Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Soka la Tanzania ni punda afe mzigo ufike

Simba Kipigo Prisons.jpeg Soka la Tanzania ni punda afe mzigo ufike

Wed, 6 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, aliwahi kusema, ‘nikipewa saa sita kukata mti, nitatumia saa nne kunoa shoka.

Hapa Lincoln alikuwa analenga kuonesha umuhimu wa kujiandaa.

Unapojiandaa vizuri, unaweza kufanya jambo kubwa kwa mafanikio hadi watu wakashangaa.

Mara nyingi watu husingizia bahati pale wanapomuona mwenzao amefanikiwa halafu wao wanakwama.

Ni kweli, wakati mwingine bahati ina mchango mkubwa sana kwenye mafanikio. Lakini bahati ni nini?

Bahati ni njia panda ambapo barabara inayoitwa maandalizi hukutana na ile ya nafasi au fursa.

Yaani huwezi kupata bahati kama hujajiandaa. Hakuna aliyewahi kuokota pesa akiwa kitandani kwake.

Lazima uamke na utoke nyumbani kwako, na huwezi kutoka kama hukujiandaa.

Nimetumia maneno mengi kulizungumzia hilo nikilenga namna mamlaka za mpira nchini zinavyokwamisha maandalizi ya klabu zetu.

MUDA WA KUPUMZIKA NA KUJIANDAA

Msimu wa soka Tanzania wa 2021/22 umefungwa rasmi Julai pili baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports pale Arusha.

Msimu mpya wa 2022/23 utaanza rasmi Agosti 27 kwa mchezo wa ngao ya jamii.

Kutoka Julai pili hadi Agosti 17 ni siku 46 ambazo ni sawa na wiki 6, siku 3, saa 23, dakika 59 na sekunde 59...au tuseme wiki sita na nusu.

Kitaalamu maandalizi ya kabla ya msimu, yaani pre season, huchukua wiki sita kamili.

Kwa hiyo ili timu zetu zijiandae vilivyo msimu ujao, zinahitaji wiki sita za maandalizi ya kabla ya msimu...ambazo ni sawa na siku 43.

Na ili timu zianze maandalizi ya msimu mpya, lazima wachezaji wapate angalau siku 30 za kupumzika kutokana na hekaheka za msimu uliotangulia.

Kwa hiyo msimu mpya kitaalamu unapaswa kuanza baada ya siku 76 tangu kumalizika Kwa msimu uliopita.

Lakini msimu wetu hapa Tanzania utaanza siku 46 baada ya kumalizika kwa msimu wa nyuma yake.

Maana yake, kukiwa na wiki 6 yaani za maandalizi ambazo ni sawa na siku 43 , basi wachezaji itabidi wapumzike kwa siku zile tatu na ushei zitakazobaki katika zile siku 46.

Au kukiwa na mapumziko ya siku 30, maana yake maandalizi ya msimu mpya yawe ya siku 16 zitakazobaki kwenye zile 46.

Haya mawili yote hayawezekani kwenda, kitakachofanyika ni kuzigawa zile siku 46 ili angalau muda wa mapumziko na maandalizi upatikane japo kidogo kidogo.

Kwao, ratiba itakuwa imeenda sawa...mambo yao yamewanyookea na watajipa bonasi kubwa.

Hawajali kama wachezaji watakosa muda mzuri wa kupumzika, hawajali kama watakosa muda mzuri wa maandalizi.

VIWANJA

Anayepanga hivi ni mamlaka, yaani bodi ya ligi - kama wasimamizi wa ligi zetu za kulipwa, na TFF - kama wasimamizi wa mpira wenyewe kwa ujumla - pamoja na mechi ya Ngao ya Jamii, mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports na hata ligi za madaraja ya chini.

Vyombo hivi viwili ndivyo wakati fulani vilifungia viwanja vya mpira kwa sababu havikuwa na kuta, na kuhamishia mechi kwenye viwanja vyenye kuta lakini havina sehemu nzuri za kuchezea.

Kwa mfano kuhamishia kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga mechi Mwadui FC kutoka Uwanja wa Mwadui Complex, ilikuwa moja ya uamuzi ya kipunda punda kabisa

Sehemu ya kuchezea ya Uwanja wa Kambarage ilikuwa ya hovyo hata kwa mashindano ya mchangani.

Lakini kwa sababu ukuta ulikuwepo, hakukuwa na shida kwao.

Hawa wachezaji katika ngazi ya juu kama Ligi Kuu, wanapaswa kuenziwa kama watu wa mfano.

Hupaswi kuwachezesha sehemu yoyote tu...hapana.

Kama uwanja fulani hauna vigezo, hamishia hiyo mechi kwenye uwanja wenye vigezo hata kama uko mbali kiasi gani.

Lakini wao hawakujali, mradi mambo yao yameenda na mwisho wa msimu wakapeana bonasi kubwa kujipongeza.

TUZO ZA WACHEZAJI BORA

Msimu uliopita, Idd Seleman Nado wa Azam FC alikuwa bora kuliko Feisal Salum na hata Mukoko Tonombe wa Yanga pia.

Lakini kuwania tuzo za mchezaji bora, Nado hakuwemo, wakawemo watu ambao aliwazidi mbali sana.

Msimu huu kijana mzawa George Mpole kutoka Geita ambaye ameibuka mfungaji bora, hayumo kwenye tuzo yoyote ya kugombania zaidi ya ufungaji Bora, ambayo haitegemei kupendekezwa na wenye mpira wao.

Tuzo ni pongezi kwa waliojitajidi katika msimu mzima ili kuwaonyesha kwamba jitihada zao zimeonekana, na kuwahamasisha wajitahidi tena msimu ujao.

Lakini pia kuwahamasisha waliokosa tuzo ili msimu ujao waongeze jitihada.

Lakini kwa kamati ya tuzo ya TFF haipo hivyo, wao kwao tuzo ni kufurahisha nafsi zao na nafsi za Yanga na Simba.

Hivi Yanga na Simba zinaingiaje kuwania tuzo za timu zenye nidhamu kwa makosa yote waliyoyafanya msimu huu?

Ni faini ngapi wamepigwa kwa kukosa nidhamu...inakuwaje wanawaweka katika tuzo hiyo?

Wanaostahili wanaachwa kisha kuchukuliwa wasiostahili ili mambo yao yaende na mwisho wapeane mabonasi makubwa kijipongeza.

Punda afe lakini mzigo ufike!

Columnist: Mwanaspoti