Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mchakato kura za maoni usiwagawe wanachama

454e4889a895266a35566055270dbfc0 Mchakato kura za maoni usiwagawe wanachama

Wed, 22 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

DUNIA hivi sasa imeweka macho na masikio Tanzania, ikifuatilia kwa karibu michakato mbalimbali ya kisiasa, inayoendelea ndani ya vyama kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Pazia kwa nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani, limefunguliwa katika vyama vingi vya siasa na baadhi vimeamua kuweka mchakato wa kuwapata wagombea kuwa wa wazi zaidi, ili kuimarisha haki na usawa kuanzia ngazi ya chini ambayo ndio msingi wa demokrasia.

Chama kilichoamua kuendesha kura zake katika mchakato wa kura za maoni kwa uwazi ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndicho chama tawala. Hatua hii imeelezwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa ni kubwa, yenye kudhihirisha demokrasia ya kweli, haki na usawa kwa wagombea.

Aidha, mchakato wa kura za maoni pia unaendelea katika vyama vingine nchini, kikiwamo chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho tumeshuhudia baadhi ya wabunge wakitetea majimbo yao katika kura hizo za maoni.

Hatua hii ya kura za maoni ni ya awali katika kuwapata watu makini, wenye uwezo na sifa stahiki, watakaopeperusha vyema bendera za vyama vyao ili kupata ushindi na kuwatumikia wananchi katika nafasi walizoomba.

Nafahamu kuna mchakato mrefu, kwa kila chama kumchagua mgombea mmoja kati ya mamia ya waliotangaza nia na kuchukua fomu kuomba ridhaa katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo urais, ubunge, uwakilishi na udiwani.

Kwa mfano, kwa mara ya kwanza ndani ya vyama vya siasa mwaka huu tumeshuhudia utitiri wa watangaza nia katika jimbo moja kwa mamia ya watu. Mfano mzuri ni CCM ambako kwa nchi nzima wanachama zaidi ya 10,000 walitangaza nia na kuchukua fomu kuomba ridhaa ya chama kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali. Hali hii imejitokeza pia Chadema kwa baadhi ya majimbo.

Kama nilivyosema awali, mchakato huu wa kura za maoni unapaswa kutazamwa, kama hatua ya awali ya kidemokrasia ndani ya chama na kamwe usiwagawe wanachama, bali kila mgombea ambaye kura hazikutosha, akumbuke dhana isemayo kuwa ‘Asiyekubali kushindwa si mshindani’.

Tukumbuke hata wanafunzi darasani, wanasoma pamoja lakini mtihani unapokuja, lazima kuwe na wa kwanza hadi wa mwisho na si kwamba wa mwisho hajui kitu. Natamani hatua hii iimarishe vyama kwa kuwaweka wagombea na wanachama wote pamoja kumuunga mkono atakayechaguliwa.

Nasema hivyo kwa kuwa hakuna anayejua katika ngazi za kamati za taifa ndani ya vyama jina gani, litapendekezwa na kurejeshwa ili mhusika agombee nafasi hiyo kwa wananchi.

Wakati huu ndio mgumu zaidi, hasa kutokana na ukweli kwamba mtu anaweza kushinda kura za maoni jimboni, lakini ikajulikana alitumia fedha, hakubaliki kwa wananchi au ana kashfa ya rushwa, hivyo ikaonekana hawezi kupeperusha bendera ya chama kwa umma, akaachwa. Hili limewahi kutokea ndani ya CCM na bila shaka katika vyama vingine pia.

Binafsi, naamini siku zote katika dhana ya umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Kama kuna wakati wanachama wa vyama vya siasa nchini, wanatakiwa kuwa na umoja ni wakati huu wa mchakato wa awali wa kura za maoni.

Tuweke mbele Tanzania yetu na kuuacha 'umimi' pembeni ili kuupinga ubinafsi na kumuunga mkono, atakayechaguliwa ndani ya chama na mengine tuwaachie wananchi, kuamua nani wanamtaka kuwa kiongozi wao kwa miaka mingine mitano katika nafasi zitakazoshindaniwa.

Columnist: habarileo.co.tz