Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Marais wa Tanzania na michezo

IMG 4297 Wanamichezo Ikulu.jpeg Marais wa Tanzania na michezo

Tue, 13 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hivi karibuni Klabu ya Yanga ilialikwa Ikulu ya Rais Samia Hassan Suluhu kwa ajili ya kupongezwa baada ya kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ilicheza fainali hiyo dhidi ya USM Alger ya Algeria na katika mchezo wa kwanza ilipoteza nyumbani kwa mabao 2-1 na kwenda kushinda ugenini kwa bao 1-0. Bao la ugenini liliitoa Yanga.

Mbali na Rais Samia, kuipongeza Yanga, pia alifanikiwa kutatua mgogoro wa usajili ulioibuka kati ya Yanga na kiungo wa timu hiyo, Feisal Salumu ‘Fei Toto’

Yanga sio timu ya kwanza kualikwa Ikulu kwani karibu awamu zote zilizoongoza Tanzania zilikuwa zikialika timu mbalimbali Ikulu, nyayo zilizofuatwa na Rais Samia safari hii ni kutatua migogoro ya kimichezo. Mwaka 1964, mashindano ya Gossage Cup (baadaye yaliitwa Kombe la Challenge) yalifanyika jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yaliyoshirikisha timu za Kenya, Uganda, Zanzibar na Tanzania Bara. Septemba 26, Tanzania Bara ilifungua mchezo wa kwanza dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’, katika mchezo huo ambapo ilishinda bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti Mbwana Abushiri.

Septemba 29, Tanzania Bara ilirudi tena uwanjani dhidi ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’na kuifunga mabao 3-1.

Mabao ya Abdulrahaman Lukongo (mawili) na Abdullah Aziz. Mchezo wa mwisho Tanzania Bara (baadaye iliitwa Kilimanjaro Stars) ilicheza dhidi ya Uganda na kushinda mabao 3-0.

TIMU YAITWA IKULU

Baada ya ushindi huo, Rais wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere aliita Timu ya Taifa ya Tanzania Bara Ikulu na kushereheka nao pamoja.

Hii inaweza kuwa ndio timu ya kwanza kwenda Ikulu kama ile ya mwaka 1944 ya Tanganyika iliyotwaa Gossage Cup haikuitwa Ikulu.

Bado Tanzania ikiwa kwenye makali yake iliendelea kutesa kwenye mashindano hayo baada ya kwenda kutetea taji lake mwaka unafuata wa 1965 ambalo fainali zake zilifanyika Uganda.

RAIS NYERERE AGOMA KUKAGUA TIMU

Mwaka 1972, katika sherehe za miaka 10 ya Tanganyika, Rais Julius Nyerere hakushuka chini kuzikagua Timu za Taifa za Tanzania na Sudan na kumwachia jukumu hilo Rais wa Sudan, Jaafar Nimeiry.

Kitendo hicho kilitokea Desemba 9, mwaka huo baada ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania kuingia uwanjani wakiwa vifua wazi. Ni kipa tu Omary Mahadhi ndiye aliyevaa jezi ya juu, lakini wachezaji wote walivaa bukta tu. Jezi za Timu ya Taifa zilisahaulika, hadi wakati wa mapumziko ndipo wachezaji hao walivaa jezi zao.

ILIBEBA TENA MWAKA 1974

Baada ya hapo Tanzania ilikaa hadi mwaka 1974 ikabeba tena taji la Challenge kwa kuifunga Uganda kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya sare ya bao 1-1. Stars ilikuwa chini ya kocha mzawa, Shaban Marijani ‘Maji Mengi’ au Maji Moto.Mashindano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam timu zilikuwa katika makundi mawili. Hapa hakuna kumbukumbu kama kombe hili lilienda ikulu.

MIAKA 20 BAADAYE

Baada ya kuchukua taji hilo mwaka 1974, Timu ya Taifa ya Tanzania Bara ilikaa miaka 20 ndipo ilipoibuka na kucheza fainali dhidi ya Uganda tena. Katika Kundi A ambazo mechi zake zilichezwa Nairobi kulikuwa na timu za Tanzania, Kenya A, Somalia na Djibout.

Novemba 26, Kenya A iliifunga Somalia mabao 3-1 na Novemba 28, ikaifunga Djibout 4-1. Novemba 29, Tanzania ikaifunga Somalia 4-0. Desemba Mosi Somalia ikaifunga Djibout 1-0. Siku hiyo hiyo Kenya A ikakubali kuchapwa bao 1-0 na Tanzania. Desemba 3 Tanzania ikaikandamiza Djibout 3-0 na kufanikiwa kutinga fainali. Katika fainali ikacheza dhidi ya Uganda iliyokuwa Kundi B sambamba na Eritrea, Seychelles na Kenya B.

Katika fainali Uganda na Tanzania zilishindwa kupata mbabe baada ya sare 2-2 na mchezo kuariwa kwa penalti ambapo Tanzania ilishinda kwa mabao 4-3. Taji hili moja kwa moja lilienda Ikulu ya Tanzania na kupokewa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassani Mwinyi.

SIMBA NA MWINYI TAIFA

Mwaka 1993, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alienda Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) kushuhudia Simba ikicheza fainali ya Kombe la CAF lakini bahati mbaya kwa upande wake na Watanzania kwa ujumla taji hilo lilibebwa na Stellah Adjamen ya Ivory Coast.

Lakini pia Rais Mwinyi akiwa ameshastaafu mwaka 2002 alienda Uwanja wa Taifa kushuhudia mechi ya Simba na Yanga iliyoisha kwa Simba kushinda mabao 4-1.

Katika utawala wa Rais Mwinyi mara kadhaa matatizo ya wachezaji kuhusu usajili kama ilivyotokea kwa Fei Toto yalitatuliwa. (Tutakuja kuona siku za usoni).

RAIS MKAPA AJENGA UWANJA

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alionekana mara chache sana viwanjani kushuhudia mchezo wa soka lakini alifanikiwa kujenga Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo jijini Dar es salaam. Mwaka 2000, Rais Mkapa aliahidi kujenga uwanja kabla ya kumaliza awamu yake.

KIKWETE ALIPA MAKOCHA

Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete huyo alifanya mambo mengi kwenye michezo. Karibu michezo yote ilipata kitu kutoka kwake, serikali yake ililipa makocha wa ngumi, riadha, netball na hata riadha. Lakini kwenye soka kulikuwa na makubwa zaidi mara kadhaa alihudhuria mechi za timu ya taifa na pia alivipa nguvu vyama vya michezo kwa ujumla. Mwaka 2009, Rais Kikwete alikabidhiwa kombe la Challenge na Timu ya Taifa pale Ikulu.

RAIS MAGUFULI NA UWANJA WA DODOMA

Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli katika utawala wale aliahidi kujenga uwanja wa kisasa jijini Dodoma.

Hata hivyo hakuweza kufanikisha jambo hilo baada ya kufariki dunia akiwa mwanzoni kabisa mwa awamu yake ya pili. Hata hivyo, mrithi wake, Rais Samia ameahidi kuendeleza pale alipoishia mtangulizi wake.

Mbali na hicho, Rais Magufuli Machi 25 aliita timu ya taifa ikulu baada ya kufuzu fainali za Kombe la Afcon kule Misri ikiwa ni mara ya pili tangu mwaka 1980. Mbali na kuwaalika pia aliahidi kuwapa viwanja.

RAIS SAMIA BADO TUNAYE

Mbali na yote aliyoyafanya, Rais Samia pia ni mfadhili wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati la Wanawake (Samia Cup) na ameahidi kujenga viwanja vilivyo chini ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuviwekea nyasi bandia. Pia, Rais Samia alizipokea timu za wanawake za U-20 na U-18 Ikulu baada ya kutwaa mataji ya kimataifa. Bado serikali yake imepunguza gharama za nyasi bandia.

Columnist: Mwanaspoti