Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maadili na heshima ya taasisi

E14f141ce44a66f50de726b332f28780 Maadili na heshima ya taasisi

Thu, 22 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Maadili na heshima ya taasisi

Katika makala iliyopita, tuliangalia mtanziko unaohusisha watu wengi (multi-person dilemma), ili tuweze kuielewa vizuri aina hii ya mtanziko, kuanzia kwenye maana yake, maelezo yake na mifano yake katika utumishi wa umma.

Katika toleo hili, tutaangalia uhusiano uliopo kati ya maadili ya utumishi wa umma na heshima (reputation) inayojengeka katika taasisi, ambapo pamoja na mambo mengine, tutaangalia maana ya heshima kwa taasisi, namna maadili yanayoweza kuleta heshima kwa taasisi husika na manufaa ya heshima hiyo kwa taasisi.

Kwa mujibu wa Bendixed na Abratt kwenye chapisho lao la mwaka 2007, lenye kichwa cha habari “Corporate Identity, Ethics and Reputation in Supplier–Buyer Relationships” wanabainisha kuwa heshima kwa taasisi ni muonekano mzuri wa taasisi ambao umejengwa kwa muda mrefu.

Mtazamo wa Bendized na Abratt, unaenda sambamba na mtazamo wa Gibson, Gonzales na Castanon katika chapisho lao la mwaka 2006 lenye kichwa cha habari “the Importance of Reputation and the Role of Public Relations”, ambapo msisitizo wao mkubwa umelala kwenye ukweli kwamba uwezekano wa taasisi kujenga heshima unatokana na taasisi husika kuzingatia maadili kwa muda mrefu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa kifupi, Mella na Gazzola, katika chapisho lao la mwaka 2015 lenye kichwa cha habari “Ethics builds reputation” wamesisitiza kuwa taasisi inayoishi na kutekeleza majukumu yake kila siku kwa kuzingatia maadili ina nafasi kubwa sana ya kujijengea heshima mbele ya wadau wake.

Hili ni jambo la kweli na la wazi kabisa kwavile maadili ya utumishi wa umma, yanaambatana na kanuni mbalimbali ambazo utekelezaji wake una nafasi kubwa ya kuifanya taasisi husika, kuwa na heshima kubwa mbele ya wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na jamii nzima ya kitanzania kwa ujumla wake.

Kwa mfano, kanuni mojawapo katika utumishi wa umma nchini inamtaka mtumishi wa umma kutoa huduma bora kwa watu wote wanaohitaji huduma za taasisi husika. Ni wazi kuwa taasisi inaweza kujijengea heshima kubwa miongoni mwa wateja wake, endapo wateja hao wataona kuwa taasisi hiyo inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa wateja wanapata huduma bora kulingana na ahadi ya taasisi husika.

Mfano mwingine mzuri ni kanuni ya utumishi wa umma, ni kanuni inayomtaka mtumishi wa umma kuzingatia matumizi sahihi ya taarifa. Ni wazi kuwa taasisi haiwezi kuheshimika mbele ya wadau mbalimbali, endapo taasisi hiyo imejijengea tabia ya kutozingatia matumizi ya taasisi mbalimbali.

Hii inatokana na ukweli kuwa taasisi za umma zinatunza taarifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na taarifa za wadau mbalimbali kama watumishi, wazabuni na wateja wengine wa nje. Endapo taarifa hizo zitatumika kinyume na matarajio kuna uwezekano mkubwa wa kuleta madhara mbalimbali kwa wateja hao na hivyo kushusha heshima ya taasisi.

Heshima inayojengeka katika taasisi kutokana na taasisi ya umma kuzingatia maadili, inaweza kuleta matokeo mazuri sana kwa taasisi husika. Kwa mfano, watu mbalimbali wenye sifa za kutosha wanaweza kutamani kuajiriwa na taasisi inayoheshimika na hivyo taasisi inaweza kupata watumishi wenye sifa stahiki kwa urahisi zaidi.

Watu wanaweza kupenda kuajiriwa na taasisi zenye heshima katika jamii kwa vile wanajua kwamba wanaweza kuchangia juhudi na maarifa yao kwenye taasisi husika huku wakiwa na uhakika wa kupata matunda yanayotokana na juhudi zao bila shida pale hali inaporuhusu.

Vilevile, wazabuni waadilifu na wenye sifa zinazokidhi vigezo mbalimbali wanaweza kujitokeza kwa urahisi kwenye taasisi iliyojijengea sifa za kutosha kutokana na uwezo wake wa kuzingatia maadili katika utendaji wao wa majukumu ya kila siku.

Wazabuni wenye sifa wanaweza kupenda kufanya kazi na taasisi zenye heshima mbele ya wadau mbalimbali kwa vile wanajua kinachohitajika kutoka kwao ni uwezo wa kutekeleza mikataba ya zabuni na pia wazabuni hao wanaweza kupata heshima vilevile kutokana na mchango wao kwa taasisi husika.

Vilevile, wateja mbalimbali wanaweza kujitokeza kununua bidhaa au huduma za taasisi husika kwa vile wanajua kwamba taasisi hiyo inaheshimika kutokana na kuzingatia maadili katika utendaji wake wa majukumu ya kila siku.

Hii inatokana na ukweli kuwa taasisi zilizoweza kujijengea heshima kutokana na uadilifu zinaaminiwa na walaji wa huduma hizo kwamba thamani ya fedha wanazotumia katika kupata bidhaa au huduma kutoka katika taasisi inayoheshimika inalingana na huduma au bidhaa wanazopata.

Columnist: habarileo.co.tz