Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maajabu Simba, Yanga njia moja ya vigogo Afrika

Simba Pic Maajabu Afrika Maajabu Simba, Yanga njia moja ya vigogo Afrika

Mon, 6 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kwa sasa ipo hatua ya makundi na tayari zimehapigwa mechi za raundi tatu tatu hadi sasa na mapema wiki ijayo itaingia kwenye ngwe ya nne itakayotoa taswira ya timu zipi zitasonga mbele kwenda robo fainali na zipi zitakwama.

Msimu huu imekuwa bahati nyingine kwa Tanzania kwa kuwakilishwa na timu mbili kwenye hatua hiyo, yaani Simba na Yanga ambazoz zitakuwa na kibarua kigumu nyumbani watakapozikaribisha Vipers ya Uganda na Real Bamako ya Mali kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba itaanza kuitupa karata ya mechi za rundi ya nne ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa kwa kuvaana na Vipers siku ya Jumanne ya Machi 7, kabla ya siku inayofuata yaani Jumatano Yanga nao kuwa wenyeji wa Real Bamako katika pambano la Kundi D la Kombe la Shirikisho.

Hizo ni mechi muhimu kwa timu hizo kwani zinahitajika kupata ushindi ambao utaifanya kila moja kuweka hai matumaini ya kucheza robo fainali ya mashindano hayo msimu huu.

Simba inayoshika nafasi ya tatu kundini baada ya kushinda mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Vipers inahitaji ushindi zaidi, huku ikiiombea mabaya Horoya ya Guinea ambayo itakuwa ugenini kuvaana na vinawa kundi hilo, Raja Casablanca ya Morocco ili ijiweke katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali vinginevyo itakuwa na nfasi finyu ya kusogea mbele.

Yanga inayoshika nafasi ya pili katika kundi ililopo ikiwa na pointi nne, nayo inahitaji ushindi wa nyumbani dhidi ya Real Bamako na kisha kuombea TP Mazembe ifanye vibaya dhidi ya Monastir ya Tunisia ili ikaribie kuingiza mguu mmoja katika hatua ya robo fainali.

Katika mechi yao iliyopita iliyopigwa wiki iliyopita, timu hizo zilitoshana nguvu kwa kutoka sare ya 1-1, huku Monastir ikiitambia TP Mazembe nchini DR Congo kwa kuinyuka mabao 2-0.

Kwa tathmini ya mechi za duru la kwanza la hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika, ni timu sita tu ambazo zina nafasi kubwa ya kuingia robo fainali na kwa sasa kila moja inahitaji kupata ushindi katika mechi yake ijayo tu ili iweze kujihakikishia rasmi tiketi ya kucheza hatua inayofuata pasipo kutegemea matokeo ya timu nyingine.

Timu hizo ni Mamelodi Sundowns, Esperance na Raja Casablanca ambazo zipo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na katika Kombe la Shirikisho Afrika kuna timu za Monastir, AS Far na USM Alger.

Hata hivyo wakati vigogo hivyo sita vikijiweka karibu na robo fainali, zipo timu nyingine kubwa na tishio Afrika ambazo kwa sasa zimejikuta katika kundi moja la Simba na Yanga la kutokuwa na uhakika wa kufuzu hatua inayofuata na zinahitajika kupata ushindi katika mechi zao za raundi inayofuata huku zikiombea mabaya zingine ili ziweke hai matumaini yao ya kusonga mbele.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya vigogo vya soka Afrika ambavyo kwa sasa vimejikuta katika mtego wa Simba na Yanga wa kuhakikisha vinashinda mechi zao zijazo lakini pia kuombea nuksi timu nyingine zifanye vibaya ili zenyewe zijiweke katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

AL AHLY

Mabingwa wa kihistoria wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa wamelichukua mara 10, Al Ahly hapana shaka wapo kwenye presha kubwa kwa sasa kutokana na matokeo yasiyoridhisha katika mechi mbili za kwanza ilizocheza kwenye kundi lake ambazo ni dhidi ya Al Hilal, waliyopoteza ugenini kwa bao 1-0 na nyingine ni ile waliyotoka sare ya mabao 2-2 nyumbani mbele ya Mamelodi Sundowns.

Leo watakuwa nyumbani kukamilisha raundi tatu za mzunguko wa kwanza wakati watakapoikaribisha Coton Sport ambapo wakipata ushindi watafikisha pointi nne.

Hata hivyo, pointi hizo nne bado zitakuwa hazijawaweka salama Ahly na ili wanusurike, watapaswa kupata uhsindi katika mechi itakayofuata baada ya leo ambayo ni dhidi ya Mamelodi Sundowns ugenini huku wakiombea Al Hilal ipoteze nyumbani dhidi ya Coton Sport.

Kama Hilal itaifunga Coton Sport na Ahly ikafungwa na Mamelodi, inamaanisha kuwa ushindi wa mechi moja tu kati ya mbili zao za mwisho utamaanisha kuwa Al Ahly wanaondolewa mashindanoni.

WYDAD CASABLANCA

Jana Raja Casablanca walikuwa na mchezo wa kukamilisha raundi ya tatu dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo ambao kama wameshinda watakuwa wamefikisha pointi sita.

Hata hivyo pointi hizo sita hazitowafanya Wydad kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kutokana na msimamo wa kundi lake ulivyo na hapana hata raundi ya tatu na ya nne isitoe majibu kamili ya timu ipi inaenda robo fainali.

ZAMALEK

Mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wamekusanya pointi moja tu katika mechi tatu za mwanzo za hatua ya makundi ya mashindano hayo na wanshika mkia katika kundi D linaloongozwa na Esperance.

Ikiwa Zamalek itapoteza dhidi ya Esperance, keshokutwa Jumanne na Al Merrikh ikapata ushindi mbele ya CR Belouizdad, miamba hiyo ya soka Misri itaaga rasmi huku ikiwa imebakiza mechi mbili mkononi.

ASEC MIMOSAS

Timu ya zamani ya Aziz Ki Stephane imekusanya pointi nne tu katika mechi tatu za kundi lake A la Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na pointi nne.

Miamba hiyo ya Ivory Coast kama ilivyo kwa Yanga na Simba, hadi sasa haina uhakika wa kutinga robo fainali na inalazimika kushinda mechi zake za raundi mbili zijazo kisha kuziombea nuksi Diables Noirs na DC Motema Pembe ili isonge mbele.

PYRAMIDS FC

Miamba ya soka Misri, Pyramids FC, inashika nafasi ya pili kwenye kundi C la Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na pointi tano huku vinara wakiwa ni AS Far.

Tofauti na ilivyozoeleka hapo nyuma kwa Pyramids kujihakikishia kutinga robo fainali baada ya mechi ya raundi ya nne tu, msimu huu mambo yanaonekana kuwa tofauti na timu hiyo hata ikishinda mechi yake inayofuata bado inakuwa haijajihakikishia kufuzu.

TP MAZEMBE

Kichapo cha ugenini dhidi ya Monastir na ikiwa Yanga itaibuka na ushindi nyumbani dhidi ya Real Bamako vitaiweka TP Mazembe katika nafasi finyu ya kufuzu robo fainali kwani baada ya hapo itahitajika kushinda mechi zake mbili za mwisho huku kuiombea njaa Yanga dhidi ya Monastir.

WASIKIE WADAU

Aliyewahi kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Dk. Athuman Kihamia alisema kuwa mashindano hayo ni magumu na ndio maana ni timu chache zenye uhakika wa kwenda robo fainali hadi sasa.

"Timu nyingi Afrika zinaonekana kujiandaa vizuri na zimefanya uwekezaji mkubwa ndio maana unaona kuna timu maarufu hazijawa na uwezekano wa kusonga mbele hadi sasa hivyo Yanga na Simba zimejitahidi sana hadi sasa," aisema Kihamia.

Beki za zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kuwa Simba na Yanga zinapaswa kuhakikisha zinapata uhsindi katika mechi zao.

"Kwa sasa jambo la muhimu ni kupata ushindi katika mechi zao zilizobakia na baada ya hapo ndio mengine yatafuata. Mpira wa Afrika umebadilika na hakuna timu nyepesi hivyo kila mechi waipe uzito mkubwa," alisema Pawasa.

Columnist: Mwanaspoti