Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mbinu za Nabi ziliwaua Wasauzi

Yanga 2  Marumo Gallants Mbinu za Nabi ziliwaua Wasauzi

Sat, 13 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga imeendeleza moto wake msimu huu baada ya juzi kuweka mguu mmoja mbele kutinga Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuichapa, Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa mabao 2-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza hatua ya nusu fainali.

Yanga ilipata ushindi huo kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam na kuiofanya timu hiyo kujiweka karibu na nafasi ya kuandika historia ya kucheza fainali za CAf kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ilipoasisiwa mwaka 1935.

Katika pambano hilo ambalo lilishuhudia Wasauzi wakiibana Yanga kipindi cha kwanza na hata kwenye kipindi cha pili kwa umahiri wa kumiliki mipira na kutengeneza mashambulizi kwa akili kabla ya Kocha Nasreddine Nabi kupindua meza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji wanne kwa mpigo baada ya awali kumuingiza Joyce Lomalisa akimtoa Kibwana Shomary.

Mwanaspoti lilikuwa uwanjani kwenye pambano hilo na hapa nchini ni namna ambavyo pambano hilo la kwanza lilivyopigwa kwa Mkapa.

45 ZA KWANZA KINYONGE

Mashabiki wa Yanga walipata wakati mgumu kwenye kipindi cha kwanza kwa namna timu hiyo ilivyocheza kabla ya kubadilika kipindi cha pili na kupata ushindi huo uliowazogeza karibu kabisa na fainali za michuano ya CAF ikiwa ni rekodi kubwa zaidi kwa klabu hiyo.

Yanga ilitengeneza ushindi wake kupitia dakika 45 za kipindi cha pili baada ya kipindi cha kwanza kuwaashtua mashabiki wao wakishindwa kuonesha utulivu kutumia nafasi walizotengeneza.

Kipindi hicho cha kwanza Yanga ilipiga jumla ya mashuti 9 huku manne yakilenga lango lakini wakishidwa kuonyesha ukomavu wa kutulia kuweka mpira wavuni huku Marumo wakionekana kuwa makini kuhakikisha wanaituliza kasi ya wenyeji wao wakiweka malengo makubwa ya kumiliki mpira zaidi.

Mshambuliaji Fiston Mayele, mawinga Jesus Moloko na kiungo mshambuliaji Stephane Aziz KI wakiwa ndio vinara walioshindwa kutulia wakipoteza nafasi nyingi katika kipindi hicho cha kwanza wakionekana kucheza kwa presha zaidi.

SURA MBILI ZA NABI

Kuna Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi wa kipindi cha kwanza na Nabi wa kipindi cha pili hawa ni watu wawili tofauti kwani Yanga ambayo inarudi kipindi cha pili kama hujajishika vizuri unaweza kudhalilika kwa kipigi kikali hilo liliendelea pia juzi.

Kipindi cha pili Yanga ilirudi kwa kasi ikifanya mabadiliko wakimtoa beki wao wa kushoto aliyeanza Kibwana Shomari nafasi yake ikichukuliwa na Joyce Lomalisa ambaye ni mahiri wa kupandisha mashambulizi tofauti na Kibwana ambaye amekuwa bora kwa kuzuia.

Yanga ilionekana kuridhika na jinsi walivyowabana Marumo katika kipindi cha kwanza na kurudi na akili ya kutafuta ushindi mababadiliko ambayo yalizaa matunda dakika ya 64 wakipata bao lao la kwanza kwa winga wao Tuisila Kisinda ambaye alirudi na kasi nzuri akimwekea pasio safi mfungaji Aziz KI na kumfunga kwa akili kubwa kipa wa Marumo Washngton Arubi.

Dakika moja baada ya bao hilo Nabi hakujali Kisinda wala Aziz KI kutengeza na kufunga bao hilo aliwatoa katika mabadiliko ya watu wa nne kwa pamoja akiwatoa wawili hao pamoja na Yannick Bangala na Jesus Moloko kisha nafasi zao kuchukuliwa na Salum Aboubakar 'Sure Boy' Clement Mzize, Bernard Morrison na Mudathir Yahya.

Katika mababaliko hayo licha ya Yanga kuongeza presha ya kusaka bao la pili huku pia wakiongeza uimara wa watu wa kukaba waliingiza bao la pili lililofungwa na Morrison katika dakika za mwisho.

YATIBUA REKODI MARUMO

Katika mechi nne zilizopita za ugenini katika mashindano hayo Marumo wamefanikiwa kupata bao lolote kwenye mechi tatu lakini jana wakakutana na sapraiz baada ya kutolewa kapa kwa mara ya pili msimu huu.

Yanga inaungana na USM Alger ya Algeria walipowachapa Marumo kwa mabao 2-0 katika mechi za hatua ya makundi kipigo ambacho juzi kilijirudia hatua ambayo itawatibulia kuelekea mchezo wa marudiano.

UKUTA YANGA BALAA

Yanga imecheza jumla ya dakika 540 bila ukuta wao kuruhusu bao ambazo ni sawa na mechi 6 mfululizo na kuonyesha ukomavu mkubwa katika safu yao ya ulinzi chini ya mabeki Djuma Shaban, Joyce Lomalisa Kibwana Shomari , Dickoson Job, Kibwana Shomari, nahodha wao Bakari Mwamnyeto ambao wamekuwa wakipishana katika mechi hizo na kipa wao Djigui Diarra.

Mchezo wa mwisho Yanga kuruhusu bao ilikuwa pale jijini Bamako nchini Mali walipotoa sare ya bao 1-1 ambapo baada ya mechi hiyo hakuna ambaye amefanikiwa kushangilia bao dhidi ya timu hiyo hatua ambayo itaipa wakati mgumu Marumo kuelekea mechi ya marudiano kutimiza malengo yao ya kutakiwa kuifunga Yanga mabao 3-0 ili wafuzu.

Kazi nyingine kwa Marumo katika mpango wao huo wa kufuzu utakumbana na wakati mgumu wa kuizuia safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo ni mechi moja pekee kati ya 7 zilizopita imewshindwa kufunga bao walipocheza nyuymbani dhidi ya Rivers United.

YANGA KAZI IPO HAPA

Yanga inatakiwa kujipanga kuhakikisha wanatafuta dawa ya kuwatuliza viungo wa Marumo na safu yao ya ushambuliaji maeneo ambayo yatakuwa na makali zaidi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Mei 17 kule Afrika Kusini.

Hakuna kinachoshindikana chini ya jua Yanga inatakiwa kutambua kwamba bado mechi haijamalizika kwani Marumo inarudi nyumbani katika uwanja ambao wamewahi kushinda mabao 3-0 katika mechi za mtoano walipowatoa Al Ahly Tripol ya Libya kwa mabao hayo baada ya awali wasauz hao kupoteza ugenini kwa bao 1-0.

Marumo pia rekodi yao bora nyumbani wameshinda mechi zao nne zilizopita za shirikisho hatua ambayo inaiweka Yanga katika kuhitaji umakini zaidi kama wanataka kukamilisha ndoto yao ya kucheza fainali hiyo ya Afrika.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha Nasreddine Nabi licha ya kuonyesha kukerwa na jinsi timu yake ilivyocheza kipindi cha kwanza alisema bado timu yake ina kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wa marudiano akiwataka wachezaji wake kuongeza umakini.

"Sikufurahishwa tulivyocheza kipindi cha kwanza hatukucheza kama ambavyo jinsi tulivyoelekezana ingawa tumeshinda, hizi ni mechi ambazo tunatakiwa kuwa na akili kubwa ya kucheza kwa nidhamu kubwa , tuna kazi kubwa ugenini sitegemei tena makosa ya namna hii yatajirudia kule,"alisema Nabi.

Naye kocha wa Marumo, Dylan Kerr alisema kushindwa kwao kutumia nafasi na kupoteza umakini katika dakika za mwisho wakiruhusu bao la pili kumeufanya mchezo wa marudiano kuwa mgumu zaidi lakini watakwenda kujipanga tayari kwa mechi hiyo.

"Tulitengeneza nafasi nyingi lakini kitu kibaya tulishindwa kuzitumia, tumetoka bila bao leo (juzi), kuna wakati tulidhani kama tunakwenda kupoteza kwa bao moja lakini walipopata la pili kwa makosa yetu makubwa ya kujisahau limetuongezea ugumu zaidi, hatujakata tamaa tutakwenda kujipanga," alisema Kerr ambaye ni kocha wa zamani wa Simba.

Columnist: Mwanaspoti