Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mambo ya kuzingatia kutunga riwaya nzuri- 3

D325f9d1d711f645abed19b8b2074bd2 Mambo ya kuzingatia kutunga riwaya nzuri- 3

Thu, 17 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TUNAENDELEA na makala haya kuhusu mambo muhimu 12 ya kuzingatia wakati wa kuandika riwaya. Tayari tumeshaangalia mambo matano ya kuzingatia na leo tunaendelea na mengine.

Mambo hayo matano ya kwanza ni pamoja na kuibua wazo zuri la hadithi ambalo linaweza kukupa angalau maneno 40,000 na kuendelea. Lakini si alimradi wazo bali linalojenga kisa ambacho kitamvuta msomaji kufunua kurasa moja baada ya nyingine.

Hatua ya pili tukasema ni kuangalia kama unaanza kuandika hadithi yako kwa kudadavua muhtasari wa matukio yatakavyokuwa kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho au unaandika kwa mtindo wa kugundua mapya kadri unavyoendelea kuandika.

Hatua nyingine ni kuunda mhusika mkuu (shujaa) asiyesahaulika ambaye ndiye ataibeba riwaya yako yote sambamba na wahusika wengine akiwemo adui. Jambo la nne ni namna utakavyokuwa unaandika matukio (plot) kuanzia mwanzo wa hadithi, kilele hadi mwisho.

Tukaishia kwa kuangalia eneo la tano la utafiti. Tukaona kwamba ingawa kimsingi riwaya ni hadithi za kubuni, ili imkamate na kumvutia msomaji inapaswa kuwa ya kuaminika na kuleta maana na hivyo utafiti ni lazima. Leo tunaendelea kuangalia maeneo mengine ya kuzingatia.

Kuchagua mtazamo wako

Kuna kuchagua mtazamo wako wakati wa kuandika ambao unatumika kuwapatia wasomaji ujumbe. Huu unahusu zaidi nafsi unayoamua kutumia wakati unaandika riwaya yako. Je, unatumia nafsi ya kwanza, ya pili au ya tatu?

Nafsi ya kwanza ni kama ‘mimi, sisi, yangu au yetu’ kama kinavyoanza kitabu cha Mikononi Mwa Mauti cha Mkongwe Nobert Chiduo: ‘Nilizima taa yenye mwanga mkali na kuwasha ya rangi yenye mwanga hafifu. Halafu nikapunguza sauti ya redio na kujitupa kitandani…”

Unaweza pia kuamua kutumia nafsi ya pili yaani ‘wewe’ kama vile ulikwenda au utakwenda. Ni mara chache sana hadithi zimeandikwa kwa nafasi ya pili, mtindo ambao unatumika zaidi kwenye matangazo.

Lakini katika hadithi yako unaweza kuamua kutumia nafsi ya tatu yaani ‘yeye’ ambayo ndio inatawala zaidi katika hadithi nyingi kama vile kinavyoanza kitabu cha Turufu ya Mwisho cha mtayarishaji wa makala haya: “Baada ya kuweka mizigo yake sawia kwenye hoteli aliyofikia katikati ya mji wa Dodoma, Marina alitoka akiwa na mkoba wake mdogo tayari kumtafuta rafiki yake kipenzi, Stella.”

Inapendeza riwaya yako ikaanza kwa nafsi moja ulioamua kutumia hadi mwisho ingawa nafsi ya kwanza ina tabia ya kumbana mtunzi kwa kwenda na mhusika wake kwa kila anachofanya. Yaani kila tukio linalosimuliwa lazima mhusika ambaye anajisimulia kisa awepo na ndiye anasimulia sifa za wahusika wengine.

Mvuto tangu mwanzo

Katika filamu inasemwa kwamba ili kisa kimkamate mtazamaji, inatakiwa ndani ya dakika nane mtazamaji aone mgogoro. Kwa upande wa riwaya, inatakiwa uhakikishe utakachoanza nacho kwenye ukurasa wa kwanza kinamkamata msomaji.

Ni katika muktadha huo inashauriwa kuanzia kisa chako katikati (medias res) kwa maana tayari mhusika yoko kwenye matendo.

Yaani ikiwezekana anza na kisa cha kitakachomkamata msomaji hata kama hapo unapoanzia ndio katikati ya hadithi.

Unaweza pia ukaanza mwanzo kama mwisho, yaani tukio kubwa la kutisha linatokea ndipo unaanza kusimulia kilichosababisha kama kitabu cha Mohammed Hammie Rajabu cha Nimejitakia.

Kuanza kitabu mwanzo kama mwisho wataalamu huita tukio la papa kula mtu. Yaani kinachoanza ni ‘papa kala mwanafunzi’ kisha masimulizi ya nini kilijiri hadi mwanafunzi huyo kuliwa na papa yanakuja baadaye.

Usianze riwaya yako kwa kusimulia ‘hapo zamani za kale, alikuwepo baba na mwanae, mtoto akasoma…’ bali anza tayari mhusika akiwa yuko katikati ya mkasa.

Shikilia akili ya msomaji

Kama filamu imetungwa kutokana na kitabu (ingawa Tanzania bado hakuna utamaduni huo sana) unaweza kusikia watazamaji wa sinema wakisema walikipenda kitabu zaidi ya filamu? Wakati kitabu cha Simu ya Kifo cha Hayati Faraji Katalambula kilipoigizwa filamu kuna walioona hivyo.

Sababu ni dhahiri: Pamoja na teknolojia ya hali ya juu, watengeneza sinema wakati mwingine wanashindwa kukamata akili ya mtazamaji kama wanavyofanya waandishi wa riwaya.

Taswira ambayo mwandishi anaijenga wakati anaandika riwaya yake inatakiwa iwe ya hali ya juu kiasi kwamba hata waigizaji sinema wajiulize mara mbilimbili wakitaka kukichza kitabu husika kama kweli watafikia taswira iliyokusudiwa.

Kazi yako kama mwandishi siyo kuwafanya wasomaji wafikirie mambo jinsi unavyoyaona, lakini kuchochea aina fulani ya sinema kali kwenye akili zao.

Zidisha matatizo kwa mhusika

Ukiwa tayari umemshika msomaji wako na mwanzo mzuri wa kisa, hakikisha unamtumbukiza mhusika wako mkuu kwenye shida na matatizo makubwa.

Katika mazingira kama hayo, kila hatua anayofanya mhusika ili kujiondoa kwenye shida hiyo mbaya zinapaswa kumpeleka pabaya zaidi.

Kuweka wahusika wengi karibu na mhusika mkuu kunamfanya maisha yake yawe rahisi lakini kinachotakiwa ni kuondoa kila kinachoweza kufanya maisha ya mhusika mkuu kuwa rahisi.

Katika mazingira ya matatizo, mwongezee matatizo kama vile gari lake kuharibika, silaha yake kuibiwa, rafiki yake wa kike kumkataa, kufukuzwa, ofisi yake kuungua moto, mteja au mfadhili wake mkuu kuacha kumfadhili au kufilisika. Akiwa katika mazingira hayo, unazidi kumwingiza katika matatizo ya hatari.

Zingatia kwamba migongano na migogoro ndio injini ya riwaya.

Pamoja na hayo usimfanye mhusika wako mkuu mpumbavu na asiyejielewa. Anaweza kuwa na udhaifu au kasoro fulani lakini upungufu huwa unapaswa kutambulika na mwisho wa siku kubadilika na kuwa ushujaa.

Shida zake kadri zinavyoongezeka kuwe na mantiki kutokana na namna anavyojaribu kujiokoa au kujiondoa kwenye shida.

Kwa mfano, kama hujawaambia wasomaji wako kwamba shujaa wako aliwahi kupitia mafunzo ya karate, haiwezekani ghafla wanamwona anatembeza mkong’oto wa karate kujiokoa!

Unaweza kudokeza kwamba mhusika kadri anavyopambana ndivyo anavyoboresha misuli au rasilimali ambazo zitamwokoa mwisho wa yote, lakini shida zake zinapaswa ziwe zenye kuongezeka kadri kisa kinavyoendelea.

Mazingira kuwa magumu

Mazingira unayompitisha mhusika wako hasa katika kuelekea kwenye kilele cha hadithi yanatakiwa yawe magumu sana.

Fikiria mume wa mtu yuko baa na hawara, halafu mkewe anayempenda sana anaingia pale bila kujua kwamba mumewe yuko pale!

Mtu anaweza kuandika kisa ambacho mwanamke hazai halafu mume na ndugu wanaishia kumbeza, kumtukana na kumfanyia visa hivi na vile. Ni kisa lakini cha kawaida sana.

Lakini fikiria pale mwanamke huyu ambaye hazai na kudhihakiwa mara kwa mara, siku moja anaudhika na kumpiga na kibao cha nazi mumewe na kusababisha kifo chake, kisha akajaribu kuficha maiti ya mumewe na kudai amepotea!

Kisa kinapaswa kijengwe katika mazingira magumu yanayotoka katika mazingira ya kawaida ambayo yataifikisha hadithi yako kwenye kilele kinachomfanya mtu ashindwe kuachia kitabu.

Lete yote kwenye kilele

Kilele ndilo eneo ambalo mhusika mkuu au shujaa wako anaibuka mshindi na ni mahala ambapo adui au mtesi wake anaumbuka, kukamatwa, kuzidiwa au kukubali yaishe.

Yaani ni mahala ambapo mgogoro ambao umekuwa ukifukuta wakati wote unafikia mwisho kwa shujaa wako kumaliza jaribio la mwisho.

Lakini kumbuka kwamba kilele (climax) siyo mwisho wa hadithi bali kuna kitu kinakuja.

Wasomaji waridhike

Ingawa pengine si rahisi kumaliza kila kitu kwa sababu maisha hata ya hadithi lazima yaendelee baada ya shujaa wako kushinda, lakini mwache msomaji wako akiwa ameridhika kwa kutenga muda wake kusoma kitabu chake na pesa aliyotumia kununua kitabu.

Mwache msomaji akiwa ameridhika kwamba adui amepata fundisho, amekamatwa, amefungwa anakiri makosa na mengine kama hayo.

Mwisho wa kitabu hauwezi kuwa wa kuvutia kama kilele, lakini unapaswa uwe ni wenye kufikirisha.

Usiharakishe kumaliza hadithi, bali andika mwisho unaoridhisha kabisa ambao unashusha pazia la kitabu chote kwa kishindo.

Tukutane wiki ijayo

Columnist: habarileo.co.tz