Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Tutumie sheria ya wachezaji wa kigeni kutengeneza pesa

Wacezaji Wageni Tutumie sheria ya wachezaji wa kigeni kutengeneza pesa

Wed, 17 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hii ni makala ambayo ilitoka kwenye ukurasa huu, Januari 2021. Leo nimeamua kuirudia tena baada ya kuona marekebisho ya sheria ya wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu.

Katika makala hii niliiandika wakati ule sheria ikiruhusu wageni 10. Baadaye sheria ikafanyiwa mabadiliko na kuruhu wgeni 12, lakini kwenye mechi moja wacheze wasiozidi wanane. Sasa imefanyiwa tena mabadiliko kuruhusu wote 12 kwenye mchezo mchezo mmoja.

Ni hivi... Sheria ya usajili wa wachezaji wa kigeni Tanzania inaruhusu kila klabu kusajili wachezaji wasiozidi 12. Walioitunga sheria hii wanasema lengo lake ni kulinda vipaji na ajira kwa wachezaji wazawa.

Sitaki kujadili faida au hasara zake, lakini nataka kufungua mabano kuonesha ni namna gani tunaweza kulinda vipaji bila kuwa na kikomo cha wachezaji wa kigeni huku kila klabu ikinufaika. Tunapozungumzia kulinda vipaji tunamaanisha tunazibana klabu ili kutoa nafasi kwa wazawa kuwaendeleza na kuwatumia.

Lakini, hata hivyo, kuna mkakati mwingine utakaozishawishi klabu kuwapa nafasi wazawa au kuendeleza vipaji vya ndani.

TUFANYE HIVI

Badala tu ya kuzibana klabu na kuzitia udhaifu na unyonge tutengeneze mazingira ya kuzifanya ziifurahie sheria hii. Tutunge sheria itakayozitia moyo klabu kuwekeza kwa vijana na kuwapa nafasi, badala ya kuzitungia sheria yenye vitisho au kuzibana kwa ukomo wa idadi.

Kusiwe na sheria wala kanuni inayoweka kikomo cha wachezaji wa kigeni, badala yake iwepo sheria inayotoa vigezo kwa klabu kuwa na idadi fulani ya wageni.

Sheria iseme hivi, klabu itakayowalea vijana na kuwapandisha angalau watatu kwenye timu ya wakubwa na kuwapa nafasi angalau asilimia 15 ya msimu itapewa nafasi mbili zaidi za wachezaji wa kigeni.

Siyo mradi tu wachezaji wazawa, hapana.Ni lazima wawe

kutoka kwenye timu ya vijana. Klabu ambayo itakuwa na wachezaji wazawa lakini imewanunua wakiwa tayari wakubwa, haitapata hata nafasi moja. Hii itazifanya klabu zikazane kuwakuza vijana na kuwapa nafasi ili ziongezewe idadi ya wachezaji wageni.

Katika kufanya hivyo, wachezaji wazawa watakuwa wanapata nafasi kidogo kidogo na kuwasaidia kukua zaidi.

Klabu kama Yanga na Simba ambazo msimu huu hazijatoa nafasi kwa kijana hata mmoja kutoka akademi maana yake zisiruhusiwe kusajili mgeni hata mmoja wa kigeni. Azam FC ambayo msimu huu imempandisha kipa Twalib Nooru, ikimpa muda wa mechi angalau asilimi 15, msimu ujao iongezewe nafasi moja zaidi ya mchezaji wa kigeni.

Hapo ni lazima klabu zitatafuta uwiano wa muda wa mchezo kwa wageni na wazawa hasa kutoka akademi zao ili kuendelea kupata hizi nafasi za kusajili wachezaji wa kigeni. Wachezaji wa kigeni ni muhimu katika maendeleo ya wachezaji wazawa. Tunapokuwa na wageni wengi maana yake vijana wetu wengi wanajifunza.

Wakati Shomary Kapombe anashinda tuzo ya Taswa ya mwanamichezo bora wa 2011 (tuzo zilitolewa 2012), alisema waliomsaidia kufikia mafanikio hayo walikuwa Emmanuel Okwi na Patrice Mafisango. Ni vijana wangapi leo hii wangependa kuwa kama Clatous Chama, Prince Dube au Fiston Mayele?

Hatuwezi kuwaendeleza vijana kwa kuwazuia wageni. Tuwaache wageni waje ili watusaidie kuwaboresha vijana. Lakini tutunge sheria itakayowafanya wageni waje huku wazawa wakifaidika na klabu kupata pesa.

KIVIPI

Kutokana na sheria hii, kuna klabu zitajikuta hazina kabisa nafasi ya kusajili wachezaji wa kigeni kutokana na kutotoa muda wa mechi kwa vijana wa akademi. Lakini, kwa kuwa wachezaji wa kigeni ni muhimu, klabu hizi ziruhusiwe kununua nafasi za wachezaji wa kigeni kutoka klabu ambazo zina nafasi, lakini hazina uwezo wa kumudu wageni au hazitaki.

Tuichukulie Ruvu Shooting ya Massau Bwire kama mfano. Msimu huu iwe imepandisha vijana watano na kuwatumia kwa zaidi ya asilimia 15. Hii itawapa fursa ya kusajili wachezaji wa kigeni 15 msimu ujao. Lakini hawataki kusajili wachezaji wa kigeni, labda kwa sera zao tu au hawana fedha za kumudu wageni, basi waruhusiwe kuziuza nafasi zao kwa timu zenye kutaka wageni, lakini zimekosa fursa kwa sababu ya kutoendeleza na kuwapa muda wa mechi wazawa. Endapo Ruvu Shooting itauza nafasi moja kwa Sh10 milioni maana yake itapata milioni 150 kwa nafasi zake 15.

Hizi ni fedha nyingi zitakazoisaidia klabu hiyo kujiendesha na kuongeza ushindani kwenye ligi. Klabu nyingi zitapambana kuzalisha wachezaji na kuwatumia kwa sababu watapata fursa ya kujiongezea kipato kwa kuuza nafasi.

Hapa tutakuwa tunaufanya mpira kama biashara ya kilimo cha mihogo. Mizizi biashara, majani biashara na gogo biashara.

Klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam zina uwezo mkubwa wa kifedha na zinaweza kutengenezewa mazingira ya kugawana fedha zao na wenzao ili maisha yaende.

Klabu hizi zinashiriki mashindano ya kimataifa na zinahitaji wachezaji wengi wa kigeni kuweza kushindana na klabu kubwa za nje.

Sasa hii ni fursa kwao kupata wachezaji watakaoweza kuzisaidia kwenye mashindano hayo. Lakini pia itazisaidia timu ndogo kujipatia kipato kitakachozisaidia kujiendesha. Hapohapo tutakuwa tunahakikisha kwamba vijana wetu kutoka akademi wanapata muda wa uwanjani na klabu zinawekeza kwelikweli kwenye akademi.

Sheria ya sasa inataka kila klabu iwe na timu ya vijana, lakini kimsingi klabu nyingi zinaishi kiujanja ujanja zikiwa hazina timu halisi za vijana.

Lakini kwa sheria hii, timu zitatia msisitizo kwenye akademi zao na lengo litafikiwa. Tunapotunga sheria tuhakikishe zinawalinda wachezaji wetu mtaani, lakini pia zinatengeneza fursa za kibiashara kwa watekelezaji wa sheria hizo.

Columnist: Mwanaspoti