Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maoni: Simba chagueni viongozi bora

DBBBA2A9 77F6 41ED 8634 BB3A9FC10D1D.jpeg Uchaguzi Mkuu wa Simba unafanyika leo Januari 29

Sun, 29 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Zaidi ya wanachama 1,000 wa klabu ya Simba leo wanafanya Uchaguzi Mkuu kupata viongozi wapya watakaoiongoza kwa miaka mingine minne ijayo, baada ya uongozi uliopo kumaliza muda wake madarakani.

Kuna wagombea 14 wanachuana kwenye uchaguzi huo utakaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo Dar es Salaam ambapo wanachama hao watakuwa na jukumu la kuchagua mwenyekiti mpya na wajumbe watano kuingia kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo.

Upigaji kura unakuja ikiwa ni baada ya takriban wiki mbili za kampeni za usiku na mchana walizofanya wagombea katika matawi mbalimbali ya klabu hiyo ndani na nje ya Dar es Salaam, na leo ndiyo siku ya hukumu kwa wagombea.

Kwanza tunapenda kuwapongeza wote waliojitokeza kugombea nafasi hizo kwa ajili ya kutekeleza takwa muhimu la katiba yao, ukiwa ni uchaguzi mkuu wa pili kwa klabu hiyo kuufanya katika mfumo mpya wa uendeshaji wa umiliki wa hisa - kukiwa na pande mbili - ule wa mwekezaji na wanachama upande mwingine.

Katika kipindi chote tumeshuhudia kampeni za kusisimua ambapo wanachama waliwauliza maswali wagombea na wao kuyajibu, ikiwa sio tu kuwaridhisha waliouliza bali majibu hayo ndiyo wanayoenda kuyafanyia kazi watakapochaguliwa.

Pamoja na hayo, tunajua kwamba Simba inakabiliwa na changamoto kibao za kiuendeshaji na kimfumo ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi ili irejee katika makali iliyoanza nayo miaka mitano iliyopita ambapo ilianza kujiimarisha kimataifa na hivyo kuanza kupigiwa mfano wa kuja kuwa moja ya timu kubwa barani Afrika.

Tunajua juhudi zilizoifikisha Simba mahali hapo hazikuibuka tu, bali kuna watu walikaa na kupanga mipango mathubuti ambayo ilikuwa na majibu hayo. Hivyo, kwa wanachama wanapoingia katika uchaguzi huu wajue kwamba klabu yao ni kubwa na inahitaji watu watakaoifanya iendelee kutamba ndani na nje ya nchi na hivyo kuliletea heshima taifa letu.

Kwa upande wao, wale watakaoshindwa, tunawasihi wakubali matokeo na kujikita kushirikiana na washindi ili kwa pamoja waweze kuijenga klabu yao. Ni vyema wakajua kwamba hakuna mafanikio ambayo wanaweza kuyapata wakiwa katika hali ya kutoelewana, majungu, kufitiniana na kuhasimiana.

Kwa pande zote - ule wa mwekezaji na klabu tunawashauri washirikiane na wawe kitu kimoja. Hatutarajii kusikia minon,g'ono ya kuikwamisha klabu katika mipango iliyonayo ya kufika mbali kimataifa. Kama ni mwekezaji ajitoe kwa moyo mmoja afanye mambo na pia wawakilishi wa wanachama ndani ya bodi ya wakurugenzi wakapige kazi wasiwe "ndiyo mzee" kwa kila jambo. Tunawatakia uchaguzi mwema.

Columnist: Mwanaspoti