Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mchezaji samba Bruno Gomes anafikirisha mambo mengi

Bruno Gomes Singida Big Kiungo mshambuliaji wa Singida Big Stars, Bruno Gomes

Wed, 8 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo Mbrazili wa Singida, Bruno Gomes amenifikirisha mambo mengi. Mengine ya kijinga mengine ya maana. Ameendelea kutamba katika Ligi Kuu kwa mara nyingine tena. Juzi alimtungua Aishi Manula bao maridadi la mpira wa adhabu tukaishia kumkubali tu. Tungefanya nini zaidi?

Bruno alikuwa ananikumbusha kitu ambacho nchini kimekuwa cha nadra tofauti na zamani au kwa wenzetu. Hili linaweza kuwa bao lake la nne la mpira wa adhabu. Kifupi ni Bruno ni mtu hatari kwa kazi hiyo ya kupiga mipira iliyokufa. Waingereza wangemuita specialist.

Hapa nchini specialists wamepotea. Bruno inaonekana anajua anachokifanya. Labda alifundishwa huko alikotoka au labda ni kipaji chake maalumu. Tanzania hatuna watu ambao wamebobea katika jambo moja. Kwa mfano, Bernard Morrison tangu awafunge Simba mpira ule wa faulo hajarudia tena kupiga vile wala kufunga vile.

Soka letu la leo halina watu maalumu kwa ajili ya kazi maalumu. Zamani Abeid Mziba alibobea kwa mipira ya vichwa. Zamani Ally Malilo ‘Loketo’ wa Sigara alibobea kwa mipira ya kona. Lakini hapo hapo kuna watu waliokuwa wamebobea kwa mashuti kama kina Rajab Risasi. Mao Mkami aliyebobea kwa penalti.

Ulaya na tuliwaona wachezaji kama David Beckham, Sinisa Mihajlovic, Juninho Pernamucano na wengineo wakiwa wamebobea kwa mipira ya adhabu. Mpaka leo tunaona akina Jorginho na Mario Balotelli wakiwa wamebobea kwa mipira ya penalti. Bruno anatukumbusha kwamba Ligi lazima iwe na wataalamu wa kazi mbalimbali.

Bruno amenikumbusha kitu kingine. Hivi Mheshimiwa Mwigulu Nchemba amemtoa wapi? Kama kuna mtu anamfanyia Mheshimiwa kazi ya kutafuta wachezaji basi huwa anaifanya vema kuliko hata kwa wakubwa wetu. Wachezaji wake wengi wa kigeni anaowaleta nchini anakuwa amepatia, Bruno anatukumbusha ukubwa wa dunia.

Dirisha kubwa lililopita mbio nyingi zilikwenda kwa Stephane Aziz Ki, Kisa? Yanga na Simba zote zilimuona katika mechi za ASEC, kama wasingemuona katika mechi zile si ajabu leo Aziz asingekuwepo nchini. Limetokea jambo hilo mara nyingi, kina Luis Miquissone, Perfect Chikwende na wengineo tuliwasajili baada ya kuonyesha makali yao uwanja wa Mkapa au katika viwanja vyao wakati wanacheza na timu zetu.

Moses Phiri hatimaye alitua nchini lakini huyu ni mchezaji ambaye Simba na Yanga zilimsaka misimu mitatu nyuma, hazikuganduka kwake mpaka Simba ilipokuja kumpata, hii ina maana macho yalipoganda kwake hatukujaribu kupepesa sehemu nyingine. Ndivyo tulivyo mara zote.

Bruno anatukumbusha tu tunaweza kuifungua dunia na kupata wachezaji wengi tofauti katika kila pande ya dunia. Hata hivyo, kwa uvivu wetu bado tutarudi kukimbizana kwake mwishoni mwa msimu baada ya kujaribu kuiba mtandao wa Mheshimiwa Mwigulu katika kusaka wachezaji. Ndivyo tulivyo mara zote. Lazima wakubwa wataanza mbio za kuinasa sainiya Bruno mwishoni mwa msimu.

Kitu kingine ambacho Bruno amenifikirisha ni namna anavyoweza kucheza katika nafasi tofauti. Alianza kucheza kama kiungo mkabaji akawa bora. Sasa hivi anahamia mbele na anaendelea kuwa bora. Si ajabu akachezeshwa kama beki wa kulia na akawa bora zaidi.

Wachezaji wa namna hii wametoweka nchini, zamani alikuwepo mchezaji kama Said Mwamba, alikuwa anaweza kucheza kama mshambuliaji na anafunga. Akacheza kama kiungo akawa kiungo maridadi kweli kweli, halafu akarudishwa kucheza beki wa kati na ungeweza kudhani alikuwa beki asilia.

Hawazaliwi tena wachezaji kama Mwamba hapa nchini, sio tu kwamba alikuwa anacheza hizo nafasi ili mradi anacheza, hapana. Alikuwa anazicheza kwa ufasaha. Mwingine ambaye angeweza kufanya hivi ni Hamis Thobias Gaga ‘Gagarino’. Angeweza kucheza nafasi nyingi uwanjani kwa ufasaha ule ule.

Kwa sasa wanaoweza kutuletea haya mambo ni wageni, yupo huyu Bruno ambaye sasa amehamia mbele na anacheza kwa ufasaha, halafu yupo Yannick Bangala ambaye sioni tofauti yoyote ya kiuweledi akicheza kama kiungo ama beki wa kati. Anacheza katika ubora uleule. Zamani tulikuwa na wachezaji hawa lakini siku hizi nadhani hawazaliwi tena.

Kitu kingine ambacho sio maana sana lakini najisikia kukukumbusha ni namna gani wenzetu wametuacha mbali. Hii najikumbusha kila siku. Unafahamu Wabrazili hawajui kama kuna mchezaji wao anaitwa Bruno na anakaribia kuchukua tuzo ya mwanasoka bora wa msimu hapa Afrika Mashariki na Kati?

Huyu ni mtu ambaye taifa lake tunaishi nalo katika ulimwengu mmoja, kuna nyakati ambazo na sisi tunatamani kwenda Kombe la Dunia tukacheze na hao kina Brazil. Lakini jaribu kufikiria namna ambavyo tunaishi nao katika dunia tofauti linapokuja suala la kuwa na vipaji maridhawa.

Brazil haijui kama Bruno yupo hapa, inaweza kupanga vikosi 20 vya wachezaji wa timu zao za taifa vyenye wachezaji 40 na Bruno asifikiriwe.

Huku kwetu Bruno angekuwa panga pangua katika kikosi cha kwanza cha kocha yeyote wa Taifa Stars. Ni mchezaji gani angemuweka Bruno nje katika kikosi cha Taifa Stars?

Na hii si tu kwa Tanzania. Bruno angeweza kuanza katika vikosi vya Uganda, Kenya, Malawi, na kadhalika. Ukiwaza kufikiria tunaota kucheza Kombe la Dunia jaribu kufikiria mataifa yenye wachezaji wa kulipwa waliotapakaa kila kona na hawaitwi katika vikosi vyao vya timu ya taifa wakati sisi asilimia 95 ya wachezaji wa Stars wanacheza nyumbani.

Hili la Bruno halipo kwa Brazil tu. Mara ngapi nikumbushe wachezaji wa kigeni ambao moja kwa moja wangeingia katika kikosi cha Taifa Stars na kwao hawafikiriwi kuitwa. Bernard Morrison ni mmoja kati ya wachezaji wa aina hiyo. Hapa nchini ni staa lakini Ghana hawafikirii kama kuna mchezaji wa aina hiyo anacheza nchini.

Kitu cha mwisho ambacho kinanifikirisha ni wapi Bruno anacheza. Ametoka kwao Brazil kuja katika nchi ya dunia ya tatu kusaka maisha. Anacheza wapi? Singida. Anaishi wapi? Singida. Hawa jamaa kama Wanigeria tu au wachezaji wa Afrika Magharibi. Huwa hawachagui sehemu ya kuweka kambi.

Wanaweza wakaishi popote ili mradi watafute njia. Hapo ambacho Bruno anakisaka ni njia tu. Anaweza kuwa anasaka njia ya kuja timu kubwa za nchini, au Afrika au Ulaya. Kitu cha kwanza cha msingi ni kusaka njia kwanza kabla ya mambo mengine.

Columnist: Mwanaspoti