Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Michezo ilivyopaisha miaka mitano ya JPM

JPMSIMBAA Michezo ilivyopaisha miaka mitano ya JPM

Mon, 22 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

ILIKUWA ni miaka mitano ya kusisimua katika tasnia ya michezo, chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli 'JPM'. Ni miaka mitano ambayo Watanzania wapenda michezo hawataisahau, kwa sababu imekuja kuibua tena nchi ambayo kwa miaka kadhaa ilikuwa imelala au kusuasua kwenye masuala ya michezo.

Hata alipotoa hotuba yake ya kuvunja Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania siku ya Jumanne iliyopita, JPM ameitaja michezo, sanaa kuwa ni moja ya vitu ambavyo katika kipindi chake cha uongozi, iliipaisha kwa kiasi kikubwa bendera ya nchi katika mashindano ya kimataifa.

"Na kwa hilo, naipongeza sana timu yetu ya taifa ya soka ambayo baada ya takribani miaka 39 kupita, hatimaye mwaka jana 2019 ilifanikiwa kufuzu kuingia fainali ya Kombe la Afrika," alisema Bungeni.

Mbali na Stars, Rais pia aliwapongeza wanamichezo mbalimbali wa ngumi na riadha ambao kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita walipeperusha vema bendera ya taifa.

"Mheshimiwa Spika, kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na wasanii na wanamichezo, serikali imejipanga katika miaka mitano ijayo kuweka mkazo mkubwa zaidi kwenye sekta hii iliyowaajiri vijana wetu wengi," aliahidi.

Kwenye makala hii, tunaangalia mafanikio ya michezo yote iliyopatikana nchini chini ya uongozi wa miaka mitano ya JPM.

WANAWAKE KUTWAA CECAFA MARA MBILI

Chini ya uongozi wa Rais Magufuli, Timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Queens' ilifanikiwa kutwaa Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) mara mbili.

Mara kwa kwanza ilikuwa ni mwaka mmoja tu baada ya utawala wake, mwaka 2016, ilipotwaa ubingwa huo nchini Uganda kwa kuifunga Kenya mabao 2-1 kwenye mechi ya fainali iliyochezwa mjini Jinja.

Yalikuwa ni mabao ya Mwanahamisi Omari 'Gaucho' na Stumai Abdallah.

Miaka miwili baadaye, timu hiyo ilifanikiwa kutetea kikombe hicho kwa kuifunga Timu ya Taifa ya Ethiopia mabao 4-1, Julai, mwaka 2018 Katika mashindano yaliyofanyika jijini Kigali, Rwanda.

Kabla ya hapo iliifumua Uganda mabao 4-1 na kutoka sare na Kenya kwa kufungana bao 1-1.

SIMBU KUSHINDA MARATHON

Baada ya muda mrefu tangu kupita, hatimaye Tanzania ilifanya vema kwenye riadha mwezi Januari, mwaka 2017, miaka miwili tu ya kutwaa madaraka Rais Magufuli, pale mwanariadha aliyekuwa mgeni masikioni mwa watu, Alphonce Simbu alipotwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya riadha ya dunia yaliyojulikana kama Mumbai Marathon yaliyofanyika nchini India. Alitumia saa mbili, dakika tisa na sekunde 32 kuipeperusha vema bendera ya Tanzania.

MWAKINYO KUMTWANGA MWINGEREZA

Ilikuwa ni Septemba, mwaka 2018, kwa bondia Mtanzania asiye na jina, Hassan Mwakinyo, alipoishangaza dunia alipomtwanga Mwingereza Sam Eggington nchini Uingereza, kwenye pambano la utangulizi la bondia Amir Khan dhidi ya Samuel Vargas.

Pambano hilo lililochezwa kwenye ukumbi wa Arena Birmingham, jijini Birmingham ndilo lililomtangaza Mwakinyo na kuhesabika kuwa mmoja wa mabondia bora kabisa kwa sasa nchini, baada ya kumtwanga bondia huyo ambaye ni bingwa wa zamani wa Uingereza, Ulaya na Jumuiya za Madola kwa (TKO) sekunde ya 45 raundi ya pili.

Baada ya pambano hilo, Mwakinyo alipata sifa na hivyo kuandaliwa pambano lingine nchini Tanzania ambalo alipigana dhidi ya mmoja wa mabondia maarufu kabisa duniani, Arnel Tinampay mwishoni mwa Novemba mwaka jana 2019.

Mwakinyo alidhihirisha kuwa hakubahatisha kwa kumfinyanga Mfilipino huyo kwa pointi na kuzidi kuipaisha nchi ndani ya utawala huu.

SIMBA KUNG'ARA AFRIKA

Simba ilifanikiwa kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara kwanza tangu ilivyofanya hivyo mwaka 2003, baada ya miaka 15 kupita, wakati Tanzania ilipokuwa chini ya Uongozi wa Awamu ya Tatu ikiongozwa na Rais, Benjamin Mkapa.

Baada ya miaka hiyo kupita, chini ya Rais Magufuli, Simba ilifanikiwa kutinga hatua ya makundi baada ya kuichapa Nkana FC ya Zambia mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kutinga kwa jumla ya mabao 4-3, baada ya kufungwa mabao 2-1 nchini Zambia.

Mechi iliyosisimua wengi ilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini dhidi ya Nkana ambayo iliipeleka Simba hatua hiyo ilichezwa mwishoni mwa Desemba 2018.

Simba pia ilikuwa ndiyo timu ya mwisho kutinga hatua hiyo mwaka huo huo wa 2003.

Baada ya miaka 25, Simba ilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini, mechi iliyochezwa Machi mwaka jana.

Ingawa Simba iliwahi kufika nusu fainali ya michuano hiyo mwaka 1974, chini ya utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lakini pia ilifika robo fainali mwaka 1994, Tanzania ikiongozwa na Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili.

Rais Magufuli aliingia kwenye rekodi ya kuwa mmoja wa Marais ambao wametawala nchi, na klabu ya soka kufanikiwa kufika hatua hiyo.

STARS KUTINGA AFCON

Machi mwaka jana, Timu ya Taifa (Taifa Stars), ilikata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kwa kuichapa Uganda mabao 3-0 na kushika nafasi ya pili kwenye Kundi L, ikimaliza kwa pointi nane, kundi likiongozwa na Uganda iliyokuwa na pointi 13.

Ni moja kati ya mafanikio makubwa kwenye michezo nchini Tanzania, chini ya serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli.

Ni kwa sababu mara ya mwisho Stars kufanya hivyo ilikuwa ni miaka 39, ilipoitoa Zambia kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda bao 1-0 nyumbani na kutoka sare ya bao 1-1 mjini Ndola mwaka 1979.

Wakati huo nchi ilikuwa kwenye uongozi wa Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Nyerere na ikacheza fainali zake mwaka 1980 nchini Nigeria.

Vizazi kadhaa vilipita bila kuona tukio hilo, ambalo lilikuja kutokea tena kwenye Awamu ya Tano, Stars ikifuzu na kucheza fainali zake nchini Misri.

WASICHANA KUTWAA COSAFA

Mafanikio mengine ya michezo nchini chini ya uongozi wa Rais Magufuli ndani ya miaka yake mitano ni pale timu ya soka wa wanawake chini ya miaka 20 'Tanzanite' ilipofanikiwa kulichukua Kombe la Mataifa ya Kusini kwa Afrika (COSAFA).

Baada ya kufanya vema ma kutinga fainali, Tanzanite iliitwanga Zambia kwenye mechi ya fainali iliyochezwa Agosti, mwaka jana 2019 nchini Afrika Kusini kwa mabao ya Opa Clement na Protasia Mbunda.

U-20 KUTWAA CECAFA

Timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania Bara chini ya miaka 20 nayo haikuwa nyuma, Oktoba mwaka jana 2019 ilitwaa Kombe la Afrika Mashariki na Kati kwa kuwafunga wenzao kutoka Kenya katika mechi ya fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Njeru, Jinja nchini Uganda.

Rekodi zinaonyesha kuwa hiyo ilikuwa ni mara ya pili kutwaa. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1971, chini ya uongozi wa Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere na haikufanikiwa, hadi utawala huu wa Rais Magufuli.

Columnist: www.tanzaniaweb.live