Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Magufuli anavyodumisha tunu za taifa

E5aba22e29c4b8ad66acbb774f9bc1c7 Magufuli anavyodumisha tunu za taifa

Wed, 23 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“JAMBO la kwanza na muhimu tutakalolipa kipaumbele kikubwa kwenye miaka mitano ijayo ni kuendelea kulinda na kudumisha tunu za Taifa letu, yaani Amani, Umoja na Mshikamano, Uhuru wa Nchi yetu, Muungano na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Na katika hilo, naahidi kushirikiana kwa karibu sana na Rais mpya wa Zanzibar, Mheshimiwa Dk Hussein Mwinyi. Kamwe, hatutakuwa na mzaha na yeyote mwenye kutaka kuhatarisha amani ya nchi yetu; mwenye nia ya kuvuruga umoja na mshikamano wetu; na pia mwenye kutaka kutishia Uhuru wetu, Muungano pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar”.

Maneno haya aliyatoa Rais John Magufuli wakati wa uzinduzi wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ijumaa ya tarehe 13, Novemba 2020.

Dhana ya kudumisha tunu za taifa letu ni jambo lisilohepukika kwa kila mtanzania aliye na mapenzi mema na nchi yake japo kwa nyakati tofauti baadhi ya wanasiasa uchwara nchini mwetu hasa kutoka kwa baadhi wa vyama upinzani wamekuwa wakibeza jitihada zinazofanyika kudumisha tunu hizi.

Kwa nyakati tofauti tumeona jinsi walivyokuwa wanampinga Rais Magufuli hasa wakati wa kutumbua baadhi ya viongozi wa umma walioshindwa kutimiza majukumu yao katika uwajibikaji.

Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli, alisisitiza pasi na shaka kwamba ataendelea kutumbua watendaji ambao hawatatimiza majukumu yao ipasavyo. Ili kukuza uzalendo na hususani kwa vijana waliozaliwa baada ya uhuru Rais alielezea umuhimu wa kuanza kufundishwa kwa somo la historia ya Tanzania.

Ni wazi kwamba somo hili litasaidia kurejesha uzalendo na kudumisha umoja wetu.

Kwa lengo la kuboresha makala haya tujikumbushe tunu zetu kama taifa: Utu; Uzalendo; Uadilifu; Umoja; Uwazi; Uwajibikaji; na Tuendeee kukuza na Kuinua Lugha yetu ya Taifa.

Kwa nyakati tofauti Rais Magufuli amenukuliwa akisema vijana ndio chachu ya kuendeleza miiko na maadili ya nchi yetu. Vijana ndio chachu ya maendeleo na hivyo sisi vijana tunatakiwa kujitambua na kutambua nafasi yetu katika kuinua nchi yetu kila mmoja katika nafasi aliyonayo.

Sisi ndio tutaotengeneza Tanzania tunayoitaka; Juhudi ya kila mmoja inahitajika katika kuhakikisha hili linafanikiwa.

Utu ni nguzo kuu. Yatupasa tutangulize mbele utu katika matendo yetu yote, tuwe waungwana; wapenda haki; wenye kauli njema; wenye hekima.

Haya aliyathibitisha katika hotuba yake wakati wa kuapisha baraza jipya la mawaziri alipowataka wateule wakawatumikie watanzania kwa moyo wote huku wakitanguliza utu katika utendaji kazi wao na kuacha kula vishoka kwenye magari yao.

Uzalendo ni nguzo muhimu kwani tukitambua kuwa juhudi zetu kila mmoja zikijumuishwa tutaipata Tanzania tunayoihitaji, kila mtu atatekeleza wajibu wake. Tuipende na tuitangaze nchi yetu ya Tanzania, kila mmoja wetu aibebe nchi yetu moyoni na katika matendo yake.

Uadilifu wetu ndio utakaoonesha mafanikio. Wapo baadhi ya wanasiasa wanaoisema vibaya nchi yetu kisa tu wamekosa madaraka! Huku ni kutokujitambua na kujidhalilisha kabla ya nchi yetu.

Ingefaa sana wanasiasa hawa badala ya kutangatanga kila kona usiku kucha wakiomba hifadhi nje ya nchi wakati kwenye nchi yao amani ipo tele tena hakuna ‘lock down ya covid-19, kutulia na kuungana na chama tawala katika kusaka maendeleo mapana ya nchi yetu’.

Katika nyanja zote umoja kwangu nawaza kusema ndio tunu ya muhimu zaidi hasa kwetu vijana kwani tunatambua usemi usemao; “Umoja Ni Nguvu; Utengano ni Udhaifu.”

Umoja wetu ndio utakaotupa yale matunda na mafanikio tunayotamani kuyaona. Tuache kufuata mikumbo potofu inayotolewa na baadhi ya wanasiasa wenye nia mbaya na nchi yetu. Badala yake tuungane katika kushirikiana na watendaji kuleta maendeleo ya nchi yetu.

Mara nyingi Rais Magufuli, amekuwa akisisitiza dhana ya kushirikiana kila mmoja kwa nafasi yake katika kuwatumikia watanzania.

Kimsingi, kuna baadhi ya ofisi wafanyakazi kila mmoja alikuwa anafanya kazi kivyake jambo ambalo kwa sasa linapotea kabisa. Wote wanafanya kazi kwa ushirikiano kwa maslahi mapana ya kitaifa. Hii inatimiza ahadi ya saba ya mwanachama wa TANU (sasa ni CCM) inayosema, ‘nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu’.

Uwazi ni muhimu; dhana hii kwa njia tofauti kila mara alipo pata nafasi Ndugu Magufuli amezidi kuisisitiza. Mara nyingi tumeshuhudia akiwaumbua baadhi ya watendaji walioshiriki kuliibia taifa letu.

Amekuwa akiwaeleza bila kuficha kwamba dhana ya utumishi wema ni nzuri kwa maslahi mapana ya taifa letu. Bila kuogopa mtu amekuwa akiweka bayana utajiri wa nchi tulio nao huku akibainisha wazi kwa watanzania jinsi tulivyokuwa tukiibiwa.

Dhana yake ya uwazi wa mapato na matumizi kwa watanzania imemuongezea imani kubwa dhidi ya watanzania wote huku akisisitiza watendaji waige mfano wake. Japo inawezekana kwa wakati mwingine watendaji hao hao ndiyo wamekuwa wakimkwamisha.

Uwajibikaji ni nguzo ya muhimu kwetu vijana kwa mantiki ya kuhakikisha tunawajibika kila mmoja katika nafasi yake. Kila mtu afanye Kazi kadri ya nafasi aliyonayo popote alipo atambue kuwa yeye ni chachu ya maendeleo na mafanikio.

Tusikae tukinyooshea mtu na kusema hii ni kazi yake bali tujitathmini na tuangalie nafasi zetu sisi ni zipi; na tujitathmini kipi tunachoweza kufanya kuhakikisha tunatengeneza mazingira bora zaidi ya nchi yetu kiujumla.

Iwapo kila mmoja atatimiza majukumu yake ipasavyo, nchi yetu haitalia tena wizi wa maliasili zetu, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mambo kadha wa kadha. Haya yanadhihirishwa katika azimio la Arusha sura ya kwanza kwenye vipengele vya Imani ya tanu inaposema:

“Kwamba ni wajibu wa serikali, ambayo ni watu wenyewe, kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi ya Taifa ili kuhakikisha usitawi wa raia wote na kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine na kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani na siasa ya watu wote kuwa sawa’.

Uadilifu; dhana hii ni nyeti sana mabayo inabeba mstakabali mzima wa maono ya nchi ya usoni. Katika hotuba ya kuapisha mawaziri wapya Rais Magufuli alisisitiza kuwa jambo muhimu ni kusimamia kazi kwa weledi.

Nikimnukuu, Rais anasema: "Sitaki mitindo ile ya kisasa ya kupiga selfie kwa kila unachofanya, unapaswa kufanya kazi na ajenda nyingine ni za siri.

''Teknolojia mpya ni nzuri lakini ni muhimu kwa kuzingatia maadili ya kazi zenu. Ndani ya serikali ni vyema kufanya kazi kwa uadilifu, kuna makundi mengi katika mitandao ya kijamii. Ndani ya serikali ni vyema kuzingatia siri na maadilli tulio nayo. Idara zote ni muhimu katika taifa letu’.

Kuna wakati najiuliza, iwapo kama nchi tusingempata Rais Magufuli kipindi hiki nchi yetu tungekuwa wapi? Utunzaji wa tunu za taifa ungekuwaje? Vilio vya watanzania juu ya utofauti wa walionancho na wasionacho vingekuwaje?

Hivi ni sahihi kuchukia kiongozi ambaye anaishi maono ya Hayati Baba wa Taifa? Kwa uelewa wangu mdogo, kiongozi kama huyu anastahili kuungwa mkono wa kila namna kwa maslahi mapana ya taifa letu.

Kama watanzania, huu siyo wakati wa kuzembea badala yake ni wakati wa kuungana naye katika kuliletea taifa maendeleo makubwa sana tunayohitaji kama watanzania. Mungu azidi kumbariki na taifa letu.

Mwandisi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni +255 712 246 001; [email protected]

Columnist: habarileo.co.tz