Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Miezi sita ya Fei Toto kucheza soka viunga vya TFF

Fei Soka TFF Miezi sita ya Fei Toto kucheza soka viunga vya TFF

Tue, 9 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jinsi ambavyo maisha yanakwenda kasi. Niliwahi kusema mahala. Hatimaye tumefika Mei tukiwa na sakata la Fei Toto mkononi mwetu. Anaitwa mwanasoka lakini hachezi soka la ushindani tangu Desemba mwaka jana.

Kwa sasa Fei amekuwa maarufu katika viunga za TFF kando yake akiwa na meneja wake pamoja na wakili wake. Haonekani uwanjani tena. Niliwahi kusema mahala kwamba yeyote aliyemshauri Fei kuanzisha varangati hili katikati ya msimu hakumshauri vizuri.

Kwanza kabisa mkataba huwa unavunjwa kwa sababu maalumu. Kwa sasa hakuna sababu maalumu ya Fei kujaribu kuvunja mkataba wake katikati ya msimu. Hakuna. Labda angejaribu jambo hili mwisho wa msimu. Hakukuwa na dharura ya kuvunja mkataba.

Na kama ningekuwa mshauri wa Fei au mshauri wa tajiri wa klabu nyingine inayomtaka Fei ningemwambia tu asubiri mkataba wake umalizike Yanga. Jaribu kufikiria kwamba hatimaye tumefika mwishoni mwa msimu huu na sasa mkataba wa Fei na Yanga utakuwa umebakiza takribani miezi tisa tu ya mpira.

Kama unadhani ni mbali jaribu kuwaza ni namna gani ghafla tumefika Mei kutokea Desemba. Linaonekana kama sakata la juzi tu lakini tayari ni sakata lenye miezi sita mkononi. Ningemshauri tajiri yeyote anayemtaka Fei ampe ‘kishika uchumba’ na asisaini mkataba mpya na Yanga.

Sasa hivi mkataba wa Fei ungekuwa unaelekea ukingoni. Msimu wa soka sio mwaka ni miezi tisa tu. Fei angeenda katika maandalizi ya msimu mpya na Yanga na kisha kucheza msimu ujao kuanzia Agosti mpaka Mei halafu angeondoka kiulaini tu bila ya vurugu hizi.

Tatizo inaonekana kama vile mahitaji ya anakotaka kwenda ni dharura. Sio kweli. Fei hana miaka 40 kwamba unahofia anaweza kwisha ghafla. Bado ana muda mrefu wa kucheza soka katika kiwango cha juu. Kinachotokea kwa sasa ni kujaribu kushusha kiwango chake bila ya kufahamu.

Miezi sita iliyopita Fei amekosa kucheza mechi kibao za kimataifa katika jezi ya Yanga. Amekosa mechi za makundi za Yanga, amekosa mechi mbili za robo fainali, lakini sasa hivi anajiandaa kuzikosa mechi mbili za nusu fainali dhidi ya Marumo Gallants.

Kama angekuwa mvumilivu sasa hivi Fei angekuwa katika ‘Fitness’ ya hali ya juu. Bahati mbaya pia baada ya juzi kuendelea kupigwa chini pale TFF, kama akiendelea kuwa na msimamo ule ule na kisha kwenda kudai haki yake mbele ya safari basi tuna uhakika huenda tusimuone Fei uwanjani kwa miezi mitatu ijayo.

Mwisho wa siku kuna uwezekano mkubwa tusione tofauti ya Fei ambaye atakuwa amemaliza mkataba. Labda mwisho wa kesi yake unaweza kuwa na tofauti ndogo na mwisho wa mkataba wake na Yanga. Ni kitu kile kile tu kama angekuwa anacheza.

Anaweza kwenda katika timu yake mpya akiwa hayupo fiti. Tajiri anayemtaka Fei ingekuwa kama vile amewaazima Fei kwa muda tu kuelekea katika timu yake. Hizi za mechi za sasa zingemuweka fiti zaidi na zingemsaidia anakotaka kwenda.

Tatizo letu tunakosa uvumilivu. Wachezaji wengi mahiri barani Ulaya kwa sasa huwa wanaondoka bure katika klabu zao kwa sababu wana mipango na hawana haraka. Hawa ndio akina Antonio Rudiger ambao wamefanikiwa kutiririsha mikataba yao mpaka mwisho wa msimu.

Kama Fei na watu wake wakienda CAS wasitegemee kwamba hukumu itachukua mwezi mmoja tu. tunaweza kujikuta hadi Septemba tukisubiri maamuzi haya haya. Hata kama Fei akishinda kesi yake, kitu ambacho sikitarajii, kuna uwezekano mkubwa maamuzi hayo yakawa yametolewa nje ya dirisha la usajili wa wachezaji.

Kitu cha msingi kwa sasa ni Fei kujaribu kukutana na watu wa Yanga na kuangalia namna ya kuvunja mkataba wake. Ninachofahamu ni kwamba Fei hana mpango wa kucheza tena Yanga, na wakati huo huo Yanga nao hawana mpango na Fei.

Yanga wanachotaka ni haki yao tu. itangazwe kwamba Fei ni mchezaji wao halali ili wamuuze anakotaka kwenda. Nadhani kinachohofiwa na upande wa Fei ni kwamba Yanga wanaweza kupanga dau kubwa la kumuuza staa mwenyewe.

Hata hivyo, kwa jinsi ambavyo jambo lenyewe limewachosha Yanga huku timu yao ikiendelea kufanya vema katika michuano ya ndani nan je, kuna uwezekano mkubwa wakawa tayari kumuuza hata kwa pesa ambayo itasababisha aondoke bila ya shida.

Sioni kama kuna uwezekano wowote wa Fei kujenga daraja la mahusiano na watu wa Yanga kuanzia viongozi, wanachama, mashabiki na benchi la ufundi. Muda aliokaa nje ni mrefu. Kama angekuwa ametoweka kambini ndani ya wiki mbili wangeweza kusema kwamba mtoto alikuwa amepotoka.

Kwa kipindi ambacho amekaa nje imeonekana wazi kwamba dhamira yake haijawahi kubadilika. Suala hili lipo katika mikono yake kwa sasa. Yanga hawawezi kumfuata Fei ili wamalizane. Ni Fei ndiye ambaye anaweza kuwafuata Yanga ili wamalizane.

Kinachotokea kwa sasa ni majivuno kutoka katika kambi yake. Labda washauri wake wanataka kuionyesha Yanga ubabe katika vyombo vya sheria. Vyovyote ilivyo ambaye anaathirika kwa sasa ni Fei. Yanga wanaonekana kuwa na timu nzuri kwa sasa kiasi kwamba maisha yao yameendelea kusonga mbele bila ya Fei.

Ningekuwa mshauri wa tajiri ambaye anamtaka Fei ningemwambia tu amrudishe Fei akacheze Yanga kwa ajili ya kujiweka fiti ilia je katika timu yake akiwa vizuri miezi tisa ijayo. Ni kitu rahisi tu na ndicho ambacho wachezaji wajanja wamekuwa wakitumia kuondoka bure.

Columnist: Mwanaspoti