Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mbinu za kukuza mapato Hifadhi ya Jiolojia Ngorongoro Lengai

Fc86c686a4df885ef890882ddf50c717 Mbinu za kukuza mapato Hifadhi ya Jiolojia Ngorongoro Lengai

Tue, 19 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

APRILI 2018, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco), lilitangaza kuitambua Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kuwa Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai na hivyo, kuingizwa kwenye mtandao wa hifadhi zenye hadhi hiyo duniani.

Uchunguzi wa HabariLEO umebaini kuwa, Hifadhi ya Jiolojia ya Ngoromgoro Lengai inatambulishwa zaidi na uwepo wa Kreta ya Ngorongoro na Mlima Oldonyo Lengai. Vitu hivyo, ndivyo vinabeba jina la Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai.

Kadhalika, tamaduni zisizoathiriwa za watu wa eneo hili (Wamaasai) nazo ni kivutuio kikubwa kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo na hivyo, kuchangia kukuza uchumi na pato la wenyeji na taifa kwa jumla.

Kwa mujibu wa Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Urithi wa Malikale katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Joshua Mwankunda, hifadhi za jiolojia ni maeneo yenye urithi wa kijiolojia yenye umuhimu wa kidunia na kimataifa.

“Maeneo hayo huhifadhiwa ili kuyalinda dhidi uharibifu, kulenga kutoa mchango katika elimu ya sayansi, na maendeleo ya jamii inayoizunguka na pia, ni vivutio vya utalii ambavyo jamii inayoishi hapo hunufaika navyo kiuchumi,” anasema.

Anaongeza: “Utalii katika hifadhi za kiolojia umefanya watalii kuongeza idadi ya siku za kuwepo nchini, hivyo kuongeza mapato ya fedha.

Mwankunda anasema, mapato yanayotokana na utalii wa hifadhi ya jiolojia yameongezeka katika kipindi cha miaka mitano na kufikia Sh bilioni 2.5 mwaka 2020.

Anasema; “Katika kipindi cha mwaka 2014/15, mapato hayo yalikuwa kati ya Sh milioni 400 hadi 500, lakini mwaka 2019/20 yamefikia Sh bilioni 2.5.”

Katika moja ya mazungumzo na HabariLEO, Kamishina wa Uhifadhi wa NCAA, Dk Fredy Manongi anasema, hifadhi hizi za jiolojia zipo mbili barani Afrika. “Moja ipo nchini Morocco na hii ya Ngorongoro Lengai (Tanzania) ambayo ni ya kwanza na ya pekee katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara…”

Tanzania imejiwekea lengo la kuwafikia watalii milioni tano (5,000,000) ifikapo mwaka 2025 na hivyo, kulifanya taifa kupata Dola za Marekani bilioni sita kupitia sekta ya maliasili na utalii.

Hata hivyo, hivi karibuni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Aloyce Nzuki alifungua warsha ya siku mbili kati ya Menejimenti ya NCAA, wahariri na waandishi waandamizi wa vyombo vya habari iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa NCAA.

Katika ufunguzi huo, Dk Nzuki alionesha mshangao na kusema: "Asilimia 80 ya wageni (watalii) wanaokuja ni wapya, yaani ni asilimia 20 pekee ya watalii ndio wanapoondoka, hurudi kutembelea vivutio vyetu wengine, hawarudi...”

Alitaka kuwe na tafakuri makini mintarafu sababu za hali hiyo na namna ya kufanya ili wageni wanaokuja nchini, wakae siku nyingi na wanapoondoka, watamani kurudi tena na tena hali itakayoongeza pato litokanalo na utalii na pia, kuvifanya vivutio vilivyo Tanzania kutangazika zaidi ndani na nje ya nchi.

Kitendo cha mgeni kukaa siku nyingi nchini huongeza pato kwa kuwa hulipia malazi, chakula na kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma mbalimbali hali inayoongeza pato na kukuza uchumi.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa HabariLEO, upekee wa Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai duniani unachangiwa na matukio makubwa ya kiolojia yaliyotokea miaka mingi iliyopita na yanayoendelea kutokea hadi sasa yakiwamo maajabu ya mchanga unaohama kwa takriban mita 17 kila mwaka ukiwa na sura (umbo) ile ile ya nusu mwezi.

Mchanga huo unaelezwa kuwa ni kivutio kikubwa cha watalii wa ndani nan je ya nchi na pia hutumiwa na wenyeji (Wamasaai) kwa tamaduni na matambiko mbalimbali yakiwamo ya kuomba Baraka na kutoa shukrani.

Mwankunda anasema: “Hii ni sehemu ya upatanisho kwa jamii ya Kimaasai…”

Ofisa wa Urithi Utamaduni wa NCAA aliyepo eneo la Bonde la Oldupai, Godfrey Olemoita anasema mchanga huo uliotupwa na mlipuko wa Mlima Oldonyo Lengai yaani Mlima wa Mungu (Kimasai), ni sehemu inayoheshimika kwa wenyeji wa maeneo hayo hasa Wamaasai na wengi huenda kufanya ibada (matambiko) wakiongozwa na ‘wazee safi katika jamii.’

“Wenyeji wa maeneo hayo hufanya ibada na matambiko mbalimbali kuomba watoto; kwa wanawake ambao hawajapata watoto; wanakuja kuomba mvua na hata pia kuombea kutokuwapo kwa magonjwa yakiwamo ya mifugo na wengine huacha hata sadaka zao mbalimbali ambazo hata hivyo, siyo rahisi kuziona kutokana na mchanga huo kuhama,” anasema Olemoita.

Mwankunda anavitaja vivutio vingine miongoni mwa vingi vilivyo katika hifadhi hiyo kuwa ni pamoja na safu za miamba yenye miaka 500 hadi 800 inayojulikana kama Safu za Miamba ya Msumbiji na Bonde la Ufa. Bonde hili linayo matawi mawili, Bonde la Ufa la Mashariki (Tawi la Eyasi) na Bonde la Ufa la Gregory (Tawi la Natron Manyara).

Kwa mujibu wa chapisho na NCAA liitwalo Hifadhi-Jiolojia ya Ngorongoro Lengai, hifadhi hiyo ina utajiri mkubwa wa masalia ya viumbe hai wa kale.

Linasema: “Mabaki ya masalia haya yamehifadhiwa katika udongo wa majivu ya volcano iliyotokana na kulipuka kwa volcano za Milima ya Safu za Ngorongoro.”

“Katika vipindi tofauti, majivu ya volcano yalisafirishwa na upepo na kutupwa upande wa magharibi ya hifadhi katika Uwanda wa Serengeti.”

Olemoita anasema: “Maeneo muhimu na maarufu kwa kupatikana masalia haya ni Bonde la Olduvai na Laetori. Hayo ni pamoja na mabaki ya binadamu, wanyama, mimea, nyayo, michoro ya kwenye miamba na zana za mawe.”

Maeneo mengine ni Makumbusho ya Olduvai Gorge, Jabali la Nasera lenye urefu wa kimo cha mita 100 na mzingo wa mita 350; Kreta ya Ngorongoro; Bonde la Olkarien; Kreta ya Empakai; Mlima Oldonyo Lengai ambayo volkano yake bado ni hai.

Maoni ya wadau kukuza utalii

Wadau mbalimbali wa utalii waliozungumza na HabariLEO kwa nyakati tofauti wanasema, ili kuvutia zaidi wageni wapya na kuwafanya waliofika watamani kurudi, unahitajika umakini zaidi wa namna ya kuwahudumia.

Mmoja wa waandishi wa habari (hataki kutajwa), anasema: “Hifadhi ya Ngorongoro kwa mfano, ina vivutio vingi vyenye masimulizi mengi na ya kuvutia, mgeni akija, achague kivutio maalumu anachokitaka ili hicho, apate maelezo mengi na kwa undani ili ikibidi hata akaandike kitabu.”

Anaongeza: “Huyo akiondoka, atakuwa na hamu ya kurudi kwenda kwenye vivutio vingine ambavyo anavisikia na kuvitamani, lakini hajavifikia hivyo, akiondoka, atakuwa bado na hamu ya kurudi nchini na hili likifanyika vizuri, litachangia, kuwawezesha Watanzania kufikia lengo la mapato ya Dola za Marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025 kutokana na utalii.”

Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton anasema: “Kuwe na vifurushi maalumu vya utalii Ngorongoro…, badala ya mtu kuingia tu Ngorongoro, akamaliza vyote…”

Ikumbukwe kuwa, miongoni mwa faida za utalii wa jiolojia, ni pamoja na aina hiyo ya utalii kuongeza muda wa watalii kukaa nchini wakihamasishwa na kupata taarifa sawasawa.

Katika mada yake kwa warsha hiyo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi Mwankunda anasema: “Utalii wa jiolojia pia hupunguza msongamano wa watalii sehemu moja na badala yake, kuwafanya wasambae katika vivutio mbalimbali…”

Katika mazungumzo na gazeti hili, Mwankunda anasema, “Vyombo vya habari visaidie kutangaza habari chanya kuhusu hifadhi hii ili kuonesha tofauti na hifadhi nyingine. Kwa mfano, mtu aseme nikienda Serengeti, nitaona wanyamapori kama kule Ngorongoro, lakini nikienda hifadhi ya Ngorongoro, nitaona vitu vingi zaidi ya wanyamapori ukiwamo mchanga unaohama.”

Mkazi wa Wilaya ya Karatu, Naishok Saitoti akiwa na wanawake wenzake wawili kwa nyakati tofauti, aliungana na Manyerere kusema, ipo haja kuwa wataalamu wa lugha mbalimbali, badala ya kutumia tu, Kiingereza na lugha nyingine chache ambazo wataalamu wake nao ni wachache.

“Hii itawezesha wageni wengi kuona, kusikia na kuelewa vizuri zaidi na hivyo, kwenda kuelezea wengine wa kule kwao mpaka wale nao wapate hamu ya kuja,” alisema Naishok.

Kingine kitakachosaidia kuwafanya watalii kurudi na hivyo kuongeza pato la utalii ni kuwa na waongoza watalii na wasimulizi katika vivutio mbalimbali wenye sanaa ya kusimulia inayovutia, lakini isiyotoa taarifa tofauti, bali inayoongeza taarifa mpya zinazozidi kupatikana.

Kwa mujibu wa uchunguzi, wadau mbalimbali wanapendekeza kuwapo hamasa kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu kutembelea Hifadhi ya Jilojia ya Ngorongoro Lengai kwa kuwa hata malipo yake, ni ya chini; Sh 11,800 kwa Mtanzania.

Uwepo utaratibu maalumu utakaowezesha watalii wa ndani kupata huduma za usafiri na nyingine ndani ya hifadhi kwa gharama nafuu ili kuvutia wengi.

Vyombo vya habari viwe mstari wa mbele kupeleka habari njema nje ya nchi kuhusu utalii nje kupitia vipindi vya redio na televisheni pamoja na machapisho katika magazeti na mitandao ya kijamii.

Columnist: habarileo.co.tz