Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Messi hana kiu, Mbappe anacheka na akaunti yake

Lionel Messi Kylian Mbappe 1x7sh5n1pm0wy102tiuslo9e9r Lionel Messi na Kylian Mbappe

Sun, 12 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mwanamashairi mahiri wa zamani wa Uingereza, Joseph Addison aliwahi kusema: “Akili iliyoridhika ni baraka ambayo mtu anaweza kuifurahia maishani.” Ni kweli. Usoni sikuona, lakini moyoni niliona wakati Lionel Messi alipokuwa anaondoka Uwanja wa Allianz Arena, Jumatano usiku.

Halafu nikaitazama sura ya Kylian Mbappe usiku huo huo wa Jumatano wakati PSG ilipokuwa imetolewa na Bayern Munich katika usiku wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ilinikumbusha yule aliyesema kwamba; “Pesa sio kila kitu lakini ni afadhali ukiwa unalia ndani ya Benz kuliko ukiwa unalia huku unaendesha baiskeli.”

Kwa Messi, hawezi kutoka hadharani na kudai kwamba moyo wake umeridhika. Kama akihojiwa leo ataeleza ni namna gani ambavyo moyo wake umeumia kwa PSG kutolewa katika michuano hiyo.

Atadai kwamba ilikuwa ni ndoto yake kutwaa ubingwa wa Ulaya akiwa na PSG. Ukweli sio huu. Kwa sasa akiwa na PSG anacheza kwa juhudi, huku akitamani kufika anakofika lakini kama hatafika anajua wazi moyoni kwamba hana mambo mengi ya kupoteza.

Nafasi yake ipo huru na inafurahia maisha. Ametwaa Kombe la Dunia miezi michache iliyopita pale Qatar. Kuna kitu kikubwa kama hiki? Kuna deni kubwa zaidi lilikuwa linamkabili zaidi ya hili? Lakini kama ubingwa wa Ulaya basi Messi ametwaa mara nne akiwa na Barcelona.

Mwanadamu ana moyo ulioumbwa na nyama. Anaweza kujisukuma kadri anavyoweza lakini kuna sehemu ya akiba katika moyo wake au ubongo wake inaweza kumwambia; “Hapana, hiki umeshinda sio habari kubwa.”

Naamini Messi alisukumwa zaidi kutwaa ubingwa wa dunia na Argentina kuliko alivyotamani kutwaa ubingwa wa Ulaya na PSG. Kama ungemuuza swali hili miezi sita iliyopita angeweza kusema ukweli. Labda asingeusema kwa sababu PSG haijawahi kutwaa ubingwa wa Ulaya na mashabiki wake wana kiu.

Zaidi ya kila kitu. Naamini mafanikio ya Kombe la Dunia yatakuwa yameacha kumsukuma zaidi na zaidi katika vitu kama ubingwa wa Ulaya. Lakini pia Cristiano Ronaldo hayupo tena Ulaya. Kwanini aendelee kujisukuma zaidi na zaidi. Hawa Ronaldo na Messi walikuwa wanasukumana kwa namna fulani hivi. Na sasa mkataba wake umebakiza miezi mitatu tu ukate roho. Simuoni Messi akiendelea kucheza PSG.

Hata matajiri wenyewe wa PSG nadhani wataamka na kumuacha Messi aende zake. Wakati mwingine ni vigumu kukaa na mtu aliyeshinda kila kitu na ifikapo Juni 26 atatimiza miaka 36.

Messi anaweza kumfuata Ronaldo Saudi Arabia au anaweza kwenda Marekani kujiunga na timu ya David Beckham, Inter Miami ambayo amekuwa akihusishwa nayo kwa muda mrefu sasa. Anaweza kwenda kula pensheni yake huko kuliko kuendelea kukaa Ulaya na kukabwa na vijana kama kina Dayot Upamecano ambao damu yao inachemka.

Wakati nikiitazama sura ya Messi nilikumbana pia na sura ya Mbappe. Alikuwa anaondoka uwanjani akiwa na fadhaha. Angefanya nini zaidi kuipeleka PSG robo fainali? Afanye nini zaidi kuipa PSG ubingwa wa Ulaya? Amepambana akiwa na Neymar, akaendelea kupambana akiwa na Messi lakini mambo bado yanakataa.

Katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto alikuwa na nafasi ya kuamua kuupata ubingwa wa Ulaya kwa urahisi. Mkataba wake ulikuwa umemalizika pale Paris. Real Madrid walikuwa na mkataba mzuri kwake, lakini zaidi ni kwamba alikuwa na nafasi nzuri ya kushinda ubingwa wa Ulaya akiwa na Real Madrid kuliko PSG.

Wahispaniola walikuwa wanamsubiri akawe alama ya Real Madrid, lakini awe alama ya soka la Hispania kwa sasa. Mwishowe maamuzi ya pesa yalimshinda nguvu. Naambiwa kwamba yeye kama yeye alipewa kiasi cha Euro 100 Milioni kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea PSG.

Na baada ya hapo ana mshahara wa Euro 500,000 kwa wiki pale Paris. Kwa namna ambavyo Waarabu wa leo wana pesa Florentino Perez alizidiwa kete. Yeye na La Liga wakaishia kulalamika tu. Mbappe akaamua kuitukuza akaunti yake kuliko mambo ya ubingwa wa Ulaya.

Sio kwamba Real Madrid inakuhakikishia ubingwa wa Ulaya, lakini wote tunafahamu kwamba wakati mwingine ubingwa wa Ulaya huwa unaifuata Real Madrid. Ni kiurahisi tu. waliwahi kuuchukua miaka mitatu mfululizo katika zama hizi za Zinedine Zidane huku watu tukishangaa katika namna ambavyo walikuwa wanauchukua.

Wakauchukua tena chini ya Don Caro katika namna ambayo wote tuliishia kushangaa tu. Na tayari wametoka Anfield kufanya mauaji huku wakitabiriwa kuendeleza kitu kile kile katika mechi ya marudiano Santiago Bernabeu katikati ya wiki ijayo.

Ina maana kwamba wakati huu PSG wametolewa, Mbappe angekuwa na kina Karim Benzema, Vinicius Jr, Luka Modric na wengineo wakisaka taji la Ulaya ambalo mara nyingi huwa linawafuata. Hata hivyo yeye aliamua zake kuchagua pesa.

Mara zote Real Madrid hata kama hawapo sawa bado wapo hatua nyingi kutwaa ubingwa wa Ulaya kuliko PSG na hata Manchester City. Uzuri ni kwamba kuna wakati wachezaji wetu wanapewa chaguo la kuamua na wengi kati yao wanaamua kuchagua pesa.

Wakati Mbappe alipokuwa anaondoka uwanjani pale Allianz Arena nadhani atakuwa mnafiki kujilaumu kwanini aliamua kuongeza mkataba mpya na PSG. Alijua ambacho angeweza kupata Real Madrid na alijua ambacho angeweza kupata akiwa na PSG.

Hadi sasa kuna timu mbili ambazo zina pesa zaidi, lakini hazina ukomavu wa kiakili wa kutwaa ubingwa wa Ulaya. PSG na Manchester City. Wana sababu nyingi za kisoka za kutwaa ubingwa wa Ulaya, lakini hawana ukomavu wa kiakili.

Kuna klabu ambazo hata kama hazina pesa sana, lakini zina ukomavu wa kiakili wa kutwaa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Liverpool, Real Madrid, Barcelona, Juventus na wengineo wachache ambao wamewahi kutwaa taji hili zaidi ya mara tatu.

Mbappe amemua kutoa machozi yake akiwa ndani ya Mercedes Benz. Sio jambo baya sana kwa sababu alifanya chaguo lake mwenyewe. Haijulikani ni lini PSG watatwaa Kombe la Ulaya. Anachoweza kujifajiri ni kwamba kama ilivyo kwa Lionel Messi basi na yeye ametwaa Kombe la Dunia. Hatuwezi kumsema sana.

Columnist: Mwanaspoti