Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mgambo Tarime wasichafue kazi ya Polisi

85498 Pic+mgambo Mgambo Tarime wasichafue kazi ya Polisi

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JESHI la Akiba maarufu Mgambo lina nafasi muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, kwa kushirikiana na vyombo vingine kama Jeshi la Polisi.

Mgambo ni jeshi muhimu la akiba, hasa inapotokea ‘uchokozi’ na ndiyo maana linawekwa kama akiba iliyo tayari kwa matumizi inapohitajika na pia ili lisaidie maana idadi ya askari polisi nchini ni ndogo ukilinganisha na mahitaji na idadi ya Watanzania katika kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu unapotokea.

Ndiyo maana katika maeneo mengi, mgambo wanashirikiana vizuri na polisi kuhakikisha kunakuwapo amani na usalama miongoni mwa jamii.

Ninawapongeza askari wote wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Zimamoto, Idara ya Uhamiaji, Mgambo na kampuni binafsi za ulinzi kwa kujitoa kwao kukesha usiku wakiumwa na mbu na hata kunyeshewa mvua, huku wananchi wengine wakiendelea kuhudumia ndoa na familia zao.

Tunawapongeza polisi na walinzi wa kampuni hizo, wanaokaa katika milango ya benki, wakiwalinda wanaoingia kuchukua au kupeleka maelfu kwa mamilioni ya fedha benki, huku wenyewe pengine wakiwa hawajui familia zao zitakula nini.

Tunawapongeza wanaotumikia vema mwito wao kwa kutotawaliwa na tamaa, majivuno au kiburi, na badala yake wanaendelea kuwa faraja kwa taifa.

Watanzania wanatamani na kutarajia kuona hata mgambo wote wakitenda hivyo hivyo na kuwa tija kwa taifa, ingawa ni bahati mbaya kuwa penye msafara wa mamba, kenge hawakosekani.

Wilayani Tarime ambako nako askari wa mgambo wanashirikiana na polisi kusaidia kuzuia uhalifu, kuna mingong’ono kuwa baadhi ya mgambo (si wote), wanajigeuza miungu kwa kutojali weledi.

Baadhi yao badala ya kufanya kazi kwa bidii kusaidia kuzuia na kukabili uhalifu na watakaofanya vizuri ili hata nafasi za ajira zikipatikana wapewe kipaumbele, wao wamekuwa kama kokoro kwa ‘kuzoazoa’ watu kupeleka polisi, huku wakijua kuwa wengine hawana dalili za uhalifu na hawajawakuta katika maeneo tata kiuhalifu. Hili si jambo jema.

Wanafanya hivyo wakati mwingine wakiwa wameambatana na polisi ambao wanafuata sheria na weledi. Hali hii ni hatari, kwani wanaweka hatarini heshima ya Jeshi la Polisi inayozidi kukua siku hadi siku.

Ndiyo maana ninasema Mkuu wa Wilaya ya Tarime ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) na Mshauri wa Mgambo wa Wilaya ya Tarime, unganisheni nguvu kukemea tabia hiyo, maana lisemwalo lipo na kama halipo, laja.

Mjue kuwa mgambo wachache wasio waadilifu na wasiozingatia weledi, wasipodhibitiwa wanaweza kuharibu kabisa heshima iliyotukuka ya polisi; na kibaya zaidi wanaweza kuambukiza sumu yao kwa baadhi ya polisi au mgambo wenzao, wanaotenda kiadilifu kwa weledi na kwa umakini.

Mgambo wenye tabia hiyo wadhibitiwe na kujua kuwa utendaji wao hauwezi kutukuka, kwa kuonea wasio na makosa,wakidhani wataonekana wachapakazi na kuajiriwa.

Wajengwe kujua kuwa kufanya hivyo, wanajifungia milango ya baraka na mamlaka zinawaona kwa mbali huku wakidhani hawaonekani.

Ndiyo maana ninasema mgambo wa Tarime, wasitake kuchafua heshima ya Polisi na wanaobainika kukosa utu, weledi na uadilifu, waenguliwe ili wasiambukize sumu kwa wengine.

Columnist: habarileo.co.tz