Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maajabu ya Soka: Awali hakukuwa na Sub ujue

Substitution Awali hakukuwa na Sub ujue

Sat, 28 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mchezo wa kandanda umepitia mageuzi mengi ya sheria, kanuni, mavazi, mfumo wa kucheza kusherehekea na kadhalika.

Katika miaka ya nyuma ilikuwa dhambi kwa mlinzi kuvuka mstari wa katikati ya uwanja na aliyefanya hivyo alionekana anahatarisha timu yake kufungwa.

Siku hizi hata makipa huvuka mstari ili kuongeza mashambulizi timu inapokuwa na kiu ya kupata bao.

Nilipokuwa mdogo mchezaji aliyeumia alitibiwa na kurudi uwanjani, baadhi ya wakati damu zikimtoka.

Wakati ule ambapo muda wa mchezo ulikuwa dakika 60 na siyo 90 kama sasa kitendo cha kubadilisha mchezaji kilikuwa zaidi ni cha makubaliano na sio kanuni ya mchezo.

Timu zilitakiwa zikubaliane kabla ya mchezo kuanza na mara nyingi ilikuwa kubadilisha mchezaji mmoja tu.

Kama ulikuwa mchezo wa mashindano, iwe ligi au ya mtoano, suala la kubadilisha mchezaji lilitakiwa lielezwe katika kanuni kabla ya mashindano kuanza.

Hata hivyo, mtindo wa kubadilisha wachezaji ulitumika katika baadhi ya mashindano ya shule za Uingereza tokea katika miaka ya 1860.

Hata hivyo, mchezaji alibadilishwa kama aliumia au alifanya ujanja wa kujidai hawezi kuendelea na mchezo.

Siku hizi mchezaji anaweza kubadilishwa kama amechoka au hajisikii vizuri au kocha akiona kuingiza wachezaji wa akiba kutaimarisha ulinzi au mashambulizi ya timu.

Katika miaka ya nyuma ilikuwa kawaida kuona wachezaji wawili au watatu wanachechemea na wanaendelea kuwepo uwanjani kwa vile wangelitoka timu yao ingelielemewa kwa vile nafasi zao zilikuwa haziwezi kujazwa.

Kwa hivyo bora mchezaji aliyeumia abaki aendelee kucheza kama ilivyokuwa zamani kwa nahodha alivyolazimika kufa na tai shingoni wakati meli ikizama baada ya kushindwa kuhimili dhoruba kali.

Mara ya kwanza mtindo wa kubadilisha mchezaji katika mashindano ya kiataifa ulianza tarehe 15 Aprili, 1889. Hii ilikuwa Wales ilipopambana na Scotland.

Hili lilifanyika kwa maelewano ya hizo timu na sio kwa mujibu wa kanuni za mchezo. Siku ile kipa wa Wales, Sam Gillam alikuwa hajafika uwanjani mchezo ulipotaka kuanza na pande hizo mbili zilikubaliana atapofika Wales ingeweza kumtoa golikipana Gillam kuingia badala yake.

Mchezaji mmoja wa akiba alikaa golini na Gillam alifika uwanjani akiwa anahema mchezo ukiwa unakaribia wakati wa mapumziko.

Gillam aliingia uwanjani kuchukua nafasi yake, kitendo ambacho kiliwashangaza mashabiki wengi wa na kukiona kama ni cha ajabu.

Mjadala mrefu ulikuja kufanyika juu ya suala hili huku baadhi ya watu wakisema mtindo wa kubadilisha wachezaji unapunguza vionjo vya mchezo.

Mtindo huu ulianza rasmi kanuni ya Sherikisho la Kimataifa la Kandanda (FIFA) katika micheo ya kutafuta tiketi ya Kombe la Dunia kwa fainali za 1954.

Mchezaji wa kwanza kuingia uwanajani kuchukua nafasi ya mwenzake aliyetoka alikuwa Horst Eckel wa Ujerumani pale nchi hiyo ilipopambana na Saarland tarehe 11 Oktoba, 1953. FIFA ilichukua hatua hiyo baada ya kuona wachezaji wengi walilazimika kubaki uwanjani wakichemea baada ya kuumia katika fainal za Kombe la Dunia za 1950.

Baadhi ya wachezaji walijiumiza zaidi kwa kujilazimisha kucheza kwa sababu kama wangelitoka timu zao zingelazimika kucheza na wahezaji wachache. FIFA ilisema lengo la kuchukua hatua hiyo ni kupunguza maumivu katika soka ili mchezo uwe zaidi wa burdani na sio mateso.

Ligi Kuu ya Uingerea ilianza kutumia rasmi sheria ya kubadilisha wachezaji katika msimu wa 1965-66. Mchezaji wa kwanza wa akiba kuingia uwanjani katika mashindano haya alikuwa Keith Peacock wa Charlton Athletic baada ya golikipa Mike Rose kuumia dakika 11tu baada ya kuanza pambano na Bolton Wanderers mnamo tarehe 21 Agosti, 1965.

Siku chache baaada ya kitendo hicho nchi za Afrika ya Mashariki ziliokuwa zikitawaliwa na Uingereza, ijapokuwa zilikuwa huru, lakini bado zikiwa zinaiga mambo wanayofanya Waingereza ziliamua kuitumia sheria hii.

Sheria hii ilipoanza kutumika kwetu huku watu wengi wakiwa hawana habari nayo walipiga kelele na kuuliza kama tiketi moja ya basi inaweza kutumiwa na wasafiri wawili.

Wakati ule niliandika makala ndefu kuielezea sheria hii na mmoja wa wasomaji akasema bado tulikuwa tunatawaliwa na Uingereza. Mwengine aliileza sheria ile kama “ ukoloni mamboleo”.

Shabiki mmoja ndiyo alitoa kali zaidi aliposema:” Ni vyema kwa timu kuruhusiwa hata kubadili wachezaji wote 11 kama kocha anaona hawachezi vizuri”. Jamaa huyualishauuri hata mtu akiwa hakupendezewa na mchezo angeliruhusiwa kutoka nje na kumpa mtu mwengine tiketi yake aingie uwanjani kuangalia mchezo.

Hoja yake ni kama iliruhusiwa kubadili wachezaji kwanini isiruhusiwe pia kubadili watazamaji. Hapo mwanzo sheria hii iliruhusu kila timu kubadili mchezaji mmoja tu.

Scotland ambayo kwanza ilikataa kuitumia sheria hii ilibadili uamuzi wake na kuitumia mwaka 1966. Sheria ilipoanza kukubalika rasmi kimataifa ndio sheria nyingi zinazohsu wachezaji wa akiba zikatungwa, kama vile namna ya mchezaji atakavyotoka na mwengine kuingia kwa kupitia katikati ya uwanja.

Sheria hizo mpya pia zilijumisha muamuzi kumpa kadi ya njano au nyekundu mchezaji aliyekuwepo kwenye bao la akiba, kocha au mchuaji wa misuli kama ameona kauli au vitendo vyake sio vizuri.

Hata hivyo sheria ya ubadilishaji mchezaji haimpi mamlaka muamuzi kulazimisha mchezaji abadilishwe na timu yake na inapotokea mchezaji kukataa kutii amri ya kocha wake ya kutoka nje muamuzi ataendelea na kuchezesha.

Labda tujiulize : Kama nafasi ya mchezaji inaweza kuchukuliwa na mchezaji mwengine kwa nini hivyo hivyo isiwe kwa watazamaji? Wakati ndio utakaotoa uamuzi wa suala hili, lakini kwa hali ilivyo sasa tusubiri.

Columnist: Mwanaspoti