkoa wa Pwani, anakiri vilinge vimemsaidia kufahamu mengi mintarafu ukatili wa kijinsia katika eneo lake.

Mwanahomboza ambaye ni mwanamke wa makamo, anasema sasa ana uwezo wa kuelezea aina tofauti za ukatili wa kijinsia, haki za binadamu katika, na pia anaweza kuandaa mpango wa namna ya kushiriki kudhibiti unyanyasaji kwa wanawake na vikundi vingine vilivyo katika eneo lake.

"Nimejifunza aina tofauti za unyanyasaji wa kijinsia unaofanyika nyumbani na hata mahali pa kazi,” anasema.

Katika mkutano kwa njia ya simu uliofanyika makao makuu ya TGNP, Mabibo, Dar es Salaam hivi karibuni, Mkufunzi wa Jinsia, Deogratias Temba, alisema TGNP inaendesha vituo vya kusimulia hadithi ili kuwapa wanawake fursa ya kusimulia mafanikio yao na changamoto za maendeleo zilizo katika maeneo yao ya makazi.

"Tunavutiwa zaidi na ujenzi wa uwezo, kuhakikisha kuwa wanawake tunaowafundisha wanapata uwezo wa kushughulikia changamoto za jinsia na maendeleo wanazokabiliana nazo katika maisha ya kila siku.”

“Tunawafundisha pia namna ya kuboresha maisha yao kwa kujiunga na vituo vya mikopo katika vijiji vyao," anasema Temba.

Naye Devotha Likokola aliyeshiriki mahojiano hayo kwa njia ya simu na wanawake walionufaika na TGNP vilinge, anasema wakati wanawake wamefundishwa vizuri, wanaweza kupata mapato mazuri, si kwao tu, bali kwa jamii kwa jumla.

Leo, neno 'Vicoba' linajulikana kila kona ya nchi na wanawake na vijana wengi wamejiunga navyo katika maeneo yao kama fursa ya kukusanya mtaji kwa njia ya mikopo na kuongeza uzalishaji wao.

Devotha ambaye ndiye mwanzilishi wa Vicoba, alitumia mkutano huo kuwashauri wanawake namna ya kubadilisha na kuyafanya maisha yao kuwa bora.

Anasema wanawake wengi wanakabiliwa na changamoto kubwa katika maendeleo yao kibinafsi kwa kuwa hawajapewa maarifa sahihi ya nini cha kufanya ili kuboresha maisha kijamii na kiuchumi.

Mwanamke huya ambaye pia ni mwanasiasa aliyehudumu kama mbunge kwa miaka kumi, anasimulia historia yake akisema, alifanya kazi katika benki ya NBC na kuacha kazi mwaka 1989.

Anasema alipoacha kazi aliamua kufungua mgahawa kama uwekezaji wake, kabla ya kuhamia zaidi katika uwanja siasa kwa kushiriki udiwani huko Songea kabla ya kuingia bungeni.

Kwa mujibu wa Devota, katika kipindi hicho aliamua kuanzisha kituo endelevu cha mikopo inayolenga kuwakomboa wanawake kimaendeleo.

Anasema anajivunia mpango huo kuwasaidia wanawake wengi kujiongezea kipato na kuwa msaada mkubwa katika kukidhi mahitaji ya familia wao kama vile kuwapeleka shule bora na kujenga nyumba nzuri.

“Lengo ni kusimamia vikundi vidogo vya wanachama ambao wamefundishwa. Serikali pia imekuwa ikihimiza watu kuja katika mabaraza mbalimbali ili kujiunga na vikundi kama hivyo, ili walengwa wafaidike," anasema.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kati cha Kibosho, Juliet Mkonyi, anasema amenufaika na vilindi vya TGNP, na sasa ameweza kujenga mabweni katika shule nyngine za kata na kuboresha utoaji wa huduma katika zahanati katika eneo lake.

"Baada ya kusikia alichokisema Mama Devota Likokola kuhusu kuboresha maisha ya wanawake, sasa ninaweza kuweka mipango ya namna ya kuwapa vifaa vya mikopo wanawake ili waweze kuendesha biashara na miradi ndogo ndani nje ya kijiji chetu," anasema.

Naye Paulina Shirima anayefanya kazi katika Kijiji cha Okaoni, anasema amejitahidi kusaidia wanawake wengi kuanzisha kilimo cha mbogamboga huko Umbwe Okaoni.

Anasema wanawake hao wamefanikiwa kutoa aina tofauti za mboga za majani ikiwa ni pamoja na nyanya na kabeji.

Ingawa anaitaja changamoto ya kukosekana kwa usafiri w auhakika kama kikwazo, anasema anafurahi kuona wale aliofanikiwa kuwatyembea, wamefanikiwa.

Mkazi wa mkoani Pwani, Mwanaisha Waziri, ni mmoja miongoni mwa wanawake wengi waliofaidika na Kituo cha Kusimulia Hadithi cha TGNP.

Anasema katika kijiji chake, hakukuwa na shule ya sekondari, lakini wamefanikiwa kujenga moja, na hadi sasa wamejenga vyumba vitatu vya madarasa, ofisi ya walimu ofisi na choo cha shimo.

"Tuna kamati za wazazi wenye nguvu zinazokutana mara nyingi, kuhakikisha watu wanachangia pesa kuwezesha ujenzi wa shule hii kukamilika.”

“Kwa kweli mafunzo ya TGNP yamesaidia viongozi wa wanawake kujua majukumu yao katika jamii, na sasa wana ujasiri wa kuzungumza bila woga,” anasema Mwanaisha.

Kwa upande wake, Sharifa Issa Salum kutoka Kata ya Kibuta wilayani Kisarawe, kwa kushirikiana na wanaume katika eneo lake, wanawake wamechimba kisima cha maji ambacho kimetatua shida ya maji katika kijiji hicho na kusaidia kutoa nafasi zaidi hata kwa watoto kuhudhuria zaidi shuleni na kupata muda wa ziada kufuatilia masomo.

Anatoa shukrani akisema mafunzo ya TGNP yamesaidia kuhamasisha wanawake kuhusu majukumu yao katika jamii.

Mmoja wa watendaji wa TGNP anayekataa kutajwa anasema: “TGNP inafahamu kuwa, bila ujumuishaji wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, hakuna chochote endelevu kinachoweza kutekelezwa katika kufanikisha maendeleo.”

Anasema TGNP inaendesha semina nchi nzima kuwezesha wanawake katika vituo vyao vya maarifa vilivyowekwa ili kuwawezesha kama kikundi kuwa endelevu na kila mshiriki mmoja katika vituo hivi kuwa na uwezo wa kiuchumi.

Miongoni mwa mipango mingi ni utekelezaji wa Miradi ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi (WEE) inayolenga kuwezesha jamii ya msingi kuanzisha na kuendesha vituo bora vya maarifa vinavyosaidia wanachama kuanza na kuendesha shughuli za kuongeza mapato katika jamii za vijijini kama Wilaya za Kisarawe, Moshi Vijijini na Morogoro. .

Kuwawezesha wanawake wenye ujuzi na mjasiriamali kujua namna ya kushughulikia changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku za kiuchumi.

Uchunguzi wa makala haya umebaini kuwa, TGNP inafanya kazi na wadau wanaotetea haki za wanawake ili kumaliza aina zote za ubaguzi, unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na vikundi vingine vilivyotengwa wakiwamo watoto na watu.

Kimsingi wadau mbalimbali wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia wanasema uwezeshaji wanawake lazima uanzie chini kuliko na wengi wasio na sauti ya kijamii, kiuchumi wala kisiasa.

Mdau yeyote, liwe shirika la kike linalojitahidi kuchangia kujenga harakati mahiri ya mabadiliko ili kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na haki ya kijamii ni mshirika wa TGNP katika biashara.

Kimsingi, wanawake wakiwezeshwa ipasavyo kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiuongozi, upo uwezekano mkubwa kwamba watoto wao wataenda shule, watapata huduma bora na za kutosha za afya sambamba na chakula.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili.

Columnist: habarileo.co.tz