Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mengi yanachangia kuwepo kwa watoto wa mitaani

5ea5b647dcd3c55aefa1e70ea3cd22f1.png Mengi yanachangia kuwepo kwa watoto wa mitaani

Mon, 28 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“KILA siku baba na mama walikuwa wakienda kilabuni na kurudi usiku wamelewa. Baba akawa anampiga mama eti ni malaya na siku nyingine baba anatupiga na sisi (watoto) na kutufukuza akisema eti sisi siyo watoto wake.”

“Mama alipoona mambo yanakuwa mengi, akatoroka; nasikia alikwenda Kenya na ndipo baba akaoa mwanamke mwingine… Huyo mwanamke akawa kila siku baba akirudi usiku, anamwambia eti anatutuma tunakataa; hatumheshimu ni afadhali waachane arudi kwao.”

Ndivyo anavyosema Jerome Kitiku (siyo jina halisi) ambaye ni mmoja wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani maeneo ya Kariakoo jijini Dar es Salaam. Anaongeza kuwa, kitendo cha mama yao wa kambo kuwasingizia mambo huku akiwanyima chakula yeye na mdogo wake, Salome, ndicho kilichowafanya waamue kutoroka kutoka nyumbani kwao Bahi kwenda Dodoma mjini na kisha kuhamahama hadi sasa wanaishi mitaani katika Jiji la Dar es Salaam.

Jerome na Salome wanaoishi na kufanya kazi katika mitaa taofauti ya Kinondoni na Ilala katika jiji hilo, ni miongoni mwa watoto wanaolazimika kutoka katika familia zao kwenda kuishi mitaani na kujihusisha na shughuli hatarishi kwao katika maneo mbalimbali ya miji kama Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Dodoma, Sumbawanga, Iringa na Mbeya kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo migogoro na ulevi wa kupindukia wa wazazi.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa HabariLEO, wakiwa mitaani watoto hao hukumbwa na adha mbalimbali zikiwamo za matusi, kupigwa, kubakwa na wengine kulawitiwa. Ni katika muktadha huo wapo wanatumbukia katika janga la kutumiwa kwa biashra ya ngono na uuzaji wa dawa za kulevya, kulala kwenye mitaro au vichochoro kukosa uhakika wa chakula na wengine kulazimika kula mabaki ya vyakula yaliyotupwa jalalani na kukosa huduma muhimu za kijamii kama afya, elimu na malazi.

Kwa mujibu wa Meneja Uchechemuzi wa taasisi inayopambana na ongezeko la watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani ya Railway Child Africa (RCA), Rose Kagoro, uwepo wa wazazi waliozaliwa, kukulia na kuzalia mitaani ni sababu nyingine inayochangia kuwapo watoto hao wanaoishi na kufanya kazi katika mazingira hatarishi.

Sababu nyingine ni baadhi ya watoto kudhani kwamba mitaani kuna uhuru wa kufanya lolote walitakalo na kwa wakati wowote, pamoja na kudhani kuwa huko mitaani kuna fursa ya haraka kupata pesa ama kwa kufanya kazi, au kwa kuomba kwa watu na kwa wafanyabiashara wakiwamo wa maduka na hoteli.

Rose anasema: “Watoto hudhani mitaani kuna fursa kwao kupata fedha haraka na hivyo kuvutiwa na uhuru wa kwenda wanakotaka kwani wanajua kwa mfano, maeneo ya Kariakoo (Dar es Salaam) siku fulani eneo fulani wafanyabiashara wanatoa pesa au chakula kama sadaka yao, hivyo wanakwenda popote.”

Rose alikuwa akizungumza katika warsha ya siku moja kwa wahariri na wandishi wa habari waandamizi iliyofanyika Sinza Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya RCA Tanzania katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2020 katika kuwahudumia watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya, Iringa na Mwanza.

Akafafanua kwamba sababu nyingine ya watoto kuishi, kuomba na kufanya kazi mitaani kuwa ni migogoro inayosababisha wazazi kutengana na watoto kupata ugumu maisha na mateso kutoka kwa ndugu wengine hasa mama na baba wa kambo; pamoja na baadhi ya wazazi na walezi kukosa muda wa kukaa na watoto wao ili kuimarisha uhusiano baina yao.

Katika ufafanuzi wake Rose anasema: “Watoto wengine wanaishi na kufanya kazi mitaani kwa kuwa wazazi wao hasa mama zao, walikuwa watoto wa mitaani, waliwazalia mitaani na hata sasa wanaishi huko huko mitaani, hivyo watoto wanazaliwa, kukulia huko na kuona ndiko wanapostahili kuishi na kufanya kazi,” anasema.

Anaongeza kwamba wangine wamezaa watoto huko, watoto wao nao wakazaa huko na kupata wajukuu huko huko, hivyo kizazi chote kinakuwa cha huko mitaani. Anaongeza: “Watoto ambao bibi, mama na wao wenyewe wamezaliwa na kukulia mitaani, ni vigumu kuwaondoa huko…”

Kuhusu uhuru na kudhani kuwa mitaani kuna fursa ya kupata fedha, katika mijadala yao washiriki walisema kitendo cha watoto hao kuamua kwenda mahali popote kwa mfano, asubuhi kuwa Kivukoni au maeneo ya Posta, mchana kuwa Magomeni na jioni au usiku kuwa Kariakoo kutegema na vuvitio mbalimbali siku hiyo, huwafanya wapotee kwa kudhani mitaani ni kuzuri.

Mmoja wa washiriki anasema: “Unajua huko mitaani, wanajua kwa mfano siku za Ijumaa, kuna maduka na hoteli ambapo wamiliki wanatoa pesa kwa wanaoomba kama sadaka, na maeneo mengine zipo siku watu wa huko wanatoa vitu kama chakula mfano wali kwa waombaji wakiwamo watoto hao hivyo, wanaona mitaani wana gfursa na uhuru wa kwenda huko bila kipingamizi na kupata vitu hivyo.”

Rose anasema kutokana na watoto hao kukumbwa na masaibu mbalimbali huku hali hiyo ikipunguza nguvu kazi ya taifa, RCA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wamekuwa wakifanya juhudi kuwafikia na kuwasaidia kwa namna mbalimbali.

Anasema ingawa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inataka mzazi amlee na kumtunza mtoto, moja ya changamoto kubwa inayowakumba RCA na wadau wengine wanaopambana kuunganisha au kuwarudisha watoto hao na familia zao, ni baadhi ya wazazi kukataa kuwapokea watoto wao wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

“Hiyo ni changamoto kubwa maana hata kama sheria ipo, lakini sisi kama sisi, hatuwezi kulazimisha wazazi au walezi hao kuishi na mtoto maana hiyo inaweza kumfanya mtoto akawa katika hatari na uwezekano wa kudhurika zaidi,” anasema Rose.

Anaendelea: “Tumebaini kuwa mtoto aliyekaa mitaani kwa miaka mitatu, minne au zaidi, ni vigumu kumrudisha nyumbani kwani anakuwa amezoea maisha yake na ukimlazimisha kwa mfano kumpeleka Musoma, kabla wewe hujafika Dar, unaweza sikia ametoroka na sasa anakwenda kwingine.”

Anapozungumzia wanachokifanya kusaidia watoto hao, Rose anasema: “Tunawabaini na kuwasaidia kisheria hasa watoto wanaokuwa wamekinzana na sheria, au waliofanyiwa ukatili kama kupigwa, kubakwa au kulawitiwa na kisha kuwatoa katika mazingira hayo kuwapeleka mazingira salama ili wasidhuriwe na wanaotaka kupoteza ushahidi.”

Anasema katika kipindi cha miaka cha 2017 hadi 2020, wamefanikiwa kuwaunganisha na familia zao watoto 1203 sawa na asilimia 74 ya walengwa 1620. “Katika mazingira hayo, familia 783 sawa na asilimia 80 ya familia lengwa 983, zimeboresha uhusiano na watoto hao nyumbani huku familia 638 sawa na asilimia 66 ya familia 972 zilizokusudiwa, zikiwa zimeboresha kipato.”

Watu mbalimbali wanapendekeza kuwa ili kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la watoto kuishi na kufanya kazi mitaani, jamii iungane kuwapa malezi, usaidizi na upendo watoto waliofiwa wazazi (yatima) ili wajione bado wapo katika ‘mikono salama’ duniani.

Wanasema familia ziishi kwa upendo na kujali maisha ya watoto huku elimu zaidi kuhusu Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, ikitolewa ili pamoja na mafundisho ya dini, wazazi waone ufahari kuwapenda na kuwajibika kuwalea watoto wao na kuwasaidia kwa kila namna au kila mazingira.

Watoto wanaoondolewa mitaani, wapokewe vizuri katika jamii, badala ya kutengwa. Nadharia iitwayo kwa Kiingereza ‘Labeling Theory’ ya Mwanasosholojia wa Marekani, Howard S. Becker mwkaa 1963 inasema mtu anayechukuliwa na jamii kama mhalifu kiasi hata cha kutoshirikiana naye ipasavyo, huwa katika hatari kubwa zaidi ya kuendelea na uhalifu ama iwe mwanzoni alikuwa mhalifu, au la.

Kwa msingi huo, washirikishwe katika mambo na shughuli za kijamii kama watu wenye mchango wa kujenga jamii huku wakioneshwa upendo kwani hata kama walifanya kosa, watabadilika na kufuata utaratibu unaokubalika kijamii katika maisha. Taasisi na jamii zifanye kama inavyofanya RCA kwa kuwaanzishia na kuwasaidia kuendeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na hata kuziwezesha kiuchumi familia zao zenye kipato duni ili ziimarike na kujenga mshikamano.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, iendelee kutoa miongozo ya namna ya kuwasaidia watoto hawa ili baadaye, watoe mchango wao kujenga taifa na jamii kwa jumla.

Columnist: habarileo.co.tz