Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: TFF hili ni bahati mbaya au lilidhamiriwa

39855 Pic+karia MZEE WA UPUPU: TFF hili ni bahati mbaya au lilidhamiriwa

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SEPTEMBA 2014 aliyekuwa mkurugenzi wa Wanachama na Sheria wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Evodius Mtawala aliachia ngazi katika hali ya kushangaza akilalamikia mazingira magumu ya kazi.

Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa, lakini taarifa za chinichini zilieleza kwamba alishindwa kufanya kazi na watu wa klabu fulani waliopo ofisi kuu za Karume.

Mtawala ambaye kabla ya hapo alikuwa katibu mkuu wa Simba aliajiriwa Desemba 2013 na utawala wa Jamal Malinzi ambao uliingia madarakani Oktoba 2013 kurithi kazi nzuri ya Leodegar Tenga.

Malinzi alifanya kazi nzuri, lakini pia kulikuwa na makosa pia - mojawapo ni watu walioajiriwa kuwa na nasaba za Uyanga. Hakuna uhakika kama hii ilimtokea bahati mbaya au ilidhamiriwa, lakini ilitokea.

Rais alikuwa yeye akiwahi kuhudumu kama seneta na

baadaye katibu mkuu pale kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.

Katibu wake mkuu, Celestine Mwesigwa pia alikuwa ni Yanga na aliwahi kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo. Msemaji Baraka Kizuguto alikuwa Yanga lialia na aliwahi kuwa msemaji wa klabu hiyo. Kizuguto akabadilishiwa majukumu na nafasi yake kuchukuliwa na Alfred Lucas. Huyu ni Yanga mwingine lialia.

Baadaye walioongezewa nguvu na mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi. Karume pakawa njano na kijani. Hili halikuwa jambo jema kwa mtawala ambaye alikuwa mweupe na mwekundu.

Alifanya kazi hivyohivyo hadi lilipofunguliwa dirisha kubwa la usajili la msimu wa 2014/15. Wakati huo Yanga walikuwa na mshambuliaji kutoka Uganda, Emmanuel Okwi ambaye alisajiliwa kwenye dirisha dogo la 2013/14. Lakini kutokana na usumbufu aliowafanyia wakataka kumuacha kwa kumshtukiza siku ya mwisho ili wamkomoe kwa kukosa timu.

Lakini kama mkurugenzi wa Sheria na Simba lialia, inadaiwa kwamba Mtawala alishtukia dili na inaelezwa kwamba mambo yalivuja na kuwafikia vigogo wa Simba ambao walimsajili kijana wao.

Hili linadaiwa kuwa kero kubwa kwa watu wa njano na kijani na inadaiwa walianza kumuona Mtawala siyo mmojawao.

Ingawa hakuna uthibitisho inaelezwa kwamba alijikuta akifanya kazi katika mazingira magumu ya kazi, naye akaacha.

TFF YA KARIA

Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeshindwa kufuzu Afcon 2022 baada ya kujikusanyia alama saba ambazo zimepitwa na Tunisia na Guinea ya Ikweta.

Matumaini ya Stars yalikatika baada ya kipigo cha kuumiza cha dakika ya mwisho dhidi ya Guinea ya Ikweta.

Kabla ya mchezo huo, kocha wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije alitimuliwa na nafasi yake kuangukia kwa Kim Poulsen.

Huyu kocha naye asubiri upupu wake kwa sababu inakuwaje anakuwa kocha wa Tanzania tu. Akifukuzwa anakaa bila timu hadi Tanzania imfuate, ina maana kama ni kocha mzuri angepata timu nzuri, japokuwa baada ya kutoka Tanzania aliifundisha FC Sønderborg iliyopo katika Mkoa wa Jutland Kusini mwa Denmark

Turudi kwenye mada. Ndayiragije akaondoka, lakini wasaidizi wake, Juma Mgunda na Selemani Matola wamebaki. Unaweza ukajiuliza hawa makocha wana siri gani na Stars kiasi kwamba hawatoki.

Dhana ya makocha wazawa kuwa wasaidizi huwa na maana kubwa sana hasa ikilenga katika kuinua uwezo wao ili baadaye waachiwe timu.

Hivi ndivyo walivyofanya Wajerumani kwa Joachim Loew ambaye alikuwa msaidizi wa Jurgen Klinsmann, lakini hii haipo kwa wasaidizi wetu pale Stars.

Kocha kama Matola hawezi akaachiwa timu ya taifa ilhali klabu tu hawezi kuachiwa. Nachoamini ni kwamba kinachomfanya aendelee kubaki kwenye benchi la Stars ni upendeleo wa TFF ya sasa ambao umejikita kwenye Usimba. Watu wengi waliopo pale TFF ni Simba.

Niseme tu kwamba kama hili limetokea kwa bahati nzuri, basi ni jambo la kushukuru maana haikuwa nia au dhamira ya wanazi wa klabu moja kujikuta wakiongoza shirikisho lenye klabu nyingi zenye nasaba tofauti.

Lakini iwapo inatokana na dhamira ya dhati kuwa hivyo, basi hili ni kosa. Vinginevyo niseme tu kuwa kama ni dhamira ya dhati, basi rais Karia atakuwa anapita njia zilezile za utawala uliopita.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz