Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mastaa hawa wafungue mlango

Nondo Mayele Mastaa hawa wafungue mlango

Wed, 10 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kazi wanayo. Hawa ni baadhi ya mastaa wa Yanga wanaokosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho cha Yanga huku washindani wao wa namba hawana mchezo wawapo uwanjani, kutokana na ubora wao mkubwa kwenye timu.

Yanga kwa sasa ni bora na kocha Nasreddine Nabi anajaribu kumpa nafasi kila mchezaji, na kazi ni kwao kumshawishi kama wanastahili kucheza kikosi cha kwanza au lah, vinginevyo wanaweza kujikuta vipaji vyao vinashuka.

Ikumbukwe kwamba soka ni ajira inayolipa kwa wachezaji ambao viwango vyao vipo juu inakuwa rahisi kuonekana na kila timu, pia inawasaidia kuvuna mamilioni kwenye usajili wa kuhamia klabu mpya ama kuongeza mikataba mipya.

Mwanaspoti linakuletea mastaa wenye kazi ngumu kuhakikisha wanapenya kikosi cha kwanza cha Nabi vinginevyo watafute 'plan B' ya kunusuru uwezo wao kama wanavyoshauriwa na wataalamu wa soka.

JOHORA vs DIARRA

Kipa namba tatu, Erick Johora tangu ajiunge Yanga hajawa na bahati ya kuaminiwa kikosi cha kwanza ukiachana na ugumu wa kupata nafasi mbele ya Djigui Diarra waliokuja nyuma yake kama Abuutwalib Mshery alipata nafasi ya kudaka, baada ya kuumia wakamsajili kwa muda Metacha Mnata aliyedaka dhidi ya TP Mazembe na alifanya vizuri.

NINJA vs MWAMNYETO

Kama kuna eneo Nabi kafanikiwa kuliweka imara ni la ulinzi, awali kulikuwa na pacha kati ya nahodha Bakari Mwanyeto na Dickson Job, ambapo Abdallah Shaibu 'Ninja' ilikuwa ngumu kupenya katikati yao.

Ninja alikwamishwa na majeraha, baada ya kupona aliomba kwenda kwa mkopo Dodoma Jiji, kabla ya kurejea tena Jangwani mambo yake bado ni magumu. Huku na kule kaibuka beki mwingine Ibrahim Hamad 'Bacca' ambapo kuna wakati Job anakaa nje, hivyo endapo Ninja akiendelea kubaki Yanga atakuwa na kazi ngumu ya kumuaminisha kocha kwamba anastahili kuwepo kikosini.

NGUSHI vs MAYELE

Licha ya uwezo wa kushambulia akitokea pembeni kama winga wa kushoto au kulia, amekuwa akitumika zaidi kama mshambuliaji wa kati tangu akiwa Mbeya Kwanza eneo ambalo kwa Yanga amekuwa akicheza kinara wa mabao 16 Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele.

Crispin Ngushi amekuwa mbali na mipango ya Nabi kutokana na kusumbuliwa na majeraha kwa muda mrefu hivyo hata ambapo Mayele alitakiwa kupumzika, amekuwa akitumika Clement Mzize ambaye anafanya vizuri, hivyo kazi kwake kutoboa mbele yao.

AMBUNDO vs MOLOKO

Dickson Ambundo ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekalia kuti kavu kwenye timu hiyo, tangu ajiunge nayo akitokea Dodoma Jiji bado hajaonyesha thamani yake kiasi cha kuambulia kusugua benchi.

Nabi amekuwa akipendelea kuwatumia Farid Mussa, Tuisila Kisinda, Jesus Moloko na Barnard Morrison hata hivyo upo uwezekano wa kocha huyo raia wa Tunisia kuingia sokoni mwishoni mwa msimu ili kuongeza nguvu katika maeneo hayo kutokana na mahitaji ya timu.

Katika nafasi hiyo kuna Denis Nkane ambaye majeraha ni kama yamemrudisha nyuma, lakini angalau alikuwa anapewa nafasi ya kucheza, ambayo ingemjengea uzoefu.

BRYSON vs LOMALISA

Kwa namna nafasi ya beki ya kushoto ilivyo ndani ya Yanga, imekuwa ngumu kwa David Bryson kupata nafasi mbele ya Joyce Lomalisa na Shomari Kibwana, hivyo ana kazi ya ziada kuonyesha kipaji chake cha kuifaidisha timu.

Japokuwa akipewa nafasi anaonekana ni beki anayeweza kupiga mashuti ya mbali kama alivyofanya kwenye Kombe la Mapinduzi ambako alipewa nafasi ya kucheza.

NINI WAFANYE

Mchezaji wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogela anasema asilimia kubwa ya mastaa wanapata nafasi kwenye klabu kongwe wanajisahau na kuona wameishafika mwisho wa karia yao, wakisahau miguu yao imebeba mamilioni ya pesa.

"Kwanza mchezaji hapaswi kukubali kushindwa, yupo kwenye timu kwa ajili ya kushindana, pia wanapokosa nafasi waombe kwenda timu nyingine kwa mkopo ili wakarejeshe viwango vyao, wakionekana wanafaa watarejea tena," anasema.

Kauli yake iliungwa mkono na beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima anayesema; "Mchezaji anapofika Yanga na Simba lazima ajue anahitaji kufanya kazi ya ziada kwani ni timu zinazohitaji wachezaji wa viwango kutokana na kupata nafasi za kucheza kimataifa."

Columnist: Mwanaspoti