Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mastaa 94 kutoka nchi 22 Duniani ndani ya Ligi Kuu Bara

Mastaa Ligi Kuu 94 Mastaa 94 kutoka nchi 22 Duniani ndani ya Ligi Kuu Bara

Thu, 8 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara umejaa wachezaji wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali duniani tofauti na ilivyozoeleka katika miaka ya nyuma ambapo wachezaji wengi walikuwa wakitokea ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na nje ya eneo hilo.

Msimu huu imekuwa tofauti kwani kila timu kati ya 16 zinazoshiriki ligi hiyo zimejitahidi kufanya skauti na kusajili wachezaji na viongozi wa mabenchi ya ufundi kutoka maeneo mbalimbali.

Ukiachana na DR Congo pamoja na Burundi na mataifa mengine ya Afrika Mashariki yaliyozoweleka kujaza mastaa wao Bongo, msimu huu kuna wachezaji wamesajiliwa na timu za Ligi Kuu kutoka maeneo mengine duniani.

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea wachezaji 94 wa kigeni watakaokipiga Bongo msimu huu pamoja na nchi walikotoka.

DR CONGO

Nchi hii ndiyo kinara katika Ligi Kuu Bara msimu huu kwa kuwa na wachezaji wengi ikitoa mastaa 17 wamaokipiga katika nchi mbalimbali ambao ni Fiston Mayele, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Yanick Bangala, Tuisila Kisinda, Jesus Moloko na Heritier Makambo - wote wakikipiga Yanga.

Wengine ni Henock Inonga wa Simba, Idris Mbombo wa Azam, Carno Biemes wa Singida Big Stars, Mwana Kibuta na Randy Bangala wa Dodoma Jiji, Mukanisa Pembele wa Coastal Union, Mbaya Kayembe na Eric Yema wa Geita Gold, Alidor Kayembe wa Namungo, Pascal Kitenge wa Mtibwa Sugar na Papy Kabamba Tshishimbi ambaye msimu huu anakipiga Ihefu alikotua akitokea Kitayosce inayoshiriki Championship.

BURUNDI

Nchi hii msimu uliopita ndio iliongoza kwa kuwa na wachezaji wengi Ligi Kuu Bara, lakini msimu huu imepigwa bao na DR Congo na sasa ina mapro 13 ambao ni Amissi Tambwe wa Singida BS, Gael Bigirimana wa Yanga, Emiry Nimubona, Cedric Mavugo ‘Tity’ na Francis Mustapha wa Coastal Union, Jonathan Nahimana anayekipiga Namungo, Arakaza MacAthur na Said Ntibanzokiza ‘Saido’ wa Geita Gold, Styve Nzigamasabo, Bigirimana Blaise na Emmanuel Mvuyekure wa KMC, Matore Kalonda wa Mtibwa Sugar pamoja na Blanchard Ngabonziza wa Polisi.

UGANDA

Nchi hii inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na wachezaji wengi ikiwa nao 11 kwenye Ligi Kuu ambao ni Khalid Aucho wa Yanga, Nicholaus Wadada wa Ihefu, Shafik Batambuze wa Singida Big Stars, Ambrose Owio na Joel Madondo wa Polisi Tanzania, Mohamed Hassan wa Mbeya City, Deus Bukenya, Jackson Kibirige na Hamis Kiiza wa Kagera Sugar, Josseph Ssemuje wa Mbeya City na James Ssetuba anayeidakia Ihefu.

GHANA

Nchi hii inashika nafasi ya nne kati ya nchi zenye mapro wengi Ligi Kuu ikiwa na wachezaji tisa kwenye michuano hiyo ambao ni James Akaminko wa Azam, Bernard Morrison wa Yanga, Augustine Okrah wa Simba, Opare Collins na Christian Zigah wa Dodoma Jiji, Emmanuel Asante wa Namungo, James Kotei wa Mtibwa Sugar, Shawn Oduro wa Geita Gold na Nicholaus Gyan wa Singida Big Stars.

KENYA

Majirani, Kenya wanafuata katika nafasi ya tano wakiwa na wachezaji saba kwenye Ligi Kuu Bara ambao ni Kenneth Muguna wa Azam, Joash Onyango wa Simba, Farouk Shikhalo wa Mtibwa Sugar, Amos Isense wa Tanzania Prisons, Bolton Omwenga wa Kagera Sugar, Christopher Oruchum wa Namungo na Sosteneth Idah wa Polisi.

ZAMBIA

Taifa hili linashika nafasi ya sita kwa kuwa na wachezaji kwenye Ligi Kuu Bara likiwa nao watano ambao ni Clatous Chama na Moses Phiri wa Simba, Lazarous Kambole wa Yanga, Rodgers Kola wa Azam na Obrey Chirwa anayekipiga Ihefu.

BRAZIL

Msimu huu imerejea kwa kasi baada ya miaka kadhaa kupita, ikeshika nafasi ya saba kwa kuwa na wachezaji wengi kwenye Ligi Kuu Bara - ikiwa nao wanne ambao ni Dario Federico, Peterson Cruz, Bruno Gomes na Rodrygo Olveire wote wa Singida Big Stars.

IVORY COAST

Nchi hii inawakilishwa na wachezaji watatu kwenye Ligi Kuu Bara ambao ni Pascal Wawa wa Singida Big Stars, Tape Edinho na Kipre Junior wa Azam.

ZIMBAMBWE

Prince Dube na Bruce Kangwa wa Azam pamoja na Never Tigere wa Ihefu ndio mastaa watatu wanaoiwakilisha nchi ya Zimbabwe kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

NIGERIA

Nchi hii inawakilishwa na wachezaji watatu kwenye Ligi Kuu Bara ambao ni Victor Akpan na Nelson Okwa wa Simba pamoja na Isah Ndala wa Azam.

BURKINA FASO

Stephano Aziz Ki wa Yanga, Mohamed Ouattara wa Simba na Nurdin Barola wa KMC ni wachezaji watatu wanaoiwakilisha Burkina Faso kwenye Ligi Kuu Bara.

SENEGAL

Nchi hii pia ipo kwenye Ligi Kuu Bara ikiwakilishwa na mastaa wawili ambao ni Pape Sakho wa Simba na Malickou Ndoye wa Azam.

BENIN

Kiungo Olatoundji Djibril wa Coastal Union na beki wa kati Paterne Counou aliyesajiliwa na Namungo ndio mastaa wanaoiwakilisha Benin kwenye Ligi Kuu Bara.

CAMEROON

Nchi hii pia ipo kwenye Ligi Kuu Bara ikiwakilishwa na Moubarack Amza na Betrand Ngafei Konfor wote wa Coastal Union.

MALI

Kipa wa Yanga, Djigui Diarra na Kiungo Sadio Kanoute wa Simba ni miamba wawili wanaoiwakilisha Mali kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

COMORO

Nchi hii nayo inawakilishwa vyema kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu na makipa Ali Ahmada wa Azam pamoja na Mahamoud Mroivil wa Coastal Union.

TOGO

Seidou Blandja wa Namungo ndiye staa pekee nchini anayeiwakilisha Togo kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

RWANDA

Majirani hawa licha ya kuwa karibu, lakini wanawakilishwa na mchezaji mmoja tu msimu huu kwenye Ligi Kuu ambaye ni Meddie Kagere wa Singida Big Stars.

MALAWI

Winga hatari wa Simba, Peter Banda ndiye ‘mwanajeshi’ pekee anayeiwakilisha Malawi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

SERBIA

Dejan Georgijevic ‘Mzungu’ wa Simba ni mchezaji pekee anayeiwakilisha Serbia kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

ARGENTINA

Nchi hii nayo ipo kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwakilishwa na Miguer Escobar anayekipiga Singida Big Stars.

JAPAN

Kiungo wa Geita Gold, Shivo Shinobu ndiye mwamba anayeiwakilisha Japan kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

Ujio huo wa wachezaji wengi Tanzania ni kutoka na sababu mbalimbali ikiwemo mazingira bora ya kufanyia kazi, tamaduni za soka la Bongo, ligi kuonyeshwa kwenye runinga, ubora wa michuano hiyo na kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF kwa timu za Tanzania katika miaka ya hivi karibuni - Simba ikiipeperusha vyema bendera ya nchi.

Hata hivyo ujio wa mastaa hao mbali ya kuwa na faida kadhaa walizozileta katika Ligi Kuu Bara ikiwamo ubora walionao baadhi yao katika kuupiga, pia wanachangia katika pato la nchi kutokana na kodi wanazolipa serikalini pamoja pamoja kuleta utamaduni mpya kutoka katika mataifa yao.

Wakati wakali hao wakitua tayari dirisha la usajili Ligi Kuu Bara na mashindano mengine ya ndani limefungwa mwishoni mwa mwezi uliopita na lilishuhudia klabu nyingi zikivuta silaha mpya na kuacha wachezaji waliokuwa nao kwa nia ya kuimarisha vikosi, jambo lililoibua hisia kuwa msimu huu huenda ukawa na msisimko wa aina yake ukichagizwa pia udhamini mkubwa uliowekezwa katika Ligi Kuu.

Columnist: Mwanaspoti