Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mambo sita yaliyoiua Simba

Simba Raja Pic Mambo sita yaliyoiua Simba

Tue, 21 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kupoteza mechi ya pili hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika Simba itakuwa na kazi nyingine leo Jumanne usiku kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili dhidi ya matajiri wa Chamazi Azam FC.

Wachezaji wa Simba kwenye mechi dhidi ya Raja Casablanca hawakuonekana kucheza vizuri na kwenye maeneo mengi walikuwa wamezidiwa pengine ndio maana mchezo uliisha kwa kufungwa mabao 3-0.

Wiki hii inaweza kuwa nzuri kwa Simba kufuta machungu kama itashinda michezo miwili wa ligi dhidi ya Azam FC na baada ya hapo kushinda ugenini na Vipers ya Uganda ila matokeo yakiwa tofauti na hivyo hali itakuwa siyo shwari kwa upande wao.

Ukiachana na hilo, Mwanaspoti kupitia mwandishi maalumu ndani ya Simba linabaini kuna mambo yamechangia timu hiyo kushindwa kufanya vizuri Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi na huenda yakaleta athari hadi katika ligi na Kombe la Shirikisho (ASFC).

DIRISHA KUBWA

Simba kwenye usajili wa dirisha kubwa ilifanya usajili zaidi ya wachezaji watano ila wengi kati ya hao wameshindwa kuwa msaada kwa timu na kutoa mchango wa kutosha pengine tofauti na matarajio yao.

Wachezaji waliyoshindwa kufanya vizuri na walisajiliwa dirisha kubwa, Victor Akpan na Nelson Okwa waliyotolewa kwa mkopo Ihefu, Dejan Georgijevic, aliyekaa kwenye kikosi kwa muda mfupi na kutimkia kutokana na baadhi ya mambo kutokwenda sawa.

Wengine, Nassoro Kapama, Augustine Okrah, Habibu Kyombo bado wapo kwenye kikosi ila wameshindwa kufanya vizuri na hata kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza muda mwingi wamekuwa wakiishia benchi au jukwaani. Moses Phiri mwenye mabao kumi katika ligi na mabao matano Ligi ya Mabingwa Afrika ndiyo mchezaji pekee aliyefanya vizuri hadi sasa Simba aliyesajiliwa dirisha kubwa.

MABADILIKO BENCHI LA UFUNDI

Simba ndani ya msimu huu hadi sasa imefanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwenye awamu tofauti ilianza na kocha, Zoran Maki aliyekuja nchini akiwa na jopo la wasaidizi wake kocha wa viungo, kocha wa makipa na msaidizi.

Ligi ikiwa hata mzunguko wa tano haijafika Zoran alitimka baada ya kupata kazi mpya Misri aliondoka na wasaidizi wake wote timu ikabaki chini ya kocha, Selemani Matola aliyeongoza timu hiyo kwenye michezo kadhaa.

Baada ya muda uongozi wa Simba ulifanya mabadiliko mengine ya kuwaleta makocha watatu kwa awamu tofauti, Juma Mgunda, Sebastian Mkomwa aliyepo Yanga Princeses sasa na Mussa Mgosi aliyerudishwa timu ya vijana.

Matola aliyekuwa anafanya kazi na Mgunda amebadilishwa majukumu na sasa anatumika kama Mkurugenzi wa ufundi wa Soka la Vijana.

Wakati Mgunda akiwa anaendelea na majukumu yake uongozi ulimleta kocha mpya, Oliveira Robertinho aliyopo hadi wakati huu amekuja na wasaidizi wawili kocha wa makipa, Chlouha Zakaria na kocha msaidizi, Ouanane Sellami.

Si jambo la kawaida kwa timu yenye kuhitaji kufanya vizuri ndani ya msimu mmoja kufanya mabadiliko yote hayo katika benchi la ufundi ingawa ni nyakati tofauti lakini hatari zaidi ni kumweka nje Matola ambaye anaweza kuwa na uzoefu mkubwa kuliko makocha wote wa ndani kwenye michuano ya kimataifa kwa sasa.

WACHEZAJI BADO

Ukikifanyia tathimini kikosi cha Simba kina mapungufu kwenye maeneo mengi pengine ndio maana ikikutana na mechi zenye ushindani wa kutosha na nyakati ngumu hushindwa kufanya vizuri kama malengo yao yalivyo.

Kwenye kikosi cha Simba kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa kwenye kiwango bora nyakati zote bila kujali aina ya mechi au ushindani inaokutana nao ila kuna wengine wamekuwa na homa za vipindi kuna nyakati watacheza vizuri ila muda mwingine wanashindwa kufanya hivyo.

Hivi unakumbuka...? kuna nyakati Simba ilikuwa inapitia wakati mgumu baada ya kumkosa kiungo, Clatous Chama aliyefungiwa michezo mitatu, kikosi cha timu hiyo hakikuwa na makali kama akiwepo kiwanjani.

Hiyo si dalili nzuri kwa timu yenye kuhitaji kufanya vizuri akikosekana mchezaji mmoja inakuwa na mapungufu.

USAJILI DIRISHA DOGO

Miongoni mwa eneo lingine Simba imekutana na changamoto hadi sasa ni usajili wa wachezaji wanne waliyosajiliwa kwenye dirisha dogo lililofungwa mwezi uliyopita. Simba dirisha dogo liliwasajili Saido Ntibazonkiza, Ismael Sawadogo, Jean Baleke na Mohammed Mussa.

Sawadogo anapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza ila ameshindwa kuonyesha makali yake anaonekana kuwa mzito wa mwili hadi kwenye maamuzi ingawa nyakati nyingine huwa anafanya kazi nzuri ya kuzuia na kuanzisha mashambulizi.

Mussa hajapata nafasi ya kucheza wakati Saido na Baleke aliyefunga mabao mawili walianza kuonyesha makali yao katika michezo ya mwanzo kwenye ligi ila Ligi ya Mabingwa Afrika bado hajaonyesha hilo.

UCHAGUZI WAWAGAWA

Wiki kadhaa zimepita tangu wanachama wa Simba kukalirisha katika yao kwa kufanya uchaguzi wa viongozi sita, mwenyekiti wa wanachama, Multaza Mangungu na wajumbe wa bodi watano.

Kabla ya uchaguzi huo kulikuwa na makundi mengi tofauti yaliyowagawa baadhi ya wanachama na viongozi wa zamani kuwa tofauti kila mmoja kuvutia upande wake kwa kile alichokuwa anakiamini.

Wakati wa kampeni za uchaguzi Simba kuliibuka mambo mengi hadi mengine yale ya kuchafuana. Basi kama ulikuwa haufahamu jambo hilo halijamalizika hadi leo kwani kuna baadhi ya viongozi na watu wenye nguvu ya ushawishi wamejiweka pembeni na hawatamani kuona timu inafanikiwa.

FRIENDS OF SIMBA

Miongoni mwa watu waliyokuwa na nguvu kwenye soka la ndani na nje ya Tanzania kutokana na kuhudumu kwenye soka nyakati na nyadhifa tofauti ni kundi la (Friends Of Simba), lilikuwa likipigana kuhakikisha timu yao inafanya vizuri nyakati zote.

Nikukumbushe jambo, hii Simba ya hivi karibuni iliyopata mafanikio katika mashindano ya ndani kimataifa ukiachana na pesa alizokuwa anatoa Rais wa heshima, Mohammed Dewji 'Mo Dewji' kulikuwa na nguvu nyuma ya Friends of Simba.

Miongoni mwa watu waliyokuwa wanatengeneza FOS, Mulamu Nghambi, Mohammed Nassoro Kigoma, Zacharia Hanspoppe (marehemu), Crescentius Magori, Salim Abdallah 'Try Again', Musley Ruwey na wengine.

Lilikuwa si jambo la kushangaza kuona maandalizi ya michezo hii ya CAF, miamba hiyo ilikuwa inakutana na kuweka mipango mikakati makini ya kuhakikisha Simba inashinda nyumbani na ugenini.

Si jambo la kushangaza kuona Simba anasafiri kwenye kucheza mechi ya ugenini kuona jopo hilo ni miongoni mwa msafara na wakienda huku walikuwa wanafanikiwa kwenye malengo yao kama ilivyo michezo ya hapa nyumbani.

Kama ulikuwa haufahamu miamba hiyo kwa sasa amegawanyika na hawafanyi kazi pamoja kutokana na kukoasa maelewano ndio maana wakati huu Simba inaweza kwenye kucheza mechi ya ugenini kwenye CAF au mashindano ya ndani ukamuona, Mulamu, Try Again kwa sababu ni Mwenyekiti wa bodi ila wengine wote usiwaone.

Ngoja nikukumbushe tena katika mechi za CAF, Simba ikiwa nyumbani Mulamu ndio alikuwa msimamizi wa mambo mengi hadi uwanjani ila kwenye ya Raja Casablanca wala hakuonekana.

Itakuwa ngumu kwa Simba kufanya vizuri kwenye mashindano ya CAF hata ya ndani kama miamba hiyo isipokaa chini kwa pamoja kumaliza tofauti zao na kuelewana. ushauri

Mambo ni mengi, lakini ushauri wetu ni Simba kusimama pamoja na kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kama walivyokuwa wanafanya awali, waungane, wavunje makundi ya uchanguzi, waboreshe benchi la ufundi ili kuhakikisha mechi zijazo wanashinda.

Columnist: Mwanaspoti