Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mbegu za kiume huhifadhi virusi vya Ebola kwa miezi sita

Ebola Virus Mbegu za kiume huhifadhi virusi vya Ebola kwa miezi sita

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Imeelezwa kuwa mgonjwa wa Ebola akipona bado anaweza kuambukiza mtu mwingine ugonjwa huo kupitia mbegu za kiume na mwanamke anaweza kumwambukiza mtu mwingine kupitia matiti kwa kipindi cha miezi sita.

Ingawa ugonjwa huo haujachukuliwa kama maradhi yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana (ngono) katika baadhi ya tafiti, wataalamu wamebaini kuwa virusi vyake vinaweza kusambazwa kwa njia hiyo hata baada ya wagonjwa kupona.

Kutokana na hali hiyo hatua zaidi zimetakiwa kuchukuliwa ikiwemo tahadhari ikiwa ni siku 13 zimepita tangu kuripotiwa kwa mgonjwa wa mwisho katika nchi jirani ya Uganda, ambako ugonjwa huo umeathiri watu takribani 142 na kati yao 55 walifariki dunia tangu ulipozuka Septemba 20, mwaka huu.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Desemba 10, 2022 na Mratibu wa kukinga na kudhibiti maambukizi Wizara ya Afya, Dk Joseph Hokororo alipokuwa akitoa kwenye mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa Ebola.

“Vijidudu vya Ebola kwa mwanaume vinaendelea kuwa hai kwenye manii yake kwa zaidi ya miezi sita na hivyo ana uwezo wa kumwambukiza mwanamke atakayejamiiana naye bila kutumia kinga.

“Virusi vya Ebola husalia ndani ya mbegu za uzazi za kiume hata baada ya mgonjwa kupona kwa kuwa licha ya matibabu virusi hivyo haviwezi kuondoka kwa haraka katika manii na hivyo mgonjwa anaweza kusambaza virusi kwa mtu mwingine kwa njia hiyo.

“Kwa mwanamke anaweza kumwambukiza mtoto anayemnyonyesha kupitia matiti yake au iwapo mwanaume atanyonya matiti yake,” amesema Dk Hokororo.

Amefafanua kuwa maumbile ya virusi vya Ebola yanaipa uwezo wa kuishi kwa muda mrefu kwenye ubongo, uti wa mgongo, mbegu za kiume, nyumba ya uzazi na kwenye macho, hata baada ya mgonjwa kuthibitishwa amepona. Virusi hivyo vinaweza kuishi katika mbegu za kiume kwa muda mrefu kuliko majimaji ya mwili.

Amesema wanaopona ugonjwa huo hushauriwa kuhusu kipi wanatakiwa kukifanya na kipi wanashauriwa kutokufanya, kwani wanaweza kusababisha pia maambukizi kwa njia hizo ingawaje wanakuwa wamepona kabisa.

Dk Hokororo amesema iwapo mtu atapata maambukizi hayo hataweza kumwambukiza mwingine hadi pale atakapoanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo.

Akizungumzia unawaji mikono, mtaalamu wa kinga na kudhibiti maambukizi kutoka Jamii Bora Health Service Network, Said Chibwana amesema bado jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kunawa mikono ili kujikinga na ugonjwa wa Ebola pamoja na magonjwa mengine ambukizi.

Uganda itatangaza kukoma kwa ugonjwa huo zitakapopita siku 21 kuanzia kumtambua mgonjwa wa mwisho Novemba 27 mwaka huu.

Kuhusu Ebola

Ugonjwa wa Ebola unasababishwa na kirusi chenye anuwai tano zikiwemo anuwai za Zaire na Sudan ambazo ndiyo zinasababisha milipuko. Uchunguzi wa kimaabara umethibitisha kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola anuai aina ya Sudan (Ebola-Sudan strain) nchini Uganda.

Dalili kuu za ugonjwa huo ni homa kali, mwili kuchoka, kuumwa viungo vya mwili, vidonda katika koo, kuhara, na kutokwa damu katika matundu ya mwili yaani puani, mdomoni, masikioni, machoni na njia ya haja kubwa na ndogo hali inayosababisha kifo ndani ya muda mfupi.

Columnist: Mwananchi