Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maendeleo ya klabu yaendeleze taifa

Clement Francis Mzize.jpeg Clement Mzize

Sat, 25 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika moja ya safari zangu kwenye utumishi wa mpira wa miguu niliwahi kufika katika taifa la China. Taifa hili halisikiki katika maendeleo ya mpira wa miguu kama inavyosikika Argentina, Brazil, Ujerumani au hata Morocco, Misri, Nigeria na Senegal.Pamoja na kutosikika kwake, kuna jambo moja au mawili nilijifunza kutoka kwa Wachina.

China ilifungua milango kwa ajili ya mpira wa kulipwa (professional) ili uweze kuwaingizia watu kipato na kuruhusu wawekezaji binafsi kutia pesa zao katika michezo kama inavyofanyika kwenye mataifa yaliyoendelea kiuchumi na kimichezo.

Lengo jingine katika kuruhusu mpira wa kulipwa ni kutengeneza hamasa kwa wazawa ili wajifunze kutoka kwa nyota wanaowahusudu (role models). Kwa hiyo pale unaposikia wachezaji kama Cedric Bakambu (Beijing Guoan), Paulinho (Guangzhou Evergrande), Oscar (Shanghai SIPG) na wageni wengine wako China wana jukumu la ziada lisilo kwenye mikataba yao minono; jukumu la kuchochea utamaduni wa mpira katika taifa la China.

China inawekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya mpira wa miguu, elimu na soka la vijana na wanawake. China inatengeneza mazingira ya kutotegemea sana wageni katika soka lake la kulipwa katika miaka ijayo. China inaandaa timu za taifa za miaka ijayo, China inataka kuuza wachezaji nje kama wanavyofanya majirani zake Korea na Japan. Hilo linawezekana hasa kwa taifa ambalo likija na jambo lake huhakikisha linafanyika. Siku hizi kwenye viwanja vikubwa vya soka wanakwenda kina mama wengi na watoto kuangalia mpira. Familia itakapopenda mpira wa miguu basi taifa litaupokea utamaduni huo wenye fedha lukuki.

Katika ligi ya kulipwa ya China (Super League), ni wachezaji watatu tu wa kigeni wanaoruhusiwa kucheza kwa wakati mmoja. Pia, timu inatakiwa iwe na wachezaji wawili wa Kichina wenye umri wa chini ya miaka 23 na katika hao wawili ni lazima mmoja aanze katika kila mchezo wa ligi.

China bado hairuhusu magolikipa wa kigeni. Ni sharti la chama cha mpira cha China (CFA) kwa timu zinazoleta wachezaji wa kigeni kuchangia sehemu ya fedha waliyotumia kwa ajili ya mfuko wa maendeleo ya mpira wa miguu.

Utaratibu mzima unaweza kuonekana kama unazibana klabu za China lakini ukweli ni kwamba China isingependa kuona klabu zake zinatoa pesa nyingi huko mbele kuendelea kushindana sokoni na klabu kama Chelsea, Barcelona na myingine za Ulaya.

Nilichokiona wakati ule na kinachoendelea sasa katika mpira wa China kiliamshwa na nilichoshuhudia katika wikendi ya mpira wa Afrika katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Kwa kuangalia timu zetu za Simba na Yanga na kuangalia timu nyingine zinazoshiriki mashindano hayo, napata sababu ya kuogopa kwamba uwepo wa wachezaji wa kigeni hautakuwa na tija kama hazifanyiki juhudi na taratibu za kuendeleza mpira wa vijana na kuwapa nafasi vijana kucheza katika klabu za Ligi Kuu kwa faida ya timu za taifa na taifa kwa ujumla.

Ni jambo jema kwamba klabu vza Simba na Yanga zimewekeza kiasi kikubwa cha fedha kiasi cha kuwapa Watanzania furaha ya mpira wa Afrika lakini nadhani kuna umuhimu wa kuangalia nafasi ya wazawa hasa vijana katika klabu za Ligi Kuu.

Kuna umuhimu wa utaratibu wa leseni za klabu unaozitaka klabu kuwa na timu za vijana kusimamiwa kama ilivyo kwenye makaratasi. Vijana wanaotoka kwenye akademi za klabu na timu za vijana za taifa wapewe nafasi kadhaa za upendeleo kwenye kanuni za Ligi Kuu au Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) ili waweze kufika mbali na pia kuwa na nafasi ya kuliwakilisha vema taifa.

Ukiangalia timu kama Raja Cassablanca ya Morocco, Al Ahly ya Misri na hata Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini, wana wageni, ndiyo, lakini bado vijana wengi wazawa wana nafasi katika klabu zao.

Ni vizuri tutakaposhangilia kwa Mkapa hatoki mtu, isiwe tu kwa ajili ya klabu bali pia kwa Taifa Stars. Ni juu ya watunga sera za michezo na shirikisho la mpira wa miguu kutafuta ulali (balance) kati ya kuendeleza klabu na ligi ya kulipwa bila kuondoa jicho kwenye mafanikio endelevu ya mchezo wa mpira wa miguu ambayo hayawezi kupatikana kamwe bila kuimarisha mifumo ya mpira wa vijana.

Columnist: Mwanaspoti