Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mambo yalivyokuwa kwa ATCL wakati wa covid-19

2c1535d63dde83ff75805bd69cf21aed Mambo yalivyokuwa kwa ATCL wakati wa covid-19

Tue, 22 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KUZUKA kwa maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (covid-19), kuliathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya usafiri wa anga hapa nchini na nje ya nchi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuzuka kwa maambukizi hayo katika mji wa Wuhan uliopo Jimbo la Hubei nchini China mwezi Desemba mwaka jana na kisha kusambaa dunia nzima.

Kwa hapa Tanzania ugonjwa huo uliripotiwa kwa mara ya kwanza mwezi Machi mwaka huu jijini Arusha baada ya mwanamke mmoja raia wa Tanzania aliyetokea nchini Ubelgiji kukutwa na virusi hivyo baada ya kupimwa.

Kadhia hii ya covid-19 iliathiri sekta zote na maisha kwa ujumla ikizingatiwa kuwa baadhi ya wafanyakazi, hususani kwenye sekta binafsi walipunguzwa kazi lakini pia kuathiri baadhi ya huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi kwa ujumla wake.

Sekta ya anga ni miongoni mwa sekta zilizoathirika kutokana na ugonjwa wa covid-19 katika kipindi chote cha mwaka huu wa 2020 kutokana na mashirika mengi ya ndege kusitisha safari zake, yakiwemo yale yaliyokuwa yakileta ndege zake Tanzania.

Lakini pia hata ndege za ATCL nazo zililazimika kusitisha safari zake nje ya nchi kutokana na nchi mbalimbali kufunga anga na mipaka yake kama sehemu ya kupambana na virusi hivi.

Mwezi Julai mwaka huu, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kampuni ya Ndege nchini (ATCL), Josephat Kagirwa, alisema kwamba kutokana na nchi nyingi kufunga anga zao, ATCL ililazimika kufunga safari zake za nje mara moja na pia kupunguza safari zake za ndani kwa kati ya asilimia 80 na 90.

Anasema kufungwa kwa anga za nchi nyingi kulisababisha raia wa nchi nyingi kukwama katika mataifa mbalimbali duniani. Hali hiyo ilitoa msukumo kwa balozi za Tanzania nje ya nchi kwa kushirikiana na balozi za nchi husika zilizoko hapa nchini kushirikiana na kutafuta suluhisho la kuwasaidia raia hao na ndipo ATCL ilipata fursa ya kufanya safari maalumu za uokozi.

Kagirwa anasema miongoni mwa safari hizo maalumu za uokozi za nje ambazo ATCL imezifanya katika kipindi hiki cha covid-19 ni pamoja na kuwarudisha Watanzania na wanafunzi wa Tanzania waliokuwa China.

Ndege za ATCL pia ziliwasafirisha raia wa India kutoka nchini Zambia kurudi kwao India na wakati huohuo kuwarudisha raia wa Zambia waliokwama nchini India na kuwarudisha kwao Zambia, kuwarudisha Watanzania waliokwama India, Mauritius na nchi zingine mbalimbali kurudi hapa nchini.

Miongoni mwa Watanzania wengi waliorejeshwa hapa nchini na ATCL kutoka nchi za nje ni pamoja na Watanzania zaidi ya 250 waliokwama China na miongoni mwao walikuwa wanafunzi.

“Mnamo Oktoba 2020, nchi kadhaa zilifungua anga zao na hivyo kuwezesha ATCL kurudisha safari kadhaa katika nchi hizo husika. Mpaka sasa ATCL tumeweza kurudisha safari za Hahaya (Comoro), Entebbe (Uganda), Lusaka (Zambia) na Harare (Zimbabwe) ambapo tunaruka kwenda na kurudi katika nchi hizo mara mbili kwa wiki. Kadiri nchi zinavyofungua anga zao, safari za kawaida za abiria zitarejea na pia tutaanzisha safari katika nchi zingine ambako kuna soko,” anasema Kagirwa wakati huo.

Kabla ya mlipuko wa virusi vya corona mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, ATCL ilikuwa ikitoa huduma ya usafiri wa anga kwa ndege zake kufanya safari za India, Burundi, Zimbabwe, Uganda, Zambia na Afrika Kusini na safari za kwenda China zilikuwa zikiendelea kuratibiwa.

Kwa sasa hali imerejea katika hali yake ya kawaida kwa kuwa ndege za abiria za mashirika makubwa kama vile Qatar Airways, Ethiopian Airlines na Emirates yamerejesha safari zake za kuja hapa nchini ambazo ni muhimu kwa uchumi wa taifa.

Miongoni mwa ndege mpya ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imezinunua na tayari zipo hapa nchini zikiendelea na safari mbalimbali za ndani na nje ya nchi ni pamoja na Boeing 787-8 Dreamliner (mbili), Airbus A220-300 (mbili) na Bombardier Dash 8 Q400 (nne).Wakati huo huo serikali tayari imenunua ndege nyingine tatu ambazo zinategemea kuwasili mapema mwaka 2021 ambazo ni Airbus A220-300 (mbili) na Bombardier Dash 8 Q400 moja.

Katika kuhakikisha ATCL inazidi kuimarika kwa kuwa na ndege za kutosha, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025, imeahidi kununua ndege nyingine mpya tano ikiwemo moja ya mizigo.

Juhudi zote hizi zinakusudia kuhakikisha kampuni inaimarika na kutoa huduma bora kwa Watanzania na wengineo pia kuleta tija kwa taifa kwa ujumla.

Ajira

Kufufuliwa kwa kampuni ya ndege Tanzania kumewezesha Watanzania kupata ajira na utaalamu zaidi katika ndege za kisasa ambao haukuwepo kabla ya kununuliwa kwa ndege hizo za kisasa.

Kagirwa anasema kabla ya kufufuliwa. ATCL ilikuwa na jumla ya wafanyakazi 171 ambao wengi miongoni wao wameshastaafu na wengine bado wanaendelea na kazi. Amesema ATCL imeendelea kuongeza ajira kutokana na uhitaji, hivyo mpaka sasa ATCL ina wafanyakazi 575.

Katika idadi hiyo wamo marubani 73, wahandisi 82, wahudumu ndani ya ndege 110 pamoja na kada nyingine mbalimbali. Anasema lengo la kampuni ni kuwa na uwiano wa wafanyakazi 87 kwa ndege moja ambao mpaka sasa kwa idadi ya ndege na wafanyakazi waliopo uwiano ni wafanyakazi 72 kwa ndege moja.

“ATCL itaendelea kutoa ajira kulingana na ongezeko la ndege lakini bila kuvuka uwiano tuliojiwekea, jambo muhimu hasa ni uhitaji katika kada mbalimbali ndani ya kampuni,” anaeleza Kagirwa.

Columnist: habarileo.co.tz