Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maadhimisho ya Miaka 50 ya Kuanzishwa kwa TAZARA -3

E57932c0955211caea106fb40819d4bd Maadhimisho ya Miaka 50 ya Kuanzishwa kwa TAZARA -3

Wed, 2 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

'TAZARA Lazima Iendelee Kuangaza kama Ishara ya Urafiki kati ya China na Afrika'

MIMI nilikuwa mmoja wa maofisa walioshiriki kikamilifu katika ujenzi wa reli ya TAZARA kuanzia hatua ya upimaji na katika ujenzi wake hadi ilipofika Tunduma. Nikiwa Waziri wa Mawasiliano na Ujenzi katika kipindi chote cha ujenzi wa TAZARA, nilijihusisha sana na mradi huo. Lakini kabla ya yote liko suali, “kwa nini TAZARA ilijengwa?” Sababu muhimu ya kwanza ilikuwa kusaidia harakati za kupinga ukoloni, hususan katika eneo la kusini mwa Afrika, na kusaidia wananchi wake kupata uhuru wao.

Marais Julius K. Nyerere na Kenneth Kaunda waliziendea kwanza nchi za Magharibi, kuomba fedha ya kujenga reli hiyo, lakini wote walikataa na kupuuza wazo hilo. Katika mkutano wa maraisi hao wawili na mwenyekiti Mao Zedong, Beijing, Mwenyekiti Mao aliwauliza, “Je, reli hii itasaidia ukombozi wa Afrika?” Jibu lao lilikuwa, “Ndiyo” na mwenyekiti akasema, “Basi itajengwa.” Huo ndio uliokuwa mwanzo.

Nilishiriki katika kila hatua ya mradi huo. Nilitembea kwa miguu urefu wake wote kutoka Kisarawe hadi Tunduma, na licha ya shida na hatari zote: kutembea katika mapori mlimokuwa na nyoka wa hatari na wanyama wakali, na kuvuka mito iliyokuwa na mamba katika mitumbwi midogo; licha ya yote hayo nilifurahia kushiriki kwangu katika hatua zote. Nilipata fursa ya nadra ya kuwafahamu rafiki zetu kutoka China; wapimaji, wahandisi na wafanyakazi wa kawaida, nikihusudu ujasiri wao, bidii zao katika ufanyaji wa kazi ngumu, ustahimilivu wao na kujitolea mhanga. Nilifurahi pia kuona wafanyakazi wa Tanzania wakifanya kazi kwa bidi na ilikuwa kazi yangu kuwapa moyo na kuwashauri kuiga mfano wa wafanyakazi kutoka China.

Nilipata fursa ya kufahamu mambo mengi kuhusu Wachina, historia yao na utamaduni wao. Urafiki wa dhati ulijengwa kati ya nchi zetu tatu na watu wake. Nilikuja kuwapenda sana Wachina baada ya kujifunza na kuelewa jinsi walivyoteseka chini ya utawala wa kigeni na jinsi walivyopambana ili kuikomboa nchi yao.

Tangu kukamilika kwake, TAZARA imeleta manufaa mengi kwa Tanzania. Kabla ya kujengwa, nchi yetu ilikuwa bado kufunguka. Watu wetu hawakuwa na uwezo wa kusafiri kwenda kokote na hawakuwa na uwezo wa kusafiri hadi kufika Dar es Salaam, mji mkuu na bandari kuu. Hawakuweza kusafirisha mazao yao ya kilimo kwenda kwenye masoko mijini. Hivyo, hawakuweza kujipatia fedha za kuboresha maisha yao. Maliasili kama makaa ya mawe yaliyo kusini mwa nchi yetu yasingeweza kuchimbwa na kutumiwa kwa kutokuwepo kwa njia za usafirishaiji. Kisiasa TAZARA iliunganisha nchi na kuwafanya watu wote waone kuwa ni wamoja kwenye taifa moja. Hadi leo Tanzania bado inavuna faida ya TAZARA.

Faida nyingine muhimu, ukiacha zile za mali nilizotaja hapo juu, ni urafiki wa karibu sana na uliochanua miongoni mwa Wachina, Watanzania na Wazambia wakati wote wa ujenzi wa TAZARA. Hatukuwafahamu Wachina wala historia yao kabla ya hapo. Tuliyofahamu juu yao yalitokana na propaganda za nchi za magharibi na yalikuwa hasi. Hizo propaganda zilisema Wachina hawakuwa na uwezo wa kujenga reli hii kwa sababu, eti hawakuwa na karakana za kuzalisha chuma cha pua. Wakati mmoja nilikutana na waandishi wa habari kutoka nchi za magharibi na mmoja wao aliponiuliza swali hilonilimjibu kuwa badala ya chuma tungetumia mianzi na kuitandika kwenye njia ya reli hiyo, na baada ya kufanya hivyo tungetumia kile kitabu kidogo chekundu cha fikra za mwenyekiti Mao kuibadili mianzi ile kuwa chuma cha pua. Niliwambia hivyo kwa utani kuonyesha walivyopotoshwa na propaganda zao wenyewe.

Ujenzi wa TAZARA uliendeshwa kwa 'Moyo wa TAZARA'. Nionavyo mimi sifa kubwa ya kwanza ya 'Moyo wa TAZARA' ilikuwa mshikamano wa dhati uliyowaunga kwa pamoja wafanyakazi wa nchi zote tatu katika ngazi zote, mshikamano uliomfanya kila mmoja wao kujihisi kuwa ni sehemu ya mradi wa kihistoria ambao ungekuwa mchango katika kuleta ukombozi wa nchi zilizo kusini mwa Afrika na kuikomboa Zambia kutoka kwa ngome ya wakoloni na nchi za ubaguzi wa Rhodesia ya Kusini na Kusini mwa Afrika.

Hii ilikuwa aina mpya kabisa ya kazi yenye, ushirikiano, kujitolea mhanga na mshikamano kwenye ngazi ya chini kabisa. Tayari urafiki na ushirikiano kati ya viongozi wa nchi zetu tatu na kati ya serikali ulikuwapo. Urafiki na ushirikiano miongoni mwa watu wa kawaida lilikuwa jambo jipya katika uhusiano wa kimataifa. Wafanyakazi wote walioshiriki katika ujenzi wa TAZARA waligawana kila walichokuwa nacho kwa usawa. Hakuna aliyeachwa nyuma na Wachina waliwachukulia wafanyakazi Watanzania na Wazambia kama ndugu zao.

Ilikuwa wazi kuwa wafanyakazi wa Kichina na viongozi wao kwenye ujenzi wa TAZARA walikuja na dhamira iliyokuwa wazi; kuhakikisha kuwa reli ya TAZARA inajengwa kwa ufanisi wa kiwango cha juu sana na kwamba unakamilika katika muda. Ndiyo sababu uchapaji kazi, kujitolea na ushirikiano vilikuwa siri ya mafanikio ya mradi. Wakati ule kama nilivyokwisha sema, kulikuwa na propaganda kali dhidi ya viongozi wa China, serikali yao na watu wake. Mwanzoni, baadhi ya wataalam wetu waliosoma katika nchi za magharibi hawakuwa tayari kufuata ushauri wa kisayansi na ufumbuzi wa kihandisi wa wataalamu wa China.

TAZARA inaashiria urafiki na uamuzi wa Wachina waliokuja Tanzania na Zambia, na walijitolea. Lazima iwe katika kila njia kuendeshwa kama mradi wa kunufaika kwa pande zote kwa nchi hizo tatu ambazo ziliijenga. Kufanikiwa kwake lazima kupimwa kwa suala la faida ambayo inaendelea kuwapa watu wa Tanzania na Zambia lakini pia kwa nchi zingine za kusini mwa Africa. Lazima iendelee kung'aa kama ishara ya urafiki kati ya China na Afrika.

(Nakala hii ni dondoo wa hadithi ya marehemu Mhe. Job Lusinde kuhusu TAZARA katika kitabu kipya kilichozinduliwa Kumbukumbu la Urafiki Kati ya China na Afrika: Simulizi za Waliokuwapo Wakati wa Ujenzi wa TAZARA).

Columnist: habarileo.co.tz