Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Uefa wamechutama, Caf, TFF chutameni

Rais Karia Picc Data MZEE WA UPUPU: Uefa wamechutama, Caf, TFF chutameni

Wed, 25 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

WASWAHILI wanasema muungwana akivuliwa nguo huchutama. Hivi ndivyo walivyofanya watawala wa soka barani Ulaya, Uefa.

Baada ya kugundua wamevuliwa nguo na makosa yao miongo miwili iliyopita, wamechutama kujisitiri. Ni hivi. Hapo zamani za kale Uefa walikuwa wakiandaa mashindano matatu kwa ngazi za klabu. Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Washindi Ulaya na Kombe la Uefa au Uefa ndogo kama Waswahili walivyoibatiza.

Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa (na hadi sasa) maalumu kwa ajili ya mabingwa wa kila nchi, yaani nchi moja bingwa mmoja. Mashindano haya yalianza 1955. Kombe la Washindi Ulaya lilikuwa maalumu kwa washindi wa kombe la shirikisho la nchi. Mashindano haya yalianza 1960.

Na Kombe la Uefa au Uefa ndogo ilikuwa maalumu kwa timu zilizomaliza nafasi za juu kwenye ligi zao, lakini hazikushinda taji lolote. Mashindano hayo yalianza 1971. Mashindano yalienda vizuri hadi msimu wa 1998/99 pale Uefa ilipoamua kuliua kombe la washindi.

Walifanya hivyo ili kuyatanua mashindano ya ligi ya mabingwa, kwamba kuanzia msimu wa 1999/2000 timu zaidi ya moja kutoka nchi moja zishiriki. Yaani zile timu ambazo hapo awali zilikuwa zinaangukia kwenye Uefa ndogo nazo ziingie kwenye ligi ya mabingwa.

Hii ikasababisha zile timu zilizokuwa zikishiriki kombe la washindi kwa kutwaa kombe la shirikisho nchini kwao, ziangaukie kwenye Uefa ndogo. Kwa hiyo Ulaya yakabaki mashindano mawili tu - Ligi ya Mabingwa Ulaya na Uefa ndogo.

Kufikia 2009, Uefa ndogo nayo ikabadilishwa mfumo, muundo na jina sasa ikawa Europa League. Lakini kuwa na mashindano mawili tu ni kusababisha mkanyagano mkubwa kuwania nafasi katika bara ambalo klabu zake zina uchumi mzuri na kutamani kushiriki mashindano ya bara.

Wakagundua kwamba walikosea kuondoa kombe moja, na sasa wamelirudisha kwa jina lingine la Uefa Europa Conference League. Haya ni mashindano maalumu kwa timu zilizomaliza katika nafasi za juu kwenye ligi za nchini mwao, lakini hazikufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya wala Europa League.

Mashindano haya yanatoa nafasi kwa timu za kutoka mataifa madogo ya Ulaya ambazo haziwezi kufuzu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya angalau nazo kucheza mashindano ya Ulaya. Huu ni uungwana ambao Uefa wamefanya.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) pia tulikuwa na mashindano matatu kwa kufuata mfumo uleule wa Uefa. Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ilianza 1965, Kombe la Washindi Afrika lililoanza 1975 na Kombe la Caf ambalo lilianza 1992.

Lakini kwa kuiga mabadiliko ya Ulaya, mwaka 2003 Caf likayaunganisha mashindano ya Kombe la Caf na Kombe la Washindi Afrika na kuzaliwa mashindano mapya ya Kombe la Shirikisho Afrika. Hii ikafanya Afrika kuwe na mashindano mawili tu - bara lenye mataifa wanachama 54.

Matokeo yake kuna nchi ambazo hazipati kabisa wawakilishi katika mashindano ya bara. Hapa namaanisha ile hatua ya makundi ambayo ndiyo ligi yenyewe. Kuwa na timu inayoshiriki hatua ya makundi ya mashindano ya bara lake ni jambo zuri sana katika mpira wa nchi yoyote duniani.

Hii huwapa mashabiki wa soka nafasi ya kushuhudia maajabu ya soka la ngazi ya bara, kujipima na klabu za mataifa mengine. Tanzania kwa mfano, tumeshuhudia mzuka wa Afrika mara nne tu tangu mfumo huu uanze.

Lakini kuna nchi hazijawahi kabisa. Huku ni kuua mzuka wa mpira badala ya kuukuza. Ni wakati muafaka kwa Caf kuanzisha mashindano mengine ili kufungua wigo wa nchi kupata uwakilishi wa kibara.

Tunajua kwamba kuna mashindano ya Caf Super League yanakuja, lakini hata hivyo hayo ni ya timu chache na ushiriki wake ni wa tofauti sana. Tunataka mashindano ambayo timu zitafuzu kupitia mafanikio kwenye ligi zao kama ilivyo kwa ligi ya mabingwa au kombe la shirikisho. Tuleteeni mashindano mengine jamani.

Kwa TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, zamani Tanzania kulikuwa na Ligi ya Muungano. Ligi hii ambayo ilianza 1982 ndiyo ilikuwa Ligi Kuu ya Tanzania na bingwa ndiye alikuwa bingwa wa Tanzania. Ligi hii ilishirikisha timu kutoka Ligi Kuu Bara na Ligi Kuu Zanzibar, idadi ilitokana na nyakati.

Kwa mfano mwaka 1982 yalipoanza kulikuwa na timu nne tu, mbili kutoka kila upande. Baadaye zikaja timu sita, tatu kutoka kila upande na msimu wake wa mwisho 2003 zilikuwa nane - nne kutoka kila upande.

Mzuka ulikuwa mkubwa sana enzi zile na nchi iliunganishwa kweli. Fikiria timu ya Jamhuri kutoka Pemba inakwenda Tabora kucheza na Milambo FC. Mzuka ulikuwa mkubwa, lakini sasa zimebaki stori tu.

Ni wakati muafaka kwa TFF kuturudishia mashindano yale hasa katika kipindi hiki ambacho nafasi za Afrika ziko nne. Nafasi moja itengwe kwa ajili ya Ligi Muungano, mshindi wake apate nafasi ya kushiriki angalau Kombe la Shirikisho Afrika. Tuchutame wazee.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz