Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Tuanze kufikiria mashindano mapya

Simba Yanga 2021 Tuanze kufikiria mashindano mapya

Thu, 14 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mojawapo wa majukumu na wajibu wa chama chochote cha mpira duniani ni kuhakikisha mchezo huu mzuri unachezwa na kuchezwa tena. Ili mpira ukue na kuendelea kupendwa na kuvutia mashabiki wapya hasa watoto unatakiwa uchezwe sana yaani uchezwe na uchezwe tena.

Na ili uchezwe sana na uchezwe tena, ni lazima kuwepo na mashindano mengi. Ndiyo maana England, nchi inayoongoza kwa uchizi wa mpira, kuna mashindano matatu makubwa.

I. Ligi Kuu

Hii ndiyo ngazi ya juu zaidi ya soka nchini humo.

II. Kombe la FA

Mashindano yanayohusisha timu zote zilizosajiliwa katika mfumo rasmi wa soka nchini humo bila kujali madaraja. Haya ndiyo mashindano makongwe zaidi ya soka duniani.

III. Kombe la Ligi

Kwa sababu za kiudhamini mashindano haya yamekuwa yakibadilika jina ambapo kwa sasa yanaitwa Kombe la Carabao.

Mashindano haya yanaitwa Kombe la Ligi kwa sababu hushirikisha timu zote zinasoshiriki ligi rasmi za nchini humo.

Ligi Kuu, Championship, League One na League Two.

Katika mfumo wa soka la England, madaraja haya manne ndiyo huitwa League Football na chini ya hapo huhesabiwa kama Non League yaani mchangani, siyo ligi.

Kwa hiyo mashindano haya matatu huuchangamsha mpira wa England katika kila ngazi na kutoa nafasi kwa kila timu siku moja kukutana na timu kubwa. Mabingwa wa mashindano haya pamoja na zawadi zingine hupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Ulaya.

Bingwa wa Ligi Kuu (hadi nafasi ya nne) hupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bingwa wa Kombe la FA na Kombe la Ligi hupata tiketi ya kushiriki Europa League. Mashindano haya matatu ndiyo huwatia wendawazimu wa soka Waingereza na kuufanya mchezo huu kuwa biashara kubwa sana nchini humo.

Hiki ndicho ninachotaka Tanzania tuanze kufikiria kwa sasa. Robo fainali tatu za Simba SC kwenye mashindano ya Afrika ndani ya misimu mitano iliyopita imefanya ligi ya Tanzania kupanda viwango vya CAF hadi nafasi ya 11 kuanzia msimu ujao.

Na endapo Simba watafanya vizuri zaidi na kufika nusu fainali au hata zaidi kwenye Kombe la Shirikisho ina maana Tanzania inaweza kupanda zaidi.

Ikimbukwe kwamba ligi 12 za juu kwenye viwango vya CAF ndizo hupewa nafasi nne kwenye mashindano ya Afrika. Kwa hiyo Tanzania sasa tuna uhakika wa misimu miwili mbele kuwa na timu nne.

Endapo Simba wakiendelea kutubeba au timu zingine nazo mwakani zifanye vizuri na kufika mbali kwenye mashindano ya Afrika, maana yake nafasi zetu nne ni kama zitakuwa za kudumu. Na ikiwa hivyo, ndipo tuanze kufikiria kuanzisha mashindano mengine zaidi ya tuliyonayo kwa sasa.

Hadi sasa Tanzania ina mashindano mawili tu; Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam Sports. Na washindi wa mashindano haya ndiyo hupata tiketi ya kimataifa. Mawazo yangu ni kwamba zile nafasi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika kutokea Kombe la Azam Sports zipunguzwe ibaki moja tu kwa bingwa.

Halafu yaanzishwe mashindano mengine kama Kombe la Ligi kule England na bingwa wake ndiye apewe ile nafasi nyingine.

Hii ina maana kwamba Tanzania itakuwa na mashindano matatu ya ndani kwa msimu mmoja. Ligi Kuu, Kombe la Azam Sports na Kombe la Ligi. Halafu washindi wake wote watashiriki mashindano ya Afrika.

Hii itaongeza thamani ya mashindano, itaongeza thamani ya mpira na itaongeza burudani kwa mashabiki. Pia itaongeza thamani ya ligi zingine kwa sababu timu zake zitakuwa zinapata nafasi ya kushindana na timu kubwa hivyo kuvutia wadhamini. Inaweza isianze msimu ujao au hata misimu mitano ijayo, lakini tuanze kufikiria sasa.

Wakati Simba wakituheshimisha kimataifa na huku tukisubiri na wengine watuwakilishe vizuri Afrika, tuanze kufikiria kuanzisha mashindano mengine kama yale ya Carabao kule England kwa maendeleo ya mpira wetu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz