Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Majeraha ya Messi yapo hivi

Messi Ankle Majeraha ya Messi yapo hivi

Thu, 18 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Usiku wa Jumapili katika mchezo wa fainali ya mashindano ya Copa Amerika 2024 kwa mara nyingine tena Argentina ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo baada ya kuifunga nchi ya Colombia bao 1-0.

Mashindano hayo yaliyofanyika Marekani na fainali hiyo iliyochezwa jijini Miami kwenye Uwanja wa Hard Rock ililazimika kuongezwa dakika 30 za ziada mara baada ya kutoka sululu katika dakika 90.

Wakiwa na nahodha wao Lionel Messi ambaye siku hiyo alipata majeraha ya kifundo cha mguu wa kulia na kulazimika kutoka ndani ya uwanja katika dakika ya 64.

Katika fainali hiyo ilishuhudiwa mchezaji bora mara nane akiumia kifundo hicho mara baada ya kujipinda vibaya wakati akijaribu kuufukuza mpira kwa kasi ili apige krosi dakika ya 36. Messi alipatiwa huduma ya kwanza kwa dakika kadhaa nje ya uwanja na kufanikiwa kurudi uwanjani, lakini bado alionekana kuwa hayupo vizuri kwani alionekana akichechemea.

Mchezaji huyo alivumilia hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika na kwenda mapumziko ambapo timu ya madaktari ilikuwa ikihangaika kumpa hudumu kadhaa ikiwamo dawa za maumivu.

Kipindi cha pili aliendelea na mchezo, lakini katika dakika ya 62 kifundo hicho cha mguu wa kulia kilipata shida tena mara baada ya kujipinda vibaya wakati akijaribu kumpokonya mpira mchezaji wa Colombia. Kujipinda vile kwa kifundo ilikuwa ni uelekeo hasi ndiko kulizidisha jeraha katika kifundo hicho ambacho tayari kilikuwa kimepata jeraha kipindi cha kwanza.

Tangu kuanza kwa mashindano ya Copa Amerika, Messi alikuwa akitazama hali yake kutokana na kupata majeraha ya mguu akiwa na klabu yake ya Inter Miami.Mchezaji huyo ambaye ana umri wa miaka 37, alitoka uwanjani huku akilia kwa uchungu na hata alipokuwa ameketi katika benchi aliendelea kulia kwa huzuni.

Uchungu wake ulipotea katika dakika ya 112 za nyongeza mara baada ya mshambuliaji, Lautaro Martinez kufunga bao ambalo ndilo liliwapa ubingwa Argentina.

Wakati wachezaji wengine wakiwa wanakimbilia uwanjani kushangilia, Messi alisimama huku akiegemea zaidi mguu wa kushoto na kushangilia akiwa amesimama tu bila kukimbia.

Mguu wake uliojeruhiwa ulionekana kwa macho ya kawaida kuwa umevimba katika eneo la kifundo cha kulia. Hii iliashiria kujeruhiwa kwa eneo hilo.

Katika posti yake ya Instagram siku ya Jumatatu aliandika akiwatoa hofu mashabiki kuwa anaendelea vizuri na anamshukuru Mungu. Ingawa inaelezwa kuwa huenda akakosa mechi za klabu kwa wiki mbili.

Jumanne, wiki hii, Inter Miami ilieleza katika ukurasa wake wa Instagram kuwa mchezaji huyo alipata majeraha ya ligamenti za kifundo cha mguu wa kulia.

MAJERAHA YENYEWE

Katika majeraha yatokanayo na michezo ni kawaida kusikia kitabibu maneno ya ‘sprain na strain’. Ni maneno yanayoweza kukuchanganya na usifahamu wataalamu wa afya wanamaanisha nini.

Sprain injury ni majeraha ya kuvutika kupita kiasi au kuchanika kwa nyuzi za ligamenti ambazo katika ungio huunganisha mfupa mmoja na mwingine.

Wakati strain huwa ni majeraha yanayohusisha misuli na miishilio yake kitabibu tendoni. Aidha inawezekana ni nyuzi ndogondogo za misuli kujeruhiwa au kuvutika au kukatika kwa tendon.

Kiujumla ligamenti zote huwa na kazi za kuunganisha mifupa inayotengeneza ungio na kuituliza katika eneo lake usiende uelekeo hasi na hatimaye uingio kuwa imara na kufanya kazi zake kwa ufanisi. Kwa wanamichezo ni vigumu kukwepa kukumbana na majeraha ya kifundo cha miguu kwani ndilo eneo ambalo lina harakati nyingi wakati wa kucheza mpira wa miguu.

Wakati wa kutembea, kukimbia kuruka na kutua, kifundo huweza kutua vibaya na kujipinda hivyo kujeruhi tishu laini ikiwamo nyuzi ngumu ambazo hujivuta kupita kiasi na kusababisha kupata majeraha.

Majeraha ya kifundo cha mguu kwa wanasoka mara nyingi huwa ni kujeruhiwa kwa nyuzi za ligamenti.

Nyuzi hizi zinaweza kupata majeraha ya aina mbalimbali ikiwamo kufinywa, kujipinda, kunepa, kuvutika kuliko pitiliza, kukwanyuka, kuchubuka, kuchanika kiasi au kukatika na kuachana pande mbili. Vile vile majeraha haya yanaweza kusababisha kuleta nyufa katika mifupa inayounda ungio la kifundo. Mara zingine nyuzi za ligamenti zinaweza kuvutika sana na kubanwa katikati ya mifupa ya kifundo cha mguu.

Nyuzi za ligamenti zimejichimbia katika mifupa ya kifundo cha miguu ijulikanayo kama talus na tibia pale zinapopata majeraha huweza kusababisha maumivu, mlipuko wa kinga ya mwili na kuvimba.

Moja ya sababu inayochangia majeraha haya katika eneo la mbele la mguu wa chini la mguu ni kujeruhiwa kwa mfupa wa kifundo cha mguu au mfupa wa ugoko.

Uwepo wa mejaraha katika mifupa ikiwamo nyufa au kupasuka vipande vidogo vidogo huweza kuleta majeraha ya tishu laini zinazozunguka kuunda kifundo cha mguu.

Kwa upande wa Messi mpaka kufika jana haijatolewa taaarifa kama kuna mvunjiko wa vifupa vya eneo la kifundo. Itahitajika picha za skani na xray ili kuona hali ya mifupa.

Dalili na viashiria vya majeraha ya kifundo cha mguu ni pamoja na maumivu na kuuma pale panapominywa eneo hilo la kifundo, kupata maumivu pale unapojaribu kukukunja au kunyoonya kifundo.

Wakati wa utomasaji wa kifundo mfupa unaweza kugundua uwapo wa kichuguu katika mfupa wa mguu wa mguu au sehemu ya juu ya mfupa wa kifundo.

Messi alitoka nje ya uwanja akiwa anachechemea hali ambayo inaashiria kuwa majeraha hayo ni ya kati. Nyota huyo alitolewa uwanjani na kukaa benchi na haraka alipata tiba ya awali ya kukabiliana na maumivu na uvimbe kwa kuwekewa barafu katika eneo hilo.

Amelazimika kukatisha kwenda nchini kwao kusherehekea ubingwa huo na badala yake amebaki South Florida kuendelea na matibabu na tathimini zaidi chini ya klabu yake ya Inter Miami. Majeraha ya kifundo huwa hayatabiriki ni kawaida kuchelewa kupona. Imeelezwa Messi atakosa mechi za wiki hii za klabu ikiwamo ya Jumamosi dhidi ya Chikago.

Columnist: Mwanaspoti