Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mapinduzi elimu yanautegemea mkopo huu wa Benki ya Dunia

WBTZ Mapinduzi elimu yanautegemea mkopo huu wa Benki ya Dunia

Tue, 12 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SEKTA ya elimu ni muhimu katika maendeleo ya nchi ili kuiendeleza na kuikuza. Upatikanaji wa fedha ni nyenzo muhimu inayowezesha kupanga mipango na mikakati ambayo itaboresha sekta hiyo kikamilifu.

Serikali ndiyo yenye dhamana ya kukuza sekta zote na kuleta maendeleo huku elimu ikipewa kipaumbele.

Ndiyo maana serikali inafanya juhudi ili kufanikiwa katika mipango na mikakati ya kuleta maendeleo yanayogusa na kuboresha maisha ya watu kupitia elimu.

Hata hivyo, ni vigumu kwa serikali kufanikisha mipango yake bila fedha au misaada kutoka sekta binafsi.

Ndiyo maana serikali inasisitiza ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (Public and Private Partnership) katika shughuli za kimaendeleo.

Taasisi za fedha mathalani benki za ndani na nje ni wadau muhimu katika maendeleo ya elimu nchini kupitia misaada na mikopo wanayoitoa ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa sekta ya elimu. Taasisi za fedha zinatoa misaada ya rasilimali fedha na vitu kama viti, meza, madawati, vitabu, kompyuta, madaftari ili kusaidia juhudi za kuinua sekta ya elimu.

Benki ya Dunia (WB) imekua ikitoa mikopo kwa nchi mbalimbali duniani katika kuchagiza maendeleo ya elimu. Tanzania kama yalivyo mataifa mengine iliamua kukopa mkopo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP) ili kuweka mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia katika shule za sekondari nchini. Mradi huu unategemewa kunufaisha wanafunzi 6,000,000, hivyo ni vyema kuangalia namna ambavyo taifa litafaidika.

TIJA YA MKOPO

Namba moja itakuwa kujenga miundombinu ya shule, lengo likiwa ni utekelezaji wa sera ya elimumsingi bila ada ambao umezalisha changamoto ya mahitaji ya miundombinu kama vile madarasa, ofisi za elimu, vyoo na nyumba za walimu.

Hii ni kutokana na ongezeko la wanafunzi katika shule za sekondari. Hivyo, kupitia mkopo huu, serikali inakusudia kujenga shule nyingi ili kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri kwa kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.

“Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuongeza miundombinu katika maeneo mbalimbali ya elimu baada ya mwitikio mzuri wa elimu bila ada, ambao utaongeza idadi kubwa ya wanafunzi wanaokwenda kujiunga na elimu ya sekondari. Mradi huu utasaidia katika kuboresha na kuongeza miundombinu katika shule za sekondari nchini ambazo zitapokea wanafunzi hao waliotokana na mwitikio wa elimu bila malipo,” anasema Profesa Ndalichako.

Pili ni kuimarisha utoaji wa ushauri nasaha ili wanafunzi wanaotoka familia zenye changamoto mbalimbali za kijamii ama mazingira duni wawe na mahali pa kusemea ili serikali ichukue hatua stahili kwa ustawi bora wa wanafunzi hao. Pasipo kuwatambua wanafunzi wanaotoka mazingira magumu na utoaji wa ushauri nasaha, baadhi yao watashindwa kuendelea na masomo na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao wanazotaka kuzifikia katika maisha yao ya baadaye.

Tatu, kutoa mafunzo kazini kwa walimu yakiwamo ya kidijitali kwa wanafunzi. Mafunzo kazini pia ni muhimu katika kuhakikisha walimu wanaendana na kasi ya maendeleo iliyopo.

Miongoni mwa mipango ya Wizara ya Elimu ni kuwapatia walimu mafunzo ili kuongeza ujuzi na stadi ili kufundisha wanafunzi kisasa zaidi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Aidha, wanafunzi wanapata mafunzo ya digitali katika ujifunzaji. Hii ni kutokana na umuhimu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika kufundisha na kujifunza.

Kupitia Tehama, walimu na wanafunzi watapata maarifa na stadi mbalimbali kupitia elimu ya mtandaoni.

Aidha, suala jinginge muhimu la nne ni kuwaboreshea wanafunzi wa kike mazingira ya kujifunza. Mradi huu umekusudia kuwapunguzia changamoto wanawake wanaokabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda shule, hali inayohatarisha usalama wao. Miongoni mwa maeneo ambayo fedha za mkopo huu zitaelekezwa ni katika ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wasichana.

“Watoto wa kike wamekuwa wakipata vikwazo kutokana na umbali wa shule na kusababisha kupata changamoto wanapokwenda ama kurudi shuleni kwa hiyo kupitia mradi huu, tunakwenda kujenga shule za bweni kwa ajili ya watoto wa kike,” anasisitiza Waziri wa Elimu Ndalichako.

Pia mradi utajenga shule mpya maalum za wasichana zenye mabweni.

Pia mradi utajenga shule mpya maalum za wasichana zenye mabweni.

Kwa hakika, mkopo huu una tija kubwa kwa taifa hili kwani unakwenda kuwanufaisha watoto ambao baadhi yao wanatoka kwenye kaya maskini.

Kutokana na uboreshwaji wa sekta ya elimu kupitia mkopo huu, watoto kutoka kaya maskini wanatarajiwa kupata elimu bora kutokana na fedha kuelekezwa kwenye uboreshaji wa mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji.

Kwa hiyo ni vyema wazazi na walezi waendelee kuwalinda na kuwakinga watoto wao wakati huu wa likizo ya corona ili wawe na afya njema na kunufaika na mkopo huu wa elimu kutoka Benki ya Dunia.

Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0764-666349.

Columnist: www.tanzaniaweb.live