Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mbappe, PSG ni jeuri ya kipaji dhidi ya noti

Mbappe Kiburi Kylian Mbappe

Sun, 30 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Aliwahi kuandika Mwandishi wa Gazeti la Daily Mail, Martin Samuel: "Kila mwanadamu anajisikia, tunatofautiana tu katika kiwango cha kuonyesha kujisikia kwetu.” Waingereza neno kujisikia linajulikana kama Ego.

Nimeshika rimoti, korosho zipo kando yangu. Glasi ya mvinyo ipo kando yangu. Nashuhudia pambano kali la kujisikia kati ya Mfaransa, Kylian Mbappe na Waarabu wanaomiliki Klabu ya PSG wakiongozwa na Rais wa klabu hiyo, Nasser Al-Khelaifi.

Kwa Mbappe nimetumia neno ‘Mfaransa’ zaidi ya staa. Naam, Wafaransa ni miongoni mwa wanadamu wanaojisikia duniani. Ndivyo walivyo. Ndivyo walivyoumbwa.

Mkataba wa Mbappe unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao Juni 2024. Katika hali ya kawaida klabu yenye mchezaji kama Mbappe, katika ubora wake na umri wake, inapaswa kumuongezea mkataba mwingine kabla hajafika mwishoni mwa mkataba wake.

Kabla hatujafikiria chochote kitakachoendelea baina yao, Mbappe alianzisha vita hii kwa kuandika barua ndefu kwamba ameamua kutoongeza mkataba wake na PSG pindi mkataba wake wa sasa utakapomalizika 2024.

Kauli hii iliwavuruga PSG. Walikuwa katika ligi. Kuanzia hapo PSG wakiongozwa na jeuri ya pesa ya Mwarabu walimwambia Mbappe kwamba alikuwa na machaguo mawili. Ama kuongeza mkataba mpya au kuuzwa.

Mbappe hataki kuchukua maamuzi yoyote kati ya haya mawili. Hataki kuondoka wala hataki kuuzwa. Haishangazi kwamba alianza mazoezi ya msimu mpya na PSG baada ya kumalizika likizo yake ya kula raha Marekani kisha akaenda kwa babu zake Cameroon.

Nia ya Mbappe inajulikana. Anataka kucheza Real Madrid. Lakini anataka kuisaidia Real Madrid kwa kuamua kwenda bure Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu ujao. Waarabu wanafahamu nia ya Mbappe.

Majuzi walianza kumuonyesha jeuri kwa kumuacha Paris wakati wao wakielekea katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya pale Marekani. Hii ilikuwa jeuri ya kwanza nzuri. Timu ya kinyonge ingeweza kuanza kucheza dansi la Mbappe lakini Waarabu waligoma.

Timu ya kinyonge ingembeba Mbappe hadi Marekani huku wakiendelea kumbembeleza asaini mkataba mpya. Si ajabu wangekubali Mbappe aanze msimu mpya kwao na mwisho wa msimu angeweza kuondoka bure. Waarabu hawana mpango huo. Walimuacha Paris na wakatangaza rasmi kwamba Mbappe anauzwa.

Nilijua ambacho kingefuata. Waarabu wakawapigia simu Waarabu wenzao wa Saudi Arabia kwamba Mbappe anauzwa. Klabu ya Al Hilal ikaweka mezani ofa ya uhamisho ambayo ingevunja rekodi ya uhamisho ya dunia. Pauni 259 milioni.

Lengo la Waarabu wa PSG lilikuwa kuhakikisha kwamba Mbappe haendi Madrid. Waarabu wa Saudia wakachukua nafasi hii. Unavunjaje rekodi ya uhamisho ya dunia kwa mchezaji ambaye amebakiza miezi 12 tu ya mkataba wake? Ni ukichaa lakini anaweza kushindana na noti za Waarabu kwa sasa? Tayari wanaendelea kufanya ukichaa mwingi kwa kulipa mishahara isiyoelezeka hapo Saudia.

Dau la mshahara ambalo Mbappe aliwekewa lilikuwa kufuru. Hata hivyo, naambiwa kwamba Mbappe hana mpango wowote wa kuisikiliza ofa ya Al Hilal. Ofa ya zaidi Pauni 600 milioni kwa mwaka kucheza kwao. Walikuwa tayari acheze hata kwa msimu mmoja tu. Mbappe amegoma.

Na sasa tunashika rimoti zetu huku tukiwa na korosho kando kujaribu kujua filamu hii itaishia wapi. Inasisimua sana na hasa ambapo Mbappe amekataa dili la kwenda Saudi Arabia. Nini kitafuata? Wasiofahamu ni kwamba hauwezi kulazimisha kumuuza mchezaji bila ya hiyari yake.

Mambo matatu yanaweza kutokea. Real Madrid inaweza kutoa dau dogo kwa ajili ya kumchukua Mbappe katika dirisha hili. Hakuna klabu yoyote ya Ulaya ambayo inaweza kuvunja rekodi ya uhamisho wa dunia kwa kuzingatia muda wa mkataba uliobaki kwa Mbappe. Ni Waarabu tu ndio ambao wamejaribu wazimu huo.

Yeyote ambaye atamtaka Mbappe kutoka Ulaya lazima ataweka mezani kiasi kidogo. Kinaweza kuwa Pauni 100 milioni tu kwa mchezaji aliyebakiza miezi 12. Hakuna ambaye ataweza kufikia wazimu wa Waarabu. Lakini pia kuna timu nyingine nje ya Real Madrid inaweza kumchukua kwa mkopo wa mwaka mmoja kabla hajaenda zake Madrid mwishoni mwa msimu.

Lakini kuna uwezekano pia PSG ikaamua kumlipa mshahara Mbappe na kumsotesha benchi mpaka mwishoni mwa msimu. Inaweza kumpeleka katika timu ya vijana na wachezaji wa akiba kumuonyesha kiburi chao.

Lakini hapo hapo kuna uwezekano Mbappe mwenyewe akawa tayari kukaa nje mpaka mwishoni mwa msimu. Hii ndio inaonekana nia yake kama dili lake la kwenda Madrid katika dirisha hili litashindikana. PSG itakubali? Ni suala la kusubiri na kuona.

Ninachofahamu ni kwamba wote wawili hawatakani. Alianza Mbappe kwanza. Alipoona amekosa ubingwa wa Ulaya kwa mara nyingine. Alipoona Lionel Messi ameamua kuondoka. Ameona timu haina mwelekeo. Aliishutumu timu baada ya kuondoka kwa Messi.

Nadhani amefahamu ni vigumu kupata ubingwa wa Ulaya akiwa na PSG. Anataka kwenda Real Madrid kwanza kwa sababu ya ukubwa wa klabu hiyo lakini pia anaamini atakuwa na nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa wa Ulaya na kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.

Wakati huohuo majuzi PSG imeonekana kuwa tayari kuishi bila ya Mbappe. Imetoa maneno mengi ya kejeli dhidi yake ikiwemo kudai kwamba timu tano zimechukua ubingwa wa Ulaya kwa miaka mitano iliyopita bila ya kuwa na Mbappe.

Nadhani wanataka kutengeneza timu katika mfumo mwingine bila ya kujaza mastaa wenye majina makubwa. Mradi wao wa kwanza wa kuwachukua Galacticos unaonekana umebuma na sasa wanataka kurudi katika miradi ya kawaida kama ile ya Manchester City. Wanachukua mastaa lakini sio wale wa viwango vya kina Neymar, Messi na Mbappe.

Na sasa tunasubiri kujua filamu hii itaishia wapi. Waarabu wanaonyesha jeuri ya pesa na kutojali. Mbappe anajivunia kipaji chake huku akionyesha pia Ufaransa wake. Mwisho wa siku hatujui ni nani hasa ambaye atashinda katika filamu hii. kila mmoja anaonyesha kuwa ‘sterling’.

Kila mmoja anaonyesha kujisikia. Ambacho ninafahamu ni kwamba mashabiki wengi wa PSG wapo nyuma ya uongozi wao. Wanamuona Mbappe ni msaliti mkubwa. Inapofikia hatua hii asilimia za Mbappe kubakia PSG zinakuwa chache. Tusubiri.

Columnist: Mwanaspoti