Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maisha ya Pele ni darasa kwa wanamichezo wetu na jamii

Pele Pic Maisha ya Pele ni darasa kwa wanamichezo wetu na jamii

Sat, 7 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Siku moja nikiwa nafanya kazi na marehemu mama yangu kwenye shamba letu lililokuwa karibu na barabara. Ghafla alikatiza mwalimu wangu wa somo la kiingereza maarufu Mwalimu Jane ambaye pia sasa ni marehemu.

Mwalimu Jane alitumia muda mwingi kunisifia kwamba nilikuwa mwanafunzi wake bora katika somo la kiingereza.

Hata hivyo kabla ya kuondoka, Mwalimu Jane alimwambia mama yangu kunikanya dhidi ya marafiki zangu wanaoniingiza kwenye kucheza mpira ambao alidai utaathiri maendeleo yangu kitaaaluma.

Mwalimu Jane hakujua kitu kimoja, kwamba ilikuwa kinyume, kwani ni mimi ndiye nilikuwa nawashawishi wenzangu kucheza mpira.

Ni mimi nilikuwa nakwenda ofisini kwa mwalimu wa michezo kuomba mpira kabla hata ya muda wa somo kufika.

Pia Mwalimu Jane hakujua kama michezo ilikuwa kivutio na kichocheo kikubwa sana kwangu na sababu ya kufanya vizuri darasani. Hata nilipochaguliwa kwenda elimu ya sekondari mama yangu alinikanya kuhusu kutumia muda mwingi kwenye michezo na kwa kumtii sikucheza sana mpaka muda nakaribia kumaliza kidato cha nne ndio nikaanza kucheza na hapa hakukuwa na kizuizi kucheza mpaka nahitimisha masomo ya chuo kikuu.

Kisa changu na mwalimu Jane kinaweza kuwa kisa cha wengi.Shule na wazazi waliona michezo kama kikwazo kikubwa katika maendeleo ya kitaaluma kiasi kwamba michezo iliachwa kwa ajili ya wanafunzi wasiofanya vizuri.

Katika miaka ya karibuni nilipewa jukumu la kutafuta shule ambayo ingeshirikiana na shirikisho la mpira wa miguu katika kulea vipaji vya timu ya mpira wa miguu ya wavulana chini ya miaka 17.Nilimfuata mmiliki wa shule na kumweleza juu ya madhumuni yetu na faida ambazo angezipata ikiwa ni pamoja na kuboresha miundo mbinu ya michezo katika shule yake.

Hata hivyo, mmiliki huyo hakukubali na kwa nia njema kabisa alieleza wasiwasi wake ya kuwa kuwepo kwa wanamichezo shuleni kwake kungepunguza ufaulu wa shule yake.Alihisi uwepo wa wanamichezo utaua soko la shule yake.Mtazamo huu hauko katika mashule na wazazi pekee bali kwa jamii nzima ambayo kwa kiasi kikubwa haioni umuhimu mkubwa wa wanamichezo katika jamii tangu wakati wanacheza na hata baada ya kustaafu.

Maisha ya gwiji wa soka wa Brazil aliyeenda zake hivi karibuni Edson Arantes do Nascimento aliyejulikana kwa jina la utani Pele ni mfano wa namna mwanamichezo anaweza kutumika na kutumiwa katika jamii katika kujipatia kipato,kutangaza biashara,kuendesha kampeni za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuleta mabadiliko katika jamii.Pele aliyeanza kuchezea timu ya Taifa ya Brazil katika umri mdogo wa miaka 17 alistaafu kuchezea timu hiyo akiwa na miaka 36 huku akiwa ameshinda mataji matatu ya Kombe la Dunia.

Baada ya kustaafu,Pele alikuwa balozi wa dunia wa mpira wa miguu.Alijihusisha na shughuli nyingi na miradi mingi ya kutangaza na kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu na pia alipata mikataba ya kutangaza biashara. Hadi anaondoka duniani,ikiwa ni miaka 46 tangu kustaafu kutoka mchezo unaopendwa na wengi,Pele alikuwa bado ana mikataba na chapa nyingi tena kubwa za biashara na pia shughuli nyingi za hisani.

Pele,ambaye alipoteza figo yake moja tangu akiwa mchezaji,alikuwa bado ana shughuli za kufanya duniani na dunia ilikuwa bado inamhitaji hata angeishi miaka 100.Kuanzia chama cha mpira cha Brazil (CBF),vyama mbalimbali duniani na hata shirikisho la mpira duniani (FIFA) walikuwa bado wana mihadi na Pele.

Labda kisa kisichopendeza tunapoongelea shughuli za hayati Pele, hasa kwa wenyeji wa Afrika Mashariki inaweza kuonyesha namna tusivyowathamini wanamichezo wastaafu.Kisa hicho kilitokea Kenya Mwaka 1976 wakati Pele akiwa kwenye ziara ya kueneza mpira duniani.Pele alifanya ziara iliyokuwa imedhaminiwa na Kampuni ya Pepsi.Kama ilivyokuwa kwenye ziara zake nyingi, Pele alitegemewa kucheza mchezo wa maonyesho na kikosi cha timu ya taifa Harambee Stars au klabu moja kubwa nchini Kenya.

Bila kutegemewa,mwenyekiti wa chama cha mpira cha Kenya KFF Kenneth Matiba (sasa marehemu) alikataa kufanyika kwa mchezo wa maonyesho kwa madai ya kwamba KFF haikuhusishwa vya kutosha katika ziara hiyo.La kushangaza,Kenneth Matiba alikuwa pembeni mwa Pele wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari mara tu baada ya kuwasili nchini.Hata hivyo Pele binafsi alikwepa kuilaumu Kenya isipokuwa alikwepa kuiongelea ziara hii katika kitabu chake baadae.

Kisa cha Pele ziarani kenya kinahakisi mtazamo wetu kuhusu wanamichezo wa zamani.Utawala wa vyama vya michezo na jamii kwa ujumla huwapenda na kuwatukuza wanamichezo wanapokuwa bado wana nguvu mwilini nawakiwa bado wanashiriki michezo.Wengi baada ya kustaafu hujikuta katika hali ya kutengwa kiasi kwamba mchezaji aliyepata medali akilitumikia taifa anakosa tiketi ya kuingia uwanjani kushuhudia matukio mbalimbali ya michezo.

Wachezaji pia hawafanyi juhudi ya kuendelea kujihusisha na michezo waliyoitumikia au kutumia uzoefu wao kueneza michezo hiyo kwa jamii na matokeo yake wengi hufikia mwisho wa uhai wao wakiwa watu waliotengwa au kujitenga.

Ni hali hii huwakatisha tamaa wazazi kama mama yangu na hata walimu kama Mwalimu Jane kukata tamaa katika kuhamasisha vijana wao kushiriki michezo na kuichukulia michezo kwa uzito uleule wanaochukulia taaluma.Ukweli ni kwamba michezo ina nafasi kwa kila mmoja wetu bila kujali umri iwapo wanamichezo,vyama na wadau wote wakilitambua hilo.

Columnist: Mwanaspoti