Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mashabiki mjifunze kuwatia moyo wachezaji

8fe749d6eccd0890cfbc28e55db71691.png Mashabiki mjifunze kuwatia moyo wachezaji

Sat, 20 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MASHABIKI wa soka Tanzania wanapenda mpira na daima wanapenda kuona timu zao zikifanya vizuri. Hilo ni jambo la kawaida kwa kila aliye shabiki wa mpira duniani kote lakini ushabiki kwa mashabiki wa hapa nchini umepitiliza kiwango.

Mashabiki wanapenda kukosoa, kulaumu na siku zote wao wanajua mpira kuliko hata wachezaji na makocha. Kingine walichoumbwa nacho hasa hapa nchini mashabiki wa soka wanajua kukatisha tamaa hasa pale wanapoona timu pengine imefanya vibaya mchezo mmoja au miwili.

Ni wepesi kuhukumu kwa mchezo mmoja na kukata tamaa haraka bila kujali timu yake imekutana na mpinzani wa aina gani. Hawataki kwenda na matokeo ya kushindwa au kupata sare bali kushinda tu jambo ambalo haliwezekani.

Kingine ni kwamba kuna utamaduni umejengeka kwa baadhi ya mashabiki pengine ni kutokuwa na imani kwa kutizama matukio yaliyopita ya kihistoria au labda ni watu wenye tabia ya kuzoea kushindwa siku zote.

Unaweza kusema mchawi wa timu yako ni wewe mwenyewe shabiki kwasababu utashangaa baadhi yao kabla hata timu haijaenda kwenye mashindano baadhi wanaanza kusema hao wanakwenda tu kusindikiza, hao hawafiki mbali wanakwenda kutolewa.

Sasa inapofanya vibaya unawezaje kulaumu wakati tayari ulizungumza maneno machafu yenye laana na uchawi ndani yake? Kabla ya kusema wale wanaenda kutolewa hebu tujifunze kutoa ushauri nini kifanyike? Kuboresha ili kama ni wachezaji wajue cha kufanya.

Unaweza kusema ni haki ya shabiki kukosoa au kulaumu kwa ajili ya kuleta changamoto kwa wahusika wafanye vizuri zaidi lakini sio kila kitu kinapaswa kulaumiwa bila kutizama mazingira, uwezo wa timu yao na mpinzani wao pamoja na mambo mengine.

Kuna jambo la kujifunza katika soka au michezo yoyote ya kiushindani kwa mashabiki kuwa wavumilivu sio kila jambo linastahili kutolewa hukumu mapema. Kujifunza kuwatia moyo wachezaji na makocha wao kisha kulaumu kidogo ili wajione kuwa wamebeba jukumu la taifa.

Kingine, mashabiki wanapolaumu au kunyoosha vidole waangalie ni akina nani kwasababu kuna timu za vijana ambazo wana ndoto na ndio kwanza wanataka kufanya kitu kizuri kutimiza ndoto zao.

Wanapokosea wanahitaji kukosolewa kidogo kisha watiwe moyo kuongeza bidii zaidi na hakika wanaweza kufanya jambo kubwa. Ikiwa wanalaumiwa kila mara vipaji vyao vinaweza kufa kwasababu watapoteza kujiamini, mwelekeo na hatma ya ndoto zao inaweza kuishia njiani.

Vijana wakitiwa moyo kuwa wanaweza watacheza vizuri kwa kujiamini ndio maana hata makocha baadhi huwafariji wachezaji wao na kusema kuna mapungufu tumeyaona tunakwenda kuyarekebisha kwenye mazoezi na hata kama amemuona mchezaji fulani kakosea.

Anajua madhara yake baadaye ni yapi, maneno makali yanaharibu mtu kisaikolojia hasa kama huyu anasema hivi vipi wengine? Utaona baadhi viwango vimeshuka au wanacheza chini ya kiwango chake kwasababu tayari anakuwa amekatishwa tamaa. Inawezekana kabisa kubadilika kuanzia sasa hasa kwa timu zinazowakilisha nchi kwenye mashindano makubwa.

Kuna timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 Ngorongoro heroes ipo kwenye michuano ya Afrika Mauritania. Ianze kutiwa moyo kuanzia sasa haijalishi itasonga mbele au kutolewa mapema kwasababu ndio kwanza imeshiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo.

Wachezaji wamejifunza na kupata uzoefu na wengine wameonesha uwezo wao hata wakirudi itawapa nafasi zaidi kule wanakokwenda kwenye vituo vya soka au klabu wanazotumikia watafanya vizuri zaidi. Tunapojifunza kukosoa na kulaumu, tujifunza pia kutia moyo na kukubali kwa manufaa ya maendeleo ya soka. Lakini pia, kuwa watulivu.

Columnist: habarileo.co.tz