Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Manula kashindikana, hana mpinzani

Aishi Manula 33 Aishi Salum Manula

Tue, 26 Jul 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Uongozi wa Simba umefikia makubaliano ya kumsainisha mkataba mpya wa miaka mitatu kipa namba moja, Aishi Manula utakaomweka Msimbazi hadi 2025.

Manula alikuwa akihusishwa kuondoka baada ya awali dili lake kuonekana kusuasua, huku klabu mbalimbali za ndani na nje ya nchi zikionekana kuhitaji saini yake, ikiwemo Azam FC.

Fuatilia uchambuzi wa kipa huyo tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Msimbazi Agosti 2017 akitokea kwa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC.

MATAJI (11)

Katika kipindi cha miaka mitano Manula ameiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara nne mfululizo (2017/18), (2018/19), (2019/20) na 2020/21.

Mbali na ligi ila amechukua pia mataji mawili mfululizo ya Kombe la Shirikisho la Azam maarufu (ASFC) msimu wa 2019/2020 na 2020/2021.

Kwenye Ngao ya Jamii amechukua mara nne mfululizo tangu 2017-2020 akiwa na kikosi hicho ambacho ndicho kinaongoza kutwaa taji hilo mara tisa (9) tangu lilipoanzishwa rasmi 2001, lingine likiwa ni la Mapinduzi alilotwaa mwaka huu (2022).

TUZO BINAFSI

Manula (26) ndiye anayeongoza kwa kuweka rekodi ya kuchukua tuzo nyingi (5) za Ligi Kuu Bara kwenye nafasi anayocheza kwa kizazi cha sasa.

Manula alitwaa tuzo hizo misimu ya 2015/2016, 2016/2017 akiwa na Azam FC, huku akiwa na Simba ni 2017/2018, 2019/2020, 2020/21 kisha msimu ulioisha wa 2021/22 alipinduliwa na Djigui Diarra wa Yanga ambaye nyavu zake hazikuguswa mara 15.

Endapo msimu wa 2018/19 ungekuwa na tuzo basi Manula angekuwa anamiliki sita, kwani aliiwezesha timu yake kunyakua ubingwa kwa kufikisha pointi 93 huku akifungwa mara 15.

HANA MPINZANI

Tangu kuwasili kwenye kikosi hicho, Manula amekutana na makipa wengi ila hadi sasa hakuna aliyeleta ushindani kwake wa kutishia nafasi yake hali inayomfanya kuendelea kutamba kila uchao.

Miongoni mwa makipa hao ni Emmanuel Mseja, Said Mohamed ‘Nduda’, Deogratius Munish ‘Dida’, Jeremiah Kisubi, Ally Salim na Beno Kakolanya.

MSIKIE MWENYEWE

Akitaja siri ya kiwango chake hadi sasa Manula anasema ni kutokana na kutoleta mazoea kwenye kazi, awapo uwanjani mabeki wakikosea anawaambia ukweli na kuwakemea (kuwafokea) ili kutimiza malengo ya kuhakikisha timu inafanya vizuri.

“Kiwango changu kinatokana na ushirikiano uliopo baina yangu na mabeki, kwani wanahakikisha sifikiwi langoni mwangu kirahisi na ikitokea wamepitwa nasahihisha makosa yao,” amesema Manula.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz