Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Marefa wetu waandaliwe kutumia VAR, teknolojia ya goli

Eeyjkkj Marefa wetu waandaliwe kutumia VAR, teknolojia ya goli

Sat, 4 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

WAKATI hoja ya matumizi ya teknolojia maalum ya kusaidia waamuzi wa soka (VAR) ilipoibuliwa na Waingereza baada ya timu ya taifa ya England kukataliwa bao katika mchezo wa Kombe la Dunia 2010 dhidi ya Ujerumani, ilionekana kama ni jambo ambalo haliwezi kufanikiwa.

Kundi kubwa la wadau na mashabiki wa soka walionekana kupinga hoja ya matumizi ya VAR ama ile ya mstari wa goli ya kumjulisha mwamuzi kama mpira umevuka mstari wa goli au la wakiamini ingepoteza ladha na msisimko wa mchezo wa soka.

Hata hivyo, miaka 11 baadaye, teknolojia ya VAR na ile ya mstari wa goli zimeonekana kuwa jambo la kawaida katika soka na ni ndoto ya kila nchi kuzitumia kwa lengo la kuhakikisha waamuzi wanatoa uamuzi wa haki zaidi na kupunguza matukio yanayozinufaisha timu zisizostahili.

Tanzania ni kati ya nchi ambazo mashabiki na wadau wa soka wanatamani kuwepo kwa teknolojia hizo katika ligi yetu ingawa kiuhalisia sio jambo rahisi kutokana na gharama kubwa ya ununuzi na utunzaji wa vifaa vya teknolojia hizo.

Dunia ni kama kijiji na Tanzania sio kisiwa hivyo wakati wenzetu wanatembea, sisi angalau tunapaswa kujitahidi kutambaa badala ya kutojaribu kupiga hatua yoyote.

Ni kweli teknolojia ya VAR ni ya gharama kubwa na ni vigumu kutumika nchini kwa msimu huu, ujao au hata ule wa 2023/2024 lakini hilo halipaswi kuwa sababu ya kuzuia waamuzi na maofisa wa soka nchini kupata maarifa kuhusu matumizi ya vifaa na teknolojia hiyo.

Zipo nchi, vyama na mashirikisho rafiki ya soka ambayo tunaweza kuomba yatusaidie kuwapiga msasa maofisa wa mechi juu ya matumizi, utunzaji na usimamiaji wa teknolojia hiyo na likawa jambo lenye tija kwetu.

Kuna faida kubwa kwao kupata maarifa na ufahamu juu ya masuala ya VAR hata kama bado teknolojia hiyo haijafika ama kuanza kutumika nchini tofauti na sasa ambapo wengi wao wanaishia kuiona ikitumika katika ligi na mashindano mbalimbali kupitia luninga au kusoma na kusikia katika vyombo vya habari na mitandao mbalimbali.

Kwanza ni kuwaweka tayari maofisa na waamuzi wetu wa kutumia teknolojia hiyo pindi itakapokuja kutumika hapa nchini badala ya kuiona ngeni na mamlaka za soka kuja kutumia nguvu na gharama kubwa kuwajengea uwezo wa kuitumia siku za usoni.

Lakini pia hiyo itasaidia kuwafungulia milango ya fursa ya kupata nafasi ya kuchezesha ama kusimamia mara kwa mara mechi za mashindano ya kimataifa kama vile Kombe la Dunia, Kombe la Mataifa ya Afrika, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika na mengineyo yanayosimamiwa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Kwa sasa waamuzi wa Tanzania ambao wamekuwa wakipata fursa za mara kwa mara kuchezesha mashindano mbalimbali makubwa ya soka barani Afrika ni refa msaidizi, Frank Komba pamoja na mwanamama, Jonesia Rukyaa.

Kumbukumbu zinaonyesha waamuzi hawa kwa nyakati tofauti walishiriki program za mafunzo ya matumizi na usimamizi wa teknolojia ya VAR pindi walipoteuliwa katika orodha ya kuchezesha mashindano ya timu za taifa za vijana na zile za wanawake hivyo pengine hiyo imekuwa kati ya sababu zinazofanya wapewe kipaumbele pindi kunapofanyika uteuzi wa waamuzi wa kuchezesha mashindano tofauti tofauti kulinganisha na wenzao.

Na ni vyema kutoa wito pia kwa waamuzi wetu wajitahidi kujiendeleza katika elimu ya kawaida hasa ya lugha ili iwe rahisi kwao kumudu mafunzo ya namna hiyo iwapo mamlaka za soka zitaona haja ya kuwajengea uwezo wa matumizi ya teknolojia ambazo zinatumika kuwasaidia kama ilivyo kwa VAR au ile ya mstari wa goli.

Lazima tuwe wakweli kwamba tuna kundi kubwa la waamuzi wa soka hapa nchini ambao changamoto ya kielimu imekuwa ikiwakwamisha kupiga hatua ndani na kimataifa kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya nadharia tofauti na nchi nyingine ambapo tumeshuhudia zikiwa na kundi kubwa la waamuzi ambao wana msingi mzuri wa kielimu.

Haitokei kwa bahati mbaya wala uonevu kwa waamuzi wengi wa Tanzania kutopata fursa ya kuchezesha mechi kubwa za mashindano mbalimbali bali kuna maeneo ambayo wana udhaifu kama hayo ya matumizi ya teknolojia hivyo ili kuwasaidia ni lazima tuwatengenezee mazingira bora ya kuwapatia maarifa ambayo yanachangia kuwaangusha.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz