Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Miaka 59 ya Uhuru na wimbo Tazama ramani

2e97a18db0ba62eeaf466faf014221dd Miaka 59 ya Uhuru na wimbo Tazama ramani

Wed, 9 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TANZANIA naweza sema ni nchi yenye upekee hasa kwa kusheheni nyimbo nzuri zenye mrengo wa kukuza uzalendo dhidi ya wananchi wake. Mara nyingi nyimbo zake zimejaa mahaba makubwa ambayo tukifikiria kwa kina sana na angalau kutekeleza asilimia 75 ya kilichoko kwenye nyimbo hizo nchi yetu haiwezi kuwa tena na watu wanaoisema vibaya nje hata kidogo.

Mahaba haya yanayooneshwa kwenye nyimbo zetu hizi pengine yanalenga kutujenga kama vijana hasa kuzidi kuipenda na kuithamini nchi yetu.

Wimbo wa ‘Tazama ramani utaona nchi nzuri’ ni moja kati ya nyimbo hizo nilizogusia hapo juu. Kwa ajili ya kuleta maana katika makala haya naomba kunukuu ubeti wa pili na wa tatu:

‘Chemchemi ya furaha amani nipe tumaini, Kila mara niwe kwako nikiburudika. Nakupenda sana hata nikakusitiri, Nitalalamika kukuacha Tanzania.

Majira yetu haya, yangekuwaje sasa, Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha X2

Nchi yenye azimio lenye tumaini, Ndiwe peke yako mwanga wa Watanzania, Ninakuthamini hadharani na moyoni, Unilinde nami nikulinde hata kufa.

Majira yetu haya, yangekuwaje sasa, Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha X2

Kimsingi, wimbo huu unagusia mambo makuu ya kuzingatiwa kwa mustakabali mzima wa taifa letu. Mambo hayo ni pamoja na kudumisha amani, kutoa hali ya matumaini kwa watanzania masikini walio wengi, ulinzi wa mali asili zetu na kudumisha mapenzi mema kwa nchi yetu, yaani uzalendo.

Katika muktadha huo, dhana nzima ya kulinda maslahi ya taifa na wananchi wake ndo jambo la msingi sana katika nchi yoyote ile huru.

Kwa ajili ya kuweka mlolongo mzuri kwa msomaji, uzalendo ni hali ya mtu kuipenda, kuithamini, kuisitiri na kujitoa kwa ajili ya nchi yake.

Mzalendo wa kweli daima anaweka maslahi ya nchi mbele na ya kwake binafsi nyuma. Kwa maana hiyo, mzalendo ni mtu yeyote mzawa na mwenye kuipenda na kujitoa mhanga na saa nyingine ikibidi kufa kwa ajili ya nchi yake kwa maslahi ya wananchi walo wengi.

Uzalendo unabeba dhana nyingi sana ikianzia asili, utamaduni, lugha, siasa, historia, na mambo kadha wa kadha. Dhana zote zikifungwa kwenye dhana kuu ya utaifa.

Kuwa mzalendo ni zaidi ya kuifia nchi yako. Kwa sababu aidha kwa uzembe au kwa ujinga au kwa imani yake mtu aweza kufa lakini kumbe hakuipenda nchi ila kwa matakwa yake binafsi.

Shinikizo la kuifia nchi ni lazima liwe tunda la uaminifu, upendo wa kujitoa, kuipigania na kuitetea nchi yako. Wako wazalendo ambao wameitetea nchi yao toka utotoni, ujanani na uzeeni na hawakuifia nchi. Watu wasio wazalendo ni hawa hapa: watu wanaoihujumu nchi kwa kuiba, kutumia rasilimali za nchi vibaya, kuharibu miundombinu, kuweka pesa nje ya nchi, kuisema vibaya nchi na viongozi au watu wake, kushabikia wizi na ufisadi, kuvunja sheria za nchi, kuthamini vitu na mambo kutoka nje na mengine kama hayo.

Unaweza kweli ukawa mzawa, mwaminifu, mkweli lakini unakuwa kimya watu wanapoiba na kutumia vibaya rasilimali za nchi, wewe pia sio mzalendo kwa mfano huo.

Mara nyingi watu wengi hutumia neno la uzalendo kupotosha maana halisia ya dhana hii kwa wananchi (sasa itambulike kabisa kwamba hapa hatuzungumzii uchama japo haiepukiki). Wakati wa kupigania uhuru wa nchii, kilichokuwa kinawaongoza na kuwasukuma wapigania uhuru ni uzalendo.

Baba wa taifa na wenzie walikuwa na uzalendo wa dhati kabisa kabisa kupigania utaifa na kuulinda utaifa wetu japo tu kwa njia ya amani. Wakati huo lengo kubwa lilikuwa ni kutoa nchi yetu chini ya utawala wa mkoloni na kuleta maendeleo kwa watanganyika na baadaye watanzania wote kwa ujumla.

Kwamba haikutosha kupata uhuru tu bali kuwaletea watanzania mapinduzi ya kimaendeleo. Mapinduzi haya yalichukuliwa kama vita ya kulikomboa taifa kiuchumi.

Maneno haya yalithibitishwa kwenye sehemu ya tatu ya azimio la Arusha yanayosema: ‘TANU ina vita vya kulitoa Taifa letu katika hali ya unyonge na kulitia katika hali ya nguvu; vita vya kuwafanya wananchi wa Tanzania (na wananchi wa Afrika) watoke katika hali ya dhiki na kuwa katika hali ya neema. Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe, na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena.’

Baada ya miaka zaidi ya 50 tangu nchi yetu imepata uhuru, maneno haya yanatumiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kwa vitendo na kwa kuyasema kila mara anapolihutubia taifa kupitia matukio mbalimbali.

Je, inawezekana anarejea kwenye azimio la Arusha? Azimio lililotupiliwa mbali kwa vipindi vingi vya utawala? Kimsingi, matendo yake na staili yake ya uongozi vinaashiria kabisa kuchukizwa na umaskini wa Watanzania na unyonge wao. Na ni wazi kabisa kwamba anataka kuwatoa watanzania walio wengi katika dimbwi la umaskini.

Katika kipindi cha miaka mitano ya awali alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kurejesha heshima ya taifa letu, japo ni wazi kwamba hakupendwa na na baadhi ya wachache waliokuwa wananufaika na mfumo wa hovyo uliokuwa huipeleki nchi katika kujitegemea.

Kwa kiasi kikubwa amedhihirisha pasi na shaka kwamba aliyasoma na kuyashika vyema maneno ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere.

Swali lililo kwenye wimbo tajwa hapo awali “Majira yetu haya, yangekuwaje sasa amejitahidi kila uchao kulijibu. Kwamba kama asingekomesha wizi wa rasilimali za watanzania, sasa nchi ingekuwa wapi? Kama asingezuia usafirishwaji wa makinikia tungekuwa wapi? Kama asingezuia magendo ya madini nchi yetu ingekuwa wapi?

Kama asinge asingedhibiti dawa za kulevya kiasi kikunwa, hali ya vijana wetu ingeendelea kuwaje? Kama asingewatia moyo watanzania wakati wa covid-19 tungekuwa wapi? Na kama asingerudisha heshima ya utumishi wa umma leo hii nchi ingekuwa wapi?

Asingeondoa tabaka la walionacho na wasionacho tungekuwa wapi? Bila kuoresha miundombinu nchi ingekuwa wapi? Kama asingeboresha eneo la tiba tungekuwaje? Na kama asingetoa elimu bure na kuongeza wigo wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu hali ingekuwaje?

Maswali haya na mengineyo mengi ambayo hata Baba wa Taifa aliyasisitiza mara kwa mara wakati wa uteuzi wa mgombea urais kutoka chama tawala, yamekuja kujibiwa na Ndugu Magufuli katika kipindi hiki cha utawala wake.

Kwa muda mchache Tanzania imebadilika na kuwa gumzo ulimwenguni kwa mageuzi ya kiuchumi aliyoyaleta kwa watanzania walio wengi.

Pamoja na kwamba amejitahidi kufanya hayo bado kuna wanaoona kwamba anakosea. Kila mara wamekuwa wakimkosoa hasa kwa hoja zisizo na mashiko. Eti mtu anasema haya ni mandeleo ya vitu na siyo watu!

Kimsingi siwashangai kwa kuwa hata wakati wa kupigania uhuru kuna walioona kwamba Baba wa Taifa alikuwa anakosea. Haya aliyathibitisha wakati wa majadiliano na mwandishi wa habari, Saeed Naqvi kufuatia swali lake (ambalo sitanukuu).

Baba wa taifa alisema: “wakati tunapigania uhuru kuna waliosema kwa nini tunafanya hivyo? Walidai hatuna chochote kuendesha nchi. Lakini ilitubidi kupigania uhuru, tusingekubali kuendelea kuteseka. Hata sasa wapo wenye mawazo ya kutaka mataifa makubwa yaendelee kututawala na hivyo watafanya kila njia kutukatisha tamaa.”

Hili tumelishuhudia wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na pengine kabla ya hapo ambapo baadhi ya wanaharakati wanaojiita wanasiasa walipoamua kuhama nchi na kuisema vibaya.

Wakati Rais Magufuli anapigana kuzuia wizi wa maliasili zetu zikiwemo makinikia kuna walioona kwamba anakosea, kimsingi siwashangai kwa kuwa wangepeda nchi ibaki kuwa shamba la bibi ambalo mataifa makubwa yanachota raslimali kadri yanavyotaka huku wachache wenzetu ambao hawan uzalendo wanaoshirikiana nao ndio wakinufaika.

Tunapoadhimisha miaka 59 ya uhuru wetu leo, ni vyema kukumbushana juu ya uzalendo kwa maslahi mapana ya taifa letu na kuungana na viongozi wetu kulinda maslahi ya taifa leti lakini wakati huo huo kuhakikisha nyimbo zetu za kizalendo ziimbwe na kila mtu kufanyia kazi ujumbe uliomo.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni: +255 712 246 001; [email protected]

Columnist: habarileo.co.tz