Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mama Samia anatema kushoto, anafukia kulia

Feisal Azam E38.jpeg Mama Samia anatema kushoto, anafukia kulia

Wed, 14 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Unaelewa nini unapoambiwa kuhusu kiungo fundi uwanjani? Jibu jepesi ni kama ukimuona Clatous Chama wa Simba au Salumu Abubakar 'Sure Boy' wa Yanga.

Hao ni baadhi ya viungo bora tulionao kwenye Ligi Kuu Bara ambao wakiwa na mpira unaweza kuwatafsiri kwa Lugha ya soka 'wanatema kushoto na kufukia kulia' hali ambayo ni sawa na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan michezoni.

Naam! Viungo bora siku zote wanakuwa na sifa ya 'Kusambaza upendo', kwa maana ya kupiga pasi maeneo yote uwanjani, kushoto, kulia, mbele na nyuma na hilo ndio chimbuko la neno 'Kiungo anatema kushoto na kufukia kulia'.

Kuna muda utadhani anapiga pasi kulia, akaipeleka kushoto na muda unadhani anaenda mbele ghafra akageuka na kuanza nyuma, na hivyo ndivyo Rais Samia anafanya kwa sasa michezoni.

Unaweza kudhani anaipendelea sana Yanga kutokana na kuhusika nayo kwa sasa kwenye kila hatua inayopiga lakini ukikumbuka ndiyo klabu iliyofanya vizuri zaidi msimu huu kulinganisha na timu nyingine za Tanzania basi unaamua kuacha aendelee kuwapa maua yao Wananchi.

Jumatatu wiki iliyopita, Rais Samia aliialika Yanga Ikulu, Dar es Salaam kuipongeza kwa kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupata medali za fedha ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa wababe hao wa Jangwani kufika hapo pia ikiwa ni mara ya pili kwa timu ya Tanzania kucheza fainali ya CAF, tangu Simba ilipofanya hivyo 1993.

Ilikuwa ni sherehe ya Yanga lakini Rais Samia pia aliwaalika watu wa Simba, Azam na timu nyingine na katika hotuba yake aliwataka wote kwa pamoja kuhakikisha wanajenga timu zao ili zifanye vyema kwenye michuano ya kimataifa na kuiletea nchi heshima sambamba na kutengeneza misingi itakayozisaidia timu za taifa.

Kwa lugha ya soka hapo ametema kushoto, akafukia kulia. Mara ngapi Shughuli za Yanga, Simba na Azam wanaalikwa? Mara chache sana.

Achana na soka pia katika hafla ya Ikulu aliwaalika wadau wengine wa michezo na burudani wakiwemo wachambuzi, wanahabari, wasanii, waogeleaji na mabondia waliowakilishwa na Karim Mandonga 'Mtu Kazi' na wakati alivyokuwa akitoa hotuba baadhi yao aliwataka kama wewe unavyotaja majina ya marafiki zako kiulaini.

HAMASA USIPIME

Rais Samia hajaanza kutoa hamasa kwa Simba na Yanga tu kupitia kampeni ya 'Goli la Mama' ambapo alikuwa akiwajaza minoti Simba na Yanga kwenye kila bao walilofunga katika mashindano ya CAF ambapo Simba ilikuwa Ligi ya Mabingwa na Yanga, Kombe la Shirikisho bali alikuwepo tangu mwanzo.

Achana na Juzi Yanga kuitwa Ikulu, timu ya taifa ya Wanawake, 'Serengeti Girls' ndiyo ilikuwa ya kwanza kutinga Ikulu kama timu ya soka chini ya uongozi wa Rais Samia, nakumbuka ilikuwa Oktoba 21, 2021, baada ya kubeba ubingwa wa kusini mwa Afrika (Cosafa) na hakuishia hapo aliwapa wachezaji wale viwanja kule Dodoma ikiwa ni kama hamasa.

Baada ya hapo waliofuata kutinga Ikulu walikuwa timu ya taifa ya soka la Walemavu 'Tembo Warriors' Desemba 7, 2021, baada ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia na alikula nao chakula cha mchana akawapa hamasa ya maneno na kisha kuwachangia pesa iliyowasaidia katika fainali zile. Hizo ni baadhi ya hamasa za Rais Samia katika soka.

KODI NA MAPATO

Kama unakumbuka Rais Samia alipoingia madarakani alifuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa nyasi bandia ambazo zinaingia nchini. Hiyo ilikuwa ili kusaidia kupatikana zaidi kwa viwanja vipya vya michezo na kujenga vipya.

Pia katika hotuba yake ya Jumatatu alieleza kuwalegezea kamba wadhamini wa timu za Tanzania huku akiwataka kuongeza ufadhili katika timu hiyo akimtumia mfadhili wa Yanga, Gharib Said (GSM) kwa niaba ya wengine.

"GSM mimi sikubinyi kabisa, zile ambazo sikubinyi zipeleke katika michezo, huko ndiko Mungu alilokupangia," alisema Rais Samia.

Aidha alisema amewaelekeza makampuni ya kubashiri kuelekeza asilimia tano ya fedha wanazozipata kuipeleka michezoni ili kuendelea kukuza michezo nchini. Hivyo ni baadhi ya vitu ambavyo vikizingatiwa vitaongeza kasi ya ukuaji wa michezo nchini.

UMOJA NA UUNGWANA

Kama ilivyo kwa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kuhamasisha uungwana 'Fair Play', ndivyo ilivyo kwa Rais Samia pia ambaye amekuwa msitari wa mbele kweye kuhamasisha uungwana michezoni.

Moja ya mambo ya kiungwana aliyoyahamasisha Jumatatu pale Ikulu, ni pamoja na kuitaka Yanga kukaa pamoja na nyota wake Feisal Salum 'Fei Toto' waliye kwenye mgogoro wa kimkataba ili wayamalize.

Rais Samia alisema: "Viongozi wa Yanga nina ombi kwenu, sifurahii kusikia mnakuwa na mizozo na wachezaji, na sitaki kusema mengi, nataka niwaambie tu, hii ishu ya Fei Toto, hebu kaimalizeni.

"Kaimalizeni ili tuangalie mbele sasa, haipendezi klabu kubwa kama hii iliyofanya kazi nzuri, mnakuwa na ka ugomvi na katoto. Hebu kamalizeni mwende vizuri. Nitasubiri kupata mrejesho wa hili, siku yeyote mkiwa tayari karibuni nyumbani mje kunipa mrejesho."

Pamoja na hayo pia alizieleza mamlaka zote zinazosimamia michezo nchini kufanya kazi zao kwa ueledi bila ubaguzi wala kupendelea upande wowote na kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi kubwa katika michezo Afrika na Dunia nzima kwa ujuma.

Columnist: Mwanaspoti