Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Maalim Seif amekamilisha amani, maridhiano’

D3f738d03e951ceef8b93787e4e09c0d ‘Maalim Seif amekamilisha amani, maridhiano’

Sat, 20 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

RAIS John Magufuli amemtaja Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad kuwa alikuwa kiongozi wa tofauti, ambaye ameondoka akiwa amemaliza salama dhamira yake ya kujenga umoja na amani kwa Watanzania.

Magufuli alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi. Akiendelea kutoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Mwinyi kutokana na kifo cha Maalim Seif aliyezikwa juzi Pemba, Magufuli alikumbushia mazungumzo aliyofanya naye akiwa Chato mkoani Geita na kusema yalikuwa ni ya raha na alikuwa akihubiri umoja wa Wazanzibari na Watanzania.

“Alikuwa ni mtu mcheshi na siku zote katika ziara yake alikuwa akihubiri umoja wa Wazanzibari na Watanzania kitu ambacho amemaliza nacho. Tumshukuru Mungu kwamba Maalim Seif amemaliza salama na dhamira yake ya kujenga umoja na amani” alisema.

Akielezea namna Maalim Seif alivyokuwa kiongozi tofauti, Magufuli alisema mwaka 2015 alipopata urais na baada ya Uchaguzi wa Marudio Zanzibar, Maalim Seif alimwandikia barua akimuomba kumuona.

“Nilisita kidogo. Kwamba kwa nini anataka kuja kuniona na wakati kwenye uchaguzi hakushiriki. Aliandika tena barua ya pili na baadaye ya tatu. Kila nilipokuwa nikijaribu kupata ushauri kutoka Zanzibar nilikuwa naambiwa subiri kwanza, muache kwanza,” alisema.

Alisema “Siku moja nikaamua ngoja nimuone Seif. Alipokuja Ikulu Dar es Salaam, nilipoanza kuzungumza naye nilimuona ni mtu tofauti sana na picha iliyojengeka. Mazungumzo yalikuwa mazuri. Akaeleza kuwa hakushiriki uchaguzi wa pili.”

Rais Magufuli alisema Hamad alimhakikishia kuwa Zanzibar itakuwa salama na hatahamasisha fujo yoyote na kwamba miaka yote mitano, aliyechaguliwa ataendelea vizuri kutawala.

“Kauli hiyo niliiona baada ya miaka mitano. Alieleza kuwa anapenda amani, kauli niliyoithibitisha kwa vitendo,”alisema.

Magufuli alisema ulipotokea uchaguzi mwingine, Maalim Seif alishiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kwamba mara ya mwisho alipofika Chato akiwa ameongozana na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, mazungumzo yao yalikuwa ya raha.

“Akanipa historia nzuri akiwa CCM wakati huo akiwa TANU,” alisema.

Columnist: habarileo.co.tz