Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Makocha wazawa kwa sasa ‘wamefia’ wapi?

Mkwasa Nyingine Charles Boniface Mkwasa

Mon, 10 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ghafla nimemkumbuka marehemu Sylvester Said Mziray 'Super Coach' a.k.a Mwanangu. Kocha mmoja bishoo kuwahi kutokea Tanzania. Alikuwa anajipenda kuliko kujipenda kwenyewe.

Kocha wa mpira haswa. Mtaalamu wa ufundi. Mtanashati. Kocha pekee mzawa kuwahi kufundisha Simba na Yanga. Inavutia sana.

Katika ubora wake Mziray alikuwa kocha wa maana sana. Alikubalika ndani na nje ya nchi. Tuachane na Mziray kwanza. Twende kwa Sunday Kayuni. Mkufunzi wa makocha sasa pale CAF. Kayuni ni miongoni mwa makocha wachache Tanzania kuwahi kufundisha soka nje ya nchi kwa kiwango bora sana.

Kayuni alifanya makubwa sana pale Kenya akiwa na AFC Leopards. Alikuwa kocha tishio pale. Ameacha rekodi na historia kibao katika nchi ya ugenini. Ndiye aliyewapa Ingwe taji la 12 na la mwisho la Ligi Kuu Kenya mwaka 1998, kwani baada ya hapo hadi leo imekuwa ikilisotea kulirejesha likiwa linapitia mikononi mwa mashemeji zao, Gor Mahia 'K'Ogalo' na Tusker FC na timu nyingine.

Leo Hii haishangazi kumuona Kayuni akitumika kama Mkufunzi wa makocha. Katika ubora wake alifanya kazi kubwa sana.

Vipi kuhusu Abdallah Kibadeni? Kocha wa maana kuwahi kutokea pia katika historia ya Simba. Wengi wanamkumbuka kwa kuifikisha timu katika fainali ya CAF mwaka 1993.

Ila ukiachana na hapo Kibadeni ameifundisha Simba kwa ubora mkubwa katika nyakati tofauti. Kila Simba ilipotaka kocha mzawa ingemchukua Kibadeni. Hakuchukuliwa kama kocha msaidizi bali mkuu wa benchi la ufundi.

Kibadeni amefundisha timu nyingi nchini kwa ubora sana. Ni kocha wa heshima. Itakuwa dhambi tukiacha kumzungumza Charles Boniface Mkwasa. Kocha wa maana sana. Ameifundisha Yanga kwa nyakati tofauti.

Amekuwa kocha wa timu nyingi nchini wala Huwezi kuzitaja kwa majina. Amekuwa mpaka kocha mkuu wa Taifa Stars. Inafurahisha sana.

Kwa kifupi nchi imepitia nyakati za makocha bora wazawa.

Vipi kuhusu Juma Mwambusi. Huyu aliifanya Tanzania Prisons kuwa timu tishio. Walimaliza nafasi ya pili kwenye Ligi msimu wa 2008/09.

Prisons ikashiriki michuano ya Kimataifa. Baadaye akafundisha timu nyingine nyingi ikiwemo Mbeya City. Wengi wanaukumbuka ule msimu bora wa 2013/14. Ile Mbeya City dume.

Ilikuja na moto kweli kweli. Ikavisimamisha vigogo Simba na Yanga. Ikamaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi. Mpaka Leo watu wanaikumbuka ile Mbeya City. Watu watanielewa nikiacha kumzungumzia John Simkoko. Kocha mzawa wa mwisho kushinda taji la Ligi Kuu Bara. Alifanya hivyo na Mtibwa Sugar tena mara mbili mfululizo.

Ameishi kwenye mioyo ya watu wa Manungu hadi leo. Wengi wanaikumbuka ile Mtibwa yake. Marehemu Joel Bendera hadi leo anakumbukwa kwa kutupeleka Afcon kwa mara ya kwanza mwaka 1980. Ilikuwa ni historia kubwa kwa nchi. Ilichukua miaka 39 kufuzu tena. Sio hivyo tu, lakini akiwa shabiki wa Yanga aliacha mapenzi nyuma na kuisaidia Simba kwenda kupindua meza mbele ya Wazambia Mufulira Wanderers iliyokuwa imeshinda jijini Dar es Salaam kwa mabao 4-0.

Simba ilienda kumduwaza hadi Rais wa Kwanza wa Zambia, Kennedy Kaunda kwa Simba kushinda mabao 5-0 katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1979. Rekodi ambayo haijawahi kuandikwa popote kwenye mechi za kimataifa kwa timu kupindua meza kwa ushindi kama huo. Mungu Amrehemu, katika nyumba ya milele.

Ni ngumu kuwataja wote. Lakini kuna David Mwamwaja, Mungu amrehemu. Dan Koroso, Mbwana Makatta, Mohamed 'Adolf' Richard, Fred Felix 'Minziro', Mohammed Msomali na wengineo kibao. Ni jambo la kujivunia sana.

Ila nini kimetokea hapa katikati? Makocha wazawa wamepotea kwa kasi kama komputa za chogo. Wamekuwa adimu kwei. Hawaaminiki kabisa.

Hebu jiulize kwenye Ligi Kuu kwa sasa ni timu ngapi zinafundishwa na makocha wazawa? Ni chache kuliko uchache wenyewe.

Ni Geita Gold, Tanzania Prisons, Ruvu Shooting, Kagera Sugar, Namungo, Mtibwa Sugar na Ihefu. Timu zote hizi kama hazipo chini kwenye msimamo wa Ligi basi zipo katika daraja la kati. Hazina ushindani mkubwa.

Ni kocha gani Mzawa wa mwisho kufundisha Simba au Yanga? Mara ya mwisho Simba kuwa chini ya Mzawa ni mwaka 2014 walipokuwa chini ya Kibadeni.

Ni hadi mwanzoni mwa msimu huu walipomchukua Juma Mgunda kukaimu nafasi hiyo. Hata hivyo licha ya kuwa na leseni kubwa na kufanya vizuri bado walishindwa kumwamini na kumletea Roberto Oliveira kwaajili ya mechi za makundi za CAF.

Vipi kuhusu Yanga? Ni miaka mingi sana hawajawa chini ya mzawa. Kuna wakati Mkwasa alikaimu hapa katikati lakini baada ya hapo hawajamwamini mzawa mwingine.

Ukweli ni kwamba kwa sasa hatuna kizazi bora sana cha makocha wazawa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Hawa kina Zuberi Katwila, Seleman Matola, Shadrack Nsajigwa, Nizar Khalfan na wengineo wana kazi kubwa sana ya kufanya ili kuwa bora na kuaminiwa kama watangulizi wao. Vinginevyo tutachukua sana makocha wageni kutoka nje.

Columnist: Mwanaspoti