Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Tuishi na kauli ya Tony Kroos - tuzo zimejaa upendeleo

Mgunda Kocha wa Simba, Juma Mgunda

Wed, 14 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mapema mwaka 2021, kiungo wa kimataifa wa Ujerumani na klabu ya Real Madrid ya Hispania, Tony Kroos, alitoa maoni yaliyoshtua wengi kuhusu tuzo za wanasoka bora, kuanzia kwenye mechi moja hadi zile za ngazi ya dunia; Ballon d’Or na The Best ya Fifa.

Nanukuu: “Soka limejaa ubaguzi na upendeleo, tuko wachezaji 11 au 22 uwanjani, lakini ni washambuliaji tu ndiyo hupewa kipaumbele katika kila mchezo.”

“Utadhani wanacheza tenisi au gofu, kwamba hakuna aliyewapa pasi. Nasoma habari nyingi za upendeleo na ubaguzi kwenye vyombo vingi vya habari siku hizi.

“Wanachofanya ni kuangalia nani aliyefunga na kuwalinganisha wafungaji tu katika msimu, na kuanza mijadala ya Ballon d’or kwa sababu ya mabao yao, na kusahau waliwezaje kufunga mabao mengi.

“Nani alijituma bila kuchoka kuwasaidia hao washambuliaji? Ni timu nzima. Mpira huanzia kwa kipa na humalizikia eneo la hatari la mpinzani. Kila mchezaji anastahili kutambuliwa mchango wake kwenye wakati wa Ballon d’or kama kusingekuwa na ubaguzi na upendeleo.

“Wanatakiwa waweke wazi kama tuzo hizi ni kwa ajili ya wale tu wanaofunga mabao, ili walinzi, viungo na makipa wasijichoshe...waishi kwa amani.

“Nadhani kuanzishwa kwa tuzo za mtu mmoja mmoja kwenye soka lilikuwa wazo baya sana. Wachezaji 11 wanajitoa kwa ajili ya timu katika msimu mzima, lakini ni mmoja tu atakayepatiwa tuzo badala ya timu timu nzima.

“Mpira ni ushirikiano siyo kazi ya mtu mmoja mmoja.”

Mwisho wa kunukuu.

Nayachukua maoni haya na kurudi nayo kwenye soka letu la Tanzania.

Ukiwa mtu unayefuatilia tuzo zinavyotoka, utaona kabisa kwamba kuna upendeleo mwingi unaoendelea kwenye mpira wetu.

Rejea tuzo za mchezaji bora wa Tanzania msimu wa,2020/21, John Bocco.

Bocco alikuwa mchezaji bora wa msimu kwa sababu alikuwa mfungaji bora, sifa ambayo pia alikuwa nayo George Mpole msimu uliofuata, lakini hakushinda hiyo tuzo.

Ukiangalia timu ambayo alikuwa akiichezea Mpole hadi kuwa mfungaji bora, na ukiilinganisha na timu aliyoichezea Bocco, utaona kabisa Mpole alistahili.

Bila kumvunjia heshima gwiji Bocco, Mpole alifunga magoli magumu na ya uwezo binafsi huku Bocco akifunga mabao mengi ya penalti.

Huo msimu wa John Bocco ndiyo ambao kiungo Iddy Nado wa Azam FC alifunga mabao 10 na kutoa pasi 8 za mabao.

Lakini hakuwemo hata kwenye kuwania kiungo bora, acha mchezaji bora wa msimu...nani alikuwemo? Tonombe Mukoko na Feisal Salum.

Tonombe kiungo mgumu ambaye anacheza mechi mbili katika mchezo mmoja, dhidi ya wapinzani na dhidi ya mpira wenyewe...yaani anagombana na mpira mechi nzima.

Feisal Salum wa 2020/21 alimaliza msimu hana hata asisti moja...halafu ni kiungo wa ushambuliaji.

Alifunga mabao matano, ambayo yalikuja kwenye robo ya mwisho ya msimu.

Sasa tunatafuta kiungo bora wa msimu, tunamuacha mtu aliyefanya vizuri msimu mzima ja kumchukua mtu aliyejitahidi kwenye robo moja ya msimu...robo nyingine tatu alikuwa mtazamaji anayecheza.

Huo ndiyo upendeleo anaouzungumzia Tony Kro-os.

Rejea kwenye tuzo za kocha bora wa mwezi Novemba, 2022 halafu fananisha na tuzo za kocha wa ligi ya vijana chini ya miaka 17 Julai mwaka huu.

Kali Ongala alistahili kushinda tuzo ya Novemba, lakini ikaenda kwa Juma Mgunda wa Simba.

Mohamed Badru alistahili kushinda tuzo za kocha bora wa ligi ya chini ya miaka 17, lakini ikaenda kwa Nico Kiondo wa Simba.... upendeleo.

Mifano ni mingi sana kiasi kwamba mtu unaweza kudhani kwenye mamlaka za mpira hakuna watu wanaojua mpira unaendeshwaje.

Kama nilivyoanza huko juu kwa kumnukuu Tony Kroos, ujinga huu upo dunia nzima.

Rejea kauli ya Kevin de Bruyne wa Ubelgiji kwenye mchezo dhidi ya Canada kwenye Kombe la Dunia.

Alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi lakini yeye mwenyewe akasema hakustahili...kwa hiyo alipendelewa!

Tuishi kwenye kauli ya Tony Kroos, tuzo zimejaa upendeleo!

Columnist: Mwanaspoti