Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Makosa yanayotokana na kutozingatia alama za uakifishaji

C49cbacd8c07f29a5562280c84e2f87a Makosa ya Alama za uakifishaji

Fri, 13 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

LUGHA ya Kiswahili inakumbana na changamoto nyingi sana katika ukuaji wake. Changamoto hizo zinasababishwa na mambo mengi ikiwapo watumiaji wenyewe wa lugha hii ya Kiswahili.

Moja ya sababu ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili kufanya makosa ni kutozingatia alama za uakifishaji. Licha ya kuzidadavua alama za uakifishaji, pia tutaangazia mazingira sahihi ya matumzi ya herufi kubwa, yaani ni wapi hasa ni mahali sahihi pa kutumika herufi kubwa.

MAANA YA UAKIFISHAJI

Uakifishaji ni utumiaji wa alama za uandishi katika maandiko ili kumfanya msomaji asipate utata katika kupata maana. Maandiko hayo yanaeleweka vizuri kwa msomaji au hadhira kwa usahihi zaidi kama alama hizo zitatumika vyema.

Katika lugha ya Kiswahili kuna makosa mengi yanayofanywa na watumiaji wa lugha hii katika maandishi, pengine watumiaji wa lugha hii wanafanya makosa hayo bila kujua ama kwa uzembe tu.

Upuuzaji huu wa makosa huwajengea mazoea watumiaji na kuwafanya wawe sugu katika kufanya makosa. Vilevile, kuna makosa yanayojitokeza ndani ya lugha hasa yale ya kutozingatia matumizi ya herufi kubwa katika maandishi, hili nalo limekuwa tatizo kubwa kwa baadhi ya watumiaji wa Lugha ya Kiswahili katika maandishi hasa kutokufahamu mazingira sahihi ya kutumia herufi.

Kwa leo katika makala haya, tutaangazia matumizi sahihi ya alama za uakifishaji. Aidha, tutaonyesha namna sahihi ya kutumia alama zote za uakifishaji pamoja na kuonyesha mazingira sahihi ya kimatumizi ya herufi kubwa katika maandishi. Alama za uakifishaji ni pamoja na hizi zifuatazo: Nukta au kituo (.) mkato (,), nuktamkato (;), nuktapacha (:), kiulizo (?), mabano ( ), parandesi {}, wimbi (\), mtai (/), mshangao (!) bila kusahau kujadili mazingira sahihi yanayotakiwa kutumia herufi kubwa katika maandishi.

Kwanza kabisa tuanze na alama mojawapo ya uakifishaji ambayo ni nukta (.). Alama hii huashiria kituo kikubwa ambapo ndiyo mwisho wa sentensi. Hivyo, basi endapo mtumiaji wa lugha ataweka alama ya nukta mahali pasipo sahihi bila shaka atapotosha ujumbe au maana iliyokusudiwa haitawafikia walengwa sawasawa.

Nukta au kituo kikuu hutumika katika mazingira yafuatayo: Alama hii hutumika katika maandishi kuonesha kuwa sentensi imefika mwisho. Mfano: Waliokuja jana wasogee mbele

Katika sentensi hii msomaji hawezi kuelewa kuwa imefika mwisho au inaendelea kwa kuwa hakuna kiashirio chochote kinachomwongoza msomaji. Lakini mtu akiandika, Waliokuja jana wasogee mbele. Sentensi hii imefika mwisho kwa kuwa kuna alama inayoashiria mwisho ambayo ni alama hii (.)

Vilevile, nukta huweza kutumika wakati wa kuandika herufi za vifupisho vya maneno yanayotokana na maneno mawili au zaidi. Mfano: k.v., k.m., K.K., K.n.y. kirefu chake kama vile, kwa mfano, kupitia kwa au kabla ya Kristo na kwa niaba ya.

Pia, nukta hutumika katika kuandika vifupisho vya vyeo vya watu na heshima. Mifano: Dk., Mhe., Mch., Bw., Bi., Prof., n.k. Maneno haya yana kirefu chake kama vile, Daktari, Mheshimiwa, Bwana, Bibi na Profesa.

Kwa kupitia matumizi haya ya nukta watumiaji wa lugha hii ya Kiswahili katika maandishi bado wanasahau sana kutumia alama hii ya uakifishi (.) kwenye majina ya vyeo vya watu na heshima. Mfano: Neno Daktari kifupi chake ni Dk. Lakini watumiaji wa lugha hii ya Kiswahili wengi wao wanaandika Dk jambo ambalo ni kosa wanasahau kuweka kituo (.) ili kuonyesha kuwa ni cheo cha mtu lazima alama hiyo ionekane. Lakini hii inaweza tu kutumika kama mtindo wa chombo cha habari. Kwa mfano mtindo wa gazeti hili hautumii nukta kwenye Dk au Sh kuonesha kifupi cha shilingi.

Nukta hutumika pia wakati wa kuandika kiasi cha fedha (kama ilivyodokezwa hapo juu), vipimo mbalimbali vya desimali na katika kutenga saa na dakika, tarehe, mwezi na mwaka. Mfano: Shilingi 82.55, saa 12.15, kilogramu 2.73, tarehe 26.6.2021

Jambo la kuzingatia katika matumizi ya nukta ni kwamba, katika vipengele vilivyoorodheshwa nukta isitumike kwa kila kipengele isipokuwa kwenye kipengele cha mwisho. Mfano: Katika kipindi kijacho tutajadili mada zifuatazo:

a) ufugaji

b) ukulima

c) kisomo chenye manufaa.

Alama nyingine ya uakifishi ni nuktapacha (:), Alama hii hutumika baada ya neno au kifungu cha maneno kinachofuatwa na maelezo au ufafanuzi zaidi kwa kutaka kutaja idadi au maelezo yaliyopangiliwa hatua kwa hatua.

Mifano: Alipofika sokoni alijipatia mahitaji yafuatayo: Nyanya, vitunguu, nyama na matunda.

Ili kufika huko fuata njia ifuatayo: Pita kushoto, vuka mto na panda kulia. Pia, alama hii hutumika katika kukamilisha jina la mada au sura.

Mifano: “Mashujaa wa Tanzania: Mkwawa wa Uhehe.”

“Lugha ya Kiswahili: Chimbuko lake.”

Hata hivyo, nuktapacha huweza kutumika katika kutenga sura, aya, hasa katika maandiko matakatifu. Mifano: AL-MAIDA: 96 -100.

LUK.7:10-8.

Hivyo basi katika maandishi iwapo mtu au mtumiaji wa lugha asipojua matumizi sahihi ya alama ya nuktapacha, atashindwa kuitumia vyema katika maandishi kwa kuwa hataelewa ni wapi sahihi pa kutumia alama hiyo.

Angalizo: Vilevile nuktapacha inaweza kufuatwa na kistari au deshi hasa kabla ya kutaja mambo yanayokusudiwa kuorodheshwa. Mfano: Jarida la Kiswahili hushughulikia nyanja zifuatazo:-

Hizi ni baadhi ya alama za uakifishaji lakini hatuwezi kuzungumzia alama hizi bila kugusia matumizi sahihi ya kutumia herufi kubwa katika uandishi.

Katika kujadili makosa mbalimbali yanayojitokeza katika lugha ya Kiswahili katika maandishi ni pamoja na kutokujua mazingira sahihi ya kutumia herufi kubwa katika maandishi. Katika sehemu hii hebu tuangazie matumizi ya herufi kubwa.

Makosa yanayojitokeza ndani ya lugha yapo mengi sana hasa ya kutokuzingatia matumizi sahihi ya herufi kubwa katika maandishi, haya ni makosa yanayofanywa na watumiaji wa lugha katika maandishi. Hivyo tutaonyesha mazingira tofauti tofauti yanayofaa kutumia herufi kubwa.

Kwa kawaida herufi kubwa hutumika kwa usahihi katika mazingira yafuatayo: Wakati wa kuandika herufi ya kwanza ya neno la sentensi bila kujali aina ya neno kwa maneno mengine, herufi kubwa hutumika pale ambapo sentensi inapoanza. Mfano: Alipofika alihitaji kusomewa mapato na matumizi ya Fedha za Serikali. Elimu bila malipo kwa wananchi ni kipaumbele cha Serikali ya CCM. Kwenye sentensi hii, herufi kubwa A na E zilizokolezwa rangi ndizo zinazoonyesha mwanzo wa sentensi.

Neno linaweza kuwa la kwanza katika sentensi ya kwanza ya habari au aya au pia baada ya vituo vikuu vya uandishi vifuatavyo: Nukta, kiulizo, mshangao, alama ya nukuu na nuktapacha.

Aidha, herufi kubwa huandikwa wakati wa kuandika herufi ya kwanza ya majina yafuatayo: Wakati wa kuandika majina ya miji mbalimbali, lugha mbalimbali n.k, nchi na hata bara fulani kwa mifano: Asha, Juma, Mpanda, Tabora, Tanzania, Afrika.

Vilevile, herufi kubwa huandikwa wakati wa kuandika majina ya pande za dira kama ifuatavyo: Kaskazini, Kusini, Mashariki, Magharibi, Kusini, Mashariki n.k.

Aidha, herufi kubwa huandikwa pale anapoandika majina ya vyeo au heshima. Mfano: Rais, Shehe, Diwani, Meya, Mheshimiwa, Bwana, Bibi, Mwadhama n.k.

Si hivyo tu bali herufi kubwa zinatumika kwa usahihi wakati wa kuandika majina au sifa zinazoandamana na majina ya pekee. Mifano: Ziwa Nyasa, Bahari ya Hindi, Mlima Kilimanjaro.

Majina ya uraia, kabila, lugha au dini nayo ni miongoni mwa maneno ambayo aghalabu huandikwa kwa herufi kubwa kama hakuna sababu maalumu inayoelekeza kuandikwa kwa herufi ndogo. Mifano: Mtanzania, Mwafrika, Mwingereza, Mkristo, Mwislamu, Msukuma, Kiswahili, Kiajemi n.k.

Vilevile, herufi kubwa hutumika kuandika msamiati uliotokana na finyanzo zinazotengenezwa kwa kufupisha baadhi ya majina ya vyama, mashirika au jumuiya fulani.

Mifano: TAMISEMI, BAKITA, UWAVITA, BAKIZA, UKUTA, TATAKI (isipokuwa kama ni mtindo wa gazeti. Kwa mfano katika gazeti hili funyanzo zinazotamkika kama zilizotolewa mfao hapo huandikwa kwa herufi ndogo isipokuwa zisizotamkika kama vile ITV au TCRA).

Majina ya siku, miezi pia huanza na herufi kubwa. Mifano: Jumatatu, Ijumaa, Februari, Aprili.

Majina ya vitabu na mada mbalimbali katika uandishi. Mifano: Kusadikika, Nagona, Mzingile “Athari za UKIMWI katika Maendeleo”.

Majina ya sikukuu mbalimbali za dini na za kitaifa, mfano: Muungano, Iddi El Fitri, Pasaka, Krismasi. Majina ya sayari, Pluto, Zuhura, Zebaki na majina ya nafsi yatakapotumika kuleta maana maalumu. Mifano: Mpaji, Muumba, Mungu, Yarabi na Mola.

HITIMISHO

Alama za uakifishaji katika maandishi ni muhimu kwa kuwa husaidia katika kuufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa wasomaji.

Ikitokea hazikutumika vyema unaweza kuleta utata kwa msomaji wa taarifa au andiko lililokusudiwa. Tazama mfano ufuatao; ameombewa Rehema na Ameombewa rehema. Kwa mtumiaji wa lugha hapa atajua kuwa Rehema (katika sentensi ya kwanza) ni jina la mtu na rehema (katika sentensi ya pili) ni dua njema ambazo Mwenyezi Mungu ndiye anaweza kumpatia wema huo.

Columnist: www.habarileo.co.tz