Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Makaka alia na ishu ya hujuma

Makaka Pic Makaka alia na ishu ya hujuma

Fri, 17 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pamoja na kazi nzuri anayoifanya uwanjani, lakini kipa wa Mtibwa Sugar, Mohamed Makaka amesema huwa anasikitishwa na kuumizwa na maneno ya baadhi ya wadau wa soka wanaomtuhumu kuhujumu timu, akieleza kuwa huwa anaamua kuwapotezea.

Makaka alianza rasmi soka la ushindani akicheza ligi kuu tangu msimu wa 2014/15 alipoipandisha Stand United na kudumu nayo hadi iliposhuka daraja 2018/19.

Kipa huyo mwenye rekodi tamu na chungu za kupandisha na kushusha timu, kwa sasa anakipiga Mtibwa Sugar na amekuwa na mwenendo mzuri licha ya kupotea kwa kipindi kifupi uwanjani baada ya kuumia mkono.

Katika mazungumzo na Mwanaspoti, Makaka amefunguka mengi ikiwamo tuhuma wanazompakazia za kuhujumu timu na kwamba huwa zinamkondesha sana, ila tu huamua kupotezea.

TUHUMA ZENYEWE

Makaka anasema pamoja na soka kuwa mkombozi wa wengi kwa vijana kutokana na kujikwamua kiuchumi, lakini wapo baadhi ya watu wenye nia mbaya kumdhoofisha wachezaji kwa maslahi yao binafsi.

Anasema mpira ni mchezo wa wazi lakini wapo wadau ambao kazi yao ni kuharibu jina la mtu akibainisha kuwa skendo ambazo huwa anapata zinamchafua sana ni basi tu hunyamaza kutogombana na kila mmoja.

Anasema asilimia kubwa timu inapocheza na vigogo wa soka nchini, Yanga na Simba huwa zinaacha makovu na maumivu kwa wengi na kubainisha kuwa hata yeye hazijamuacha salama.

Anafafanua kuwa msimu wa 2020/21 akicheza Gwambina alijikuta nje ya orodha ya wachezaji wa kuanza dhidi ya Yanga kutokana na maneno ya watu kuwa anauza mechi.

“Ila utakuta wengi viongozi ni Simba na Yanga, kwahiyo ukicheza mfano na Simba ukafanya vizuri kisha ile ya Yanga ukapoteza wanafikiria mengine na kuanza kuzusha,”

“Nilishangaa sana ile mechi ya Yanga nimepangwa kuanza lakini walibadili maamuzi ya ghafla na kumpanga aliyekuwa mpinzani wangu, yote ni kutokana na maneno ya kashfa,”

“Sijawahi na haitatokea nikauza au kushiriki kwa namna yoyote kuuza mechi au kuhujumu timu yangu kwa sababu mpira ndio maisha yangu,” anasisitiza kipa huyo

REKODI YAMSHTUA

Kipa huyo anasema licha ya rekodi nzuri aliyonayo ya kupandisha timu, lakini muda mwingine huwa anawaza sana ishu ya kushusha timu na humfanya kuwa na wasiwasi japokuwa huamua kukomaa.

Anasema kuwa baada ya kupandisha Stand United ‘Chama la Wana’ lakini baadaye alishuka nayo kisha alipojiunga na Gwambina mzimu uliendelea kumfuata.

Anabainisha kuwa pamoja na yote kwa sasa anaendelea kujiimarisha kuhakikisha anaonesha uwezo na juhudi ili kuisaidia Mtibwa Sugar kufikia malengo.

“Lazima muda mwingine uwaze kwa sababu kushusha timu siyo kitu kidogo, kupandisha inaweza kuwa rahisi kwa mchezaji kwa sababu ni mafanikio ya wengi,” anasema Makaka.

KUHAMA TIMU

Hadi sasa kipa huyo ameshacheza timu nne tofauti tangu aanze soka la ushindani jambo ambalo amelifafanua akiweka sababu zinazomfanya kuhamahama timu.

Makaka anasema zipo sababu zaidi ya moja zinazofanya kubadili timu ikiwa ni kusaka changamoto mpya japo kubwa zaidi ni maslahi na kwamba ataendelea kuhama.

Katika timu alizotumikia ni pamoja na Stand United, Ruvu Shooting, Gwambina na sasa anakiwasha Mtibwa Sugar ambapo atakuwepo hadi mwisho wa msimu huu.

“Kwa sasa mpira ni ajira na maisha ya mtu, lazima kuangalia wapi kuna ulaji mzuri japokuwa mengine ni kutafuta changamoto mpya,” anasema kipa huyo.

Hata hivyo anaongeza pamoja na kuhama timu, zipo changamoto kwani kuingia kwenye mfumo wa kocha kukuamini kuliko wenyeji inahitaji nguvu na juhudi binafsi.

Anasema mara kadhaa wenyeji wanakuwa wameshatengeneza nafasi zao, hivyo inahitaji kwenda na kitu cha ziada haswa unapopata nafasi upige kazi.

“Tatizo linakuwepo kwa sababu kwenda ugenini unakuta wenyeji hivyo lazima kumuonesha kitu cha ziada kocha ili kukuamini na kukupa nafasi,” anasema.

KIWANGO CHAKE

Ni wazi kuwa Makaka kiwango chake huwa hakibadiliki, ambapo mwenyewe anaweka wazi siri yake kuendelea kulinda ubora wake ni kutokana na mazoezi binafsi.

Anasema anapokuwa likizo au nje ya uwanja huwa hatulii isipokuwa muda mwingi huwa anapiga tizi binafsi jambo ambalo limeendelea kumpa ufanisi kazini.

Anaeleza kuwa hata baada ya kupotea uwanjani kwa siku za karibuni baada ya kuumia mkono, hakuwa analala tu isipokuwa aliweka vyema ratiba za matibabu na mazoezini.

“Zaidi ni mazoezi binafsi ambayo yananipa nguvu na kulinda kipaji changu, tangu Agosti nilipatwa majeraha ya mkono nikawa nje ila niliweka vizuri ratiba kuhakikisha sipotezi kitu,” anasema.

Anasema ushindani kwenye ligi ni mkubwa hata wa namba kikosini, lakini anaamini kwa hali waliyonayo haswa morali watafanya makubwa msimu huu.

“Ushindani kuanzia wa namba hadi kwenye ligi ni mkali sana, lakini tunaendelea kupambana na kwa mwenendo wetu kwa sasa naona tunaweza kumaliza nafasi sita za juu,”

“Nashukuru tangu nimerejea uwanjani nimecheza mechi tatu na hatujapoteza tangu mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC), kisha Prisons na juzi dhidi ya Dodoma Jiji,” anasema.

AWATAJA KASEJA, DIARA

Nyota huyo anasema tangu aanze kazi ya mpira anakoshwa na ubora wa mkongwe, Juma Kaseja na amekuwa akimfuatilia muda mrefu kutokana na kile alichofanya enzi zake.

Anasema kwa misimu mitatu ya sasa, kipa wa Yanga Djigui Diara amekuwa akimkosha sana na ufanisi wake golini na anachukua somo kubwa kutoka kwa staa huyo wa kimataifa raia wa Mali.

Anasema japokuwa wapo makipa wengine anaojifunza kupata vitu akiwamo Aishi Manula, lakini Kaseja na Diara ni bora zaidi kwake na anajifunza mengi kutoka kwao.

“Kaseja ni kipa wangu wa muda wote, Diara kwa sasa namuona kama mchezaji mwenye uwezo mkubwa akicheza kwa ufasaha hana papala golini, japo hata Manula amerejesha ubora wake,” anasema Kipa huyo.

NJE YA SOKA

Mchezaji huyo anasema kama asingeingia kwenye mambo ya mpira basi kwa sasa angekuwa dereva wa malori kwani anayo taaluma ya udereva aliyoipata chuo cha ufundi stadi (Veta), Tabora.

Anasema licha ya kutoendelea sana, lakini anayo leseni ya udereva wa gari ndogo japokuwa hesabu zake zilikuwa ni kuendesha malori.

“Nina leseni ya gari za kawaida ila nilitamani kuendesha malori, ila mpira ulinipenda zaidi na siwezi kujutia kwa sababu ndio unaendesha maisha yangu na familia kwa ujumla,”anasema kipa huyo.

Columnist: Mwanaspoti