Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Maarifa hupatikana kupitia lugha mama’

88cfb07b95d6f20c5c106315b562608f.png ‘Maarifa hupatikana kupitia lugha mama’

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

ELIMU ina maana pana. Moja ya maana ya elimu ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi.

Katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa makusudi na jamii kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine. Kukua na kuongezeka kwa teknolojia, kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi duniani hata namna ya kupata elimu kumebadilika.

Unaweza kusoma kwa njia ya mtandao bila kulazimika kwenda chuoni kila siku ilimradi uwe na kompyuta yenye intaneti au simu ya kisasa. Ingawa baadhi ya watu wanalichukulia kuwa gumu ukilinganisha na kuhudhuria darasani kila siku, hata hivyo wanafunzi wanaosoma kwa njia ya mtandao wanaonesha kufanya vizuri zaidi kwenye masomo na matokeo yao ya mitihani.

Teknolojia inatumiwa si tu katika wajibu wa kutawala katika elimu bali pia katika kuwaelekeza wanafunzi. Matumizi ya teknolojia kama vile virusha maandishi na ubao mweupe hutumiwa kunasa akili za wanafunzi darasani. Teknolojia vilevile hutumiwa kuwatahini wanafunzi.

Mfano mzuri ni mfumo wa kuvutia hadhira, ambao huruhusu majibu ya mitihani moja kwa moja pamoja na majadiliano darasani. Mwalimu Daudi Makoba limekuwa si jina geni kwa watumiaji wa mtandao duniani, ni mwalimu ambaye darasa lake liko wazi mtandaoni saa zote.

Mwalimu huyo masomo yake yamenufaisha wanafunzi wengi na watu mbalimbali duniani masomo yake hupatikana bila malipo mtandaoni. Katika mahojiano, Mwalimu Mkoba yeye anaona umefikia wakati wa kutafuta mazingira ambayo wanafunzi wataweza kutumia simumtelezo (simu janja) kutokana na kuwa kufanya kazi sawa na kompyuta. Ni kwa msingi huo anaanzisha mjadala akiona kama kuwanyima wanafunzi matumizi ya simu ni kuwakosesha maarifa zaidi.

“Mimi najitahidi kuwapatia ziada baada ya masomo ya darasani lakini nilichogundua ni ukosefu wa vitabu vya kiada na ziada, ni tatizo linalokabili taifa,” anasema.

Anasema elimu ya sasa inahitaji mwanafunzi apate maarifa zaidi na njia rahisi ni kupitia mitandao ambako kuna mengi ambayo wanaweza kujifunza. Ndipo anasema kwamba iwapo matumizi ya simu yataruhusiwa mashuleni kwa kutafuta njia za kudhibiti matumizi mabaya, yatamsaidia sana mwanafunzi hasa shule za vijijini.

Anasema serikali ikarabati na kuboresha shule pia kujenga maktaba zinazojitosheleza sambamba na elimu ya matumizi bora ya mitandao kwa kushirikisha vyombo vya habari. Anasema kuna baadhi ya shule ambazo zinawanyima wanafunzi vitabu kwa kuhofia kwamba vitabu hivyo vitachanika.

Katika hali hiyo anasema suluhisho siyo kuwanyima bali kuwafundisha wanafunzi utunzaji wa vitabu na kwamba hilo litawezekana iwapo wazazi watatambua wajibu wao kielimu na kutunza vitabu kwa faida ya sasa na kizazi kijacho.

“Napigiwa simu kutoka nchi mbali mbali ili kutoa ufafanuzi wa masuala yanayohusiana na vitabu. Napigiwa simu kutoka Marekani, India na nchi nyingine,” anasema mwalimu huyo.

Makoba ambaye alihitimu taaluma ya ualimu kwa masomo ya Kiswahili na Historia amekuwa akifundisha wengi kwa njia mtandao masuala ya insha, hotuba na uhakiki kwa njia inayomrahisishia mwanafunzi kupata uelewa.

Hutoa masomo yake kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza. Anapoulizwa kuhusu mjadala wa lugha ipi kati ya Kiswahili na Kiingereza itakayomwezesha mwanafunzi wa Tanzania kupata uelewa zaidi katika masomo yake, anasema masomo yanapaswa kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili.

Anafafanua kwamba mwanafunzi anapofundishwa kwa lugha anayoifahamu vyema kama Kiswahili kilivyo kwa Watanzania wengi anapata maarifa haraka na vyema zaidi kuliko lugha ya kigeni.

Anasema wakati mwingine wanafunzi wanashindwa kuelewa kitu siyo kwa sababu nyingine isipokuwa lugha ya Kiingereza na kwamba hata kwenye mitihani wengine huwa na maarifa sahihi lakini lugha ya kigeni ikawafanya washindwe kueleza sawasawa wanachokijua na mwisho wa siku kufeli mitihani.

Anafafanua kwamba tatizo la lugha linaanzia kwenye mazingira ya shule yasiyomjenga vyema mwanafunzi kuelewa lugha ya Kiingereza na hata walimu ambao wengi pia hawakijui vyema Kiingereza.

Anasema mbali na kikwazo cha lugha, mengine yanayosababisha wanafunzi kutofaulu vyema mitihani yao ni kukosa vitabu sahihi; wao wenyewe kushindwa kujisomea na kukosa walimu wenye moyo wa kufundisha.

Anapoulizwa kutumia uzoefu wake kueleza kile kinachoelezwa mara kwa mara kwamba kiwango cha ufaulu nchini kinachopanda kipande endapo kinaendana na maarifa, mwalimu huyo anasema kama wanafunzi wengi wanafaulu maana yake maarifa yaliyolengwa yanafikiwa.

Hata hivyo, anasisitiza kwamba teknolojia ya mawasiliano nchini inaweza kukuza maarifa kwa kuwarahisishia wanafunzi kuweza kusoma kwa njia rahisi zaidi tena kwa gharama nafuu na kwamba inasaidia wanafunzi kujipatia maarifa muda wowote na mahali popote.

Mwalimu Makoba anatoa rai kwa serikali kuongeza bajeti ya elimu jambo hili litasaidia kupunguza changamoto za ukosefu wa vitabu na vifaa vingine vya kujifunzia. Elimu ndiyo msingi wa mambo yote.

Hivyo serikali ijitahidi kuongeza walimu angalau kuwe na uwiano wa 26:1, yaani wanafunzi ishirini na sita kwa mwalimu mmoja. Anasema kwa uwiano huo mwalimu atakuwa na uwezo mzuri wa kusahihisha kazi za wanafunzi kwa uangalifu na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata maarifa yanayotakiwa.

Columnist: habarileo.co.tz