Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maafikiano ya katiba 2014

Turudipic Wastaafu Jakaya Mrisho na Mohamed Shein

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza chini ya utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amewaomba Watanzania waweke kiporo hoja ya Katiba mpya ili kwanza ajenge uchumi na kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja. Kama sote tunakubaliana naye basi turudi kwenye makubaliano ya mwaka 2014.

Hakuna ubishi na ambaye atakuwa halioni hili basi tutatilia shaka uzalendo wake, kuwa hoja ya Katiba mpya imeanza kuligawa taifa letu katika vipande vipande na kuibua chuki ambayo inaanza kutishia amani na umoja wa kitaifa.

Sasa kwa kuwa Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM anaona uchumi hauwezi kujengwa katikati ya vuguvugu la madai ya Katiba mpya, basi turejee mezani kutekeleza makubaliano yale ya 2014 katika kipindi hiki cha mpito.

Nasema hivyo kwa sababu mazingira yaliyozaa makubaliano hayo yanafanana sana na tuliyonayo sasa kuelekea 2025 kwamba dalili za kwenda kwenye uchaguzi mkuu bila Katiba mpya zinaonekana wazi kama zilivyokuwa wazi mwaka 2014.

Wakati huo hali ikiwa tete Bunge Maalumu la Katiba, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alikutana na viongozi wakuu wa vyama vya siasa na kukubaliana njia za kwenda katika uchaguzi mkuu wa 2015 bila kuwa na Katiba mpya.

Katika makubaliano hayo, vilikubaliana kuifanyia mabadiliko ya 15 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ili kuruhusu mambo manne muhimu kufanyika na mojawapo likiwa ni la uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania.

Mambo mengine vyama hivyo vilikubaliana chini ya Kikwete aliyekuwa pia mwenyekiti wa CCM ni mshindi kiti cha rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50, uwepo wa mgombea huru na matokeo ya rais kuweza kupingwa mahakamani.

Katika makubaliano hayo, CCM kiliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti Phillip Mangula, wakati viongozi wa upinzani waliotia saini ni James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Dk Willibroad Slaa (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF).

Wengine walioweka saini zao katika makubaliano hayo ni Augustine Mrema (TLP), John Cheyo wa UDP na Mwenyekiti wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) na Fahmi Dovutwa wa UPDP ambaye aliwakilisha vyama vilivyokuwa ndani ya TCD.

Kufanyika kwa makubaliano hayo zilikuwa ni jitihada za makusudi kati ya Rais Kikwete wakati huo, CCM na viongozi hao wa upinzani ili kunusuru mchakato wa Katiba mpya ambao ulikuwa umewagawa Watanzania katika makundi mawili.

Upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao walikuwa wamesusia vikao vya Bunge la Katiba walirejea bungeni na kukamilisha mchakato huo hadi kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa na ilibakia tu wananchi kuipigia kura.

Lakini pamoja na makubaliano hayo, CCM ambao ndio chama tawala walipaswa kuisimamia Serikali itekeleze makubaliano hayo, haikufanya hivyo na upinzani wakaingia kwenye mtego na wakashiriki uchaguzi mkuu 2015.

Bado najiuliza sana sipati majibu, kwamba upinzani walipumbazwa na nini hadi wakakubali kuingia katika uchaguzi huo bila mabadiliko hayo madogo ya Katiba kwa sababu pengine hayo wanayoyalalamikia leo yasingelikuwepo.

Badala yake wapinzani wakaingia uchaguzi mkuu 2015 wakati makubaliano hayo hayajatekelezwa na wakawa baridi kama hakuna walichokuwa wamekubaliana, na wakaingia tena uchaguzi Serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

Hata kabla ya makubaliano hayo, Tanzania kama nchi tulikuwa na msingi wa hukumu ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mkuu Francis Nyalali, walishauri kifungu cha Katiba kinachozuia matokeo ya urais kuhojiwa kirekebishwe.

Katika ukurasa namba 176 wa taarifa za sheria au Tanzania Law Reports (TLR), ya mwaka 1996 ambayo ilinukuu hukumu ya majaji hao watatu, walishauri kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu 1995.

Nikiwanukuu Jaji Nyalali, Robert Kisanga na Lameck Mfalila walisema “kutokuwepo kwa kifungu hicho cha sheria katika uchaguzi unaoshirikisha vyama vingi inashangaza na kutokuwepo kwake ni mwanzo wa kukaribisha vurugu”.

Kuna kila dalili kwamba hiki kilichosemwa na majaji hao wanaoheshimika sana nchini kinaweza kulikumba taifa letu siku si nyingi na ndio maana ninaona busara ituongoze kutekeleza makubaliano ya 2014 tukisubiri mchakato wa katiba.

Rais Samia akizungumzia mchakato wa Katiba mpya alisema “Naomba nipeni muda nisimamishe nchi kwanza kiuchumi halafu tutashughulikia mengine. Tutashughulikia Katiba mpya, tutashughulikia mikutano ya hadhara”.

Kwa sababu kauli hii ya Rais ya kutaka Watanzania wampe muda haina kikomo (time frame), ndio maana kwangu mimi naona busara itutume kutekeleza makubaliano yale ya 2014 kwa dhamira njema ya kulivusha taifa letu 2025.

Hata hivyo, siku chache zilizopita nimemsikia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akiwataka viongozi waweke wazi huo muda anaotaka apewe ni kuanzia lini hadi lini.

Kauli hiyo ya Warioba imezua mjadala kwakuwa baadhi ya watu wanataka Rais Samia asipangiwe cha kufanya wala asilazimishwe kwa kupewa muda wa kutekeleza jambo fulani, kwakuwa kila kiongozi anapoingia madarakani huingia na vipaumbele vyake.

Mambo yote yanayogusa masilahi ya taifa ni vema umma uelimishwe kwa kina ili uwe na uelewa mpana wa kuhoji, kujibu maswali na kutolea ufafanuzi. Tusipokuwa makini mchakato wa Katiba mpya itatutenganisha badala ya kutuunganisha.

Columnist: www.tanzaniaweb.live