Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mason Greenwood namna ya utundu unavyoua ndoto

Skysports Mason Greenwood Man Utd 5659289 Mason Greenwood

Sun, 27 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Haikushangaza Sir Alex Ferguson alipowapiga marufuku wachezaji wake vijana wasinunue magari ya kifahari wakati huo akiwa kocha wa Manchester United. Magari ya kifahari yalikuwa kwa ajili ya kina Paul Ince, Ryan Giggs, Eric Cantona, Roy Keane, Peter Schmeichel na wengineo.

Watoto licha ya kuwa na noti zao ilikuwa ni marufuku kuendesha Lamborghini, Ferrari, Aston Martin Languish, Bentley na mengineyo. Sir Alex anawajua watoto wa Kiingereza na hasa wanaposhika noti. Wakorofi balaa. Walevi, wanapenda matanuzi.

Sir Alex alikuwa anayajua haya ya kina Mason Greenwood. Ni utoto na pesa tu. Majuzi Manchester United wamelazimika kuachana na Greenwood. Moja kati ya vipaji vizuri vya Kiingereza viliwavyowahi kuibuka katika miaka ya hivi karibuni.

Kisa? Alimpiga rafiki yake wa kike na kisha akamlazimisha kufanya naye ngono. Sauti zao zilisikika na hata polisi walisikia. Baadaye Manchester United ikamsimamisha kazi. Kesi ilipoendelea upande wa mwanamke uliamua kutoendelea tena na kesi.

Ilikuwa ni rahisi tu kutoendelea na kesi tena kwa sababu Greenwood aliendelea na mapenzi na dada huyo. Inawezekana kuna mlungula alipeleka upande wa mwanamke na wakafikia uamuzi huo. Baadaye alizaa na binti huyo.

Mahakama haikuwahi kumtia hatiani kwa sababu kesi ilifutwa, lakini wanawake wengi waliishupalia kesi hiyo. Majuzi United walikuwa wamedhamiria kumrudisha Greenwood kikosini, lakini habari zikavuja. Wachezaji wa timu ya wanawake wakatishia kuja juu.

Mashabiki wa kike wa Manchester United wakaja juu. Manchester United haikuwa na jinsi zaidi ya kuchana mkataba wake. Wametangaza tu kwamba Greenwood hatavaaa tena jezi ya timu hiyo. Wanachoweza kufanya kwa sasa ni kumtoa kwa mkopo mpaka mkataba wake umalizike au wamuuze kwa dau la chini.

Tatizo kwa Greenwood ni kwamba hawezi kuhamia katika timu nyingine yoyote ya Kiingereza. Timu yoyote ambayo itathubutu kumchukua Greenwood itashambuliwa vilivyo na mashabiki wa pande zote za England. Ndivyo wazungu walivyo. Kwanini unampokea mhalifu?

Nafahamu kwamba Arsenal wanamtamani, Chelsea wanamtamani, Manchester City wanamtamani. Hata Liverpool wanamtamani. Tatizo hakuna anayeweza kuthubutu kupeleka pua yake kwenda kumchukua. Ambacho United wanahofia ndicho ambacho wengine wanahofia.

Na sasa Greenwood analazimika kwenda kutafuta timu Italia au Uturuki au kwingineko. Ana miaka 21 na tayari kila kitu kwake kimekwenda kombo. Ndivyo watoto wa Kiingereza walivyo. Wachache sana ni wapole. Inatokea nadra kuwa mpole kama Bukayo Saka au Harry Kane.

Wengi wao wana mikasa. Wayne Rooney tunamjua kwa ulevi wake. Steven Gerrard ilikuwa kawaida kulewa na kupigana disko. Jack Wilshere naye alikuwa hivi hivi. Vurugu tu. Vipi kuhusu Jack Grealish? Umesikia mara ngapi mikasa yake ya ulevi. Vipi kuhusu Dele Alli ambaye mpira umemshinda akiwa na miaka 24?

Rafiki yangu John Terry naye alikuwa msela hivi hivi. Akaenda kutembea na mpenzi wa rafiki yake, Wayne Bridge. Ni sehemu ya maisha yao ya usiku. Usipokuwa makini unapotea kama Greenwood. Ukiongeza umakini kidogo unaweza kujikuta unatoboa.

Rafiki yangu Harry Maguire naye alipigana akiwa amelewa pale Ugiriki akiwa likizo. Haya ndio maisha ya kawaida ya vijana wa Kiingereza. Bahati nzuri wengi wao waliweza kunusurika na kufikia matarajio ya vipaji vyao.

Huzuni inakuja kwa Greenwood ambaye mtego wa panya umemnasa akiwa kinda wa miaka 21. Amelewa amekwenda kuanzisha vurugu kwa mpenzi wake na yote aliyofanya yamemtokea puani. Alikuwa anakuja vizuri na lazima mashabiki wa United wamebana meno kwa hasira kutokana na kile ambacho kimemtokea.

United imepata hasara kubwa kwa Greenwood. Kwanza ilikwenda kumchukua Mbrazili Antony ambaye kiukweli hafikii walau nusu ya ubora wake. Greenwood anacheza kwa malengo na analijua lango vilivyo. Antony huwa anarukaruka tu uwanjani bila malengo.

Lakini ni wazi kwamba baada ya kila kitu ambacho kimetokea thamani ya Greenwood imeshuka. Angeweza kuwa mchezaji mkubwa zaidi na angekaa klabuni kwa muda mrefu huku akiifanyia United kile ambacho mchezaji kama Saka anaifanyia Arsenal.

Lakini hapohapo ni wazi kwamba katika soko la sasa hata kama United ingeamua kumuuza Greenwood isingekosa kiasi cha Pauni 70 milioni na zaidi. Kwa sasa hakuna wanachoweza kufanya zaidi ya kukubali kwamba wamepata hasara.

Katika timu ya taifa ya England, Greenwood hawezi kucheza. Nasikia Wajamaica wanataka aichezee timu yao ya taifa. Inawezekana kwa sababu ana asili ya huko. Waingereza wamepoteza kipaji kikubwa, lakini hawana jinsi.

Ni tabia za watoto wao. Wana vurugu wakipata pesa mapema. Haishangazi kuona ndio maana Sir Alex alikuwa anajua namna ya kuwalea. Alikuwa anakwenda kuwachapa hata kwa mama zao. Alikuwa ana wapelelezi wake katika maeneo yote ya starehe ambayo vijana wake walikuwa wanakwenda.

Tatizo la kuwa na pesa nyingi katika umri mdogo linawaathiri zaidi vijana wa Kiingereza pengine kuliko vijana wa mataifa mengine. Mfano halisi ni huu hapa wa Greenwood. Hapa inaweza kuwa mwisho wa safari yake kisoka. Wakitulia huwa wanakwenda mbali zaidi, lakini wasipotulia haya ndio huwa yanakuwa matokeo yake.

Kila la heri kwake. Kuna wachezaji waliowahi kupata matatizo kama yake, lakini hawakuwahi kurudi tena katika viwango vya juu. Hawa ndio kina Adam Johnson, Ched Evans na wengineo. Hawakuwahi kurudi tena kucheza soka katika kiwango cha juu.

Labda yeye anaweza kwenda zake Italia akacheza kwa kiwango cha juu akajikuta anaishia katika timu kubwa za Italia au Hispania kama zitamtaka bila ya kukosolewa kama Waingereza wanavyoogopa. Nasikia Jose Mourinho pia ambaye ni kocha wake wa zamani United naye anamtaka.

Columnist: Mwanaspoti