Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Russia na Ukraine zimeonyesha kitu flani

RUSS UKRAINE Russia na Ukraine zimeonyesha kitu flani

Wed, 16 Mar 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa miaka mingi ulimwengu wa michezo ulikaririshwa kwamba siasa hazituhusiwi michezoni. Japo tunajua kwamba siasa inatawala asilimia zaidi ya 60 ya kila kitu duniani, lakini michezo ilijifanya kutaka kujitenga nayo.

Japo wanasiasa waliendelea kuwa marafiki wakubwa wa michezo na wanamichezo wakiwemo viongozi wa taasisi za kimichezo kama FIFA, lakini siasa ilitajwa kuwa adui. Kwenye Afcon 2008 nchini Ghana, Mohamed Aboutrika wa Misri alifunga bao dhidi ya Sudan na kuvua jezi yake ili aonyeshe ujumbe wa kisiasa wenye mlengo wa huruma kwa watu wa Gaza, Palestina.

Itakumbukwa mzozo wa miaka yote wa Israel na Palestina na wiki hiyo Israel ilifunga mipaka ya Gaza na kusababisha mtafaruku kwa sababu watu wa mji huo hutegemea mahitaji yao kutoka nje, hasa Misri. Kitendo cha Israel kuwafungia ndani kililenga kuwaua njaa.

Watu zaidi ya laki saba wakakiuka vizuizi vile na kuingia Misri kununua mahitaji yao ya msingi kama chakula. Ndipo Aboutrika akatoa ujumbe kwa dunia kuwaonea huruma watu wa Gaza ‘Sympathize With Gaza’, ndivyo fulana yake aliyoivaa kwa ndani ilivyosomeka.

Aboutrika aliandikiwa barua rasmi na CAF ya onyo kali. Caf wakasema Fifa inakataza ujumbe wa kisiasa kwenye michezo. Afrika ikamezeshwa hivyo na dunia ikaamini hivyo.

Kwenye Kombe la Dunia 2018, kocha msaidizi wa Croatia, Ognjen Vukojevic alifukuzwa kazi wakati mashindano yakiendelea kwa kosa la kuweka kwenye mtandao wa kijamii video fupi yenye ujumbe wa kisiasa akiwa na mchezaji wake, Domagoj Vida.

Vida mwenyewe ambaye ndiye alizungumza kwenye video hiyo akapewa onyo kali. Siasa haziruhusiwi. Lakini ghafla mwaka 2022 taasisi za michezo duniani zinashindana kuhubiri siasa michezoni.

Ujumbe wa kisiasa kila sehemu siyo Ligi Kuu ya England, siyo Olimpiki ya majira ya baridi, siyo tenisi. Kote ni siasa tu. Serikali ya Uingereza imeingilia michezo kwa kuiadhibu Chelsea kwa kosa ambalo siyo la kwao...siasa!

FIFA ambayo ilitudanganya kwamba siasa haziruhusiwi michezoni imekuwa kinara kwenye siasa za Russia na Ukraine.

Imekuwa ya kwanza kutoa adhabu za kimichezo kwa kuzifungia ligi zote za Russia na hata kuiondoa Russia yenyewe kwenye Kombe la Dunia...siasa!

Mwanamichezo wa Misri, Ali Farag ambaye ni bingwa wa dunia wa mchezo wa skwashi ameonyesha kuhuzunishwa kwake na harakati za kisiasa michezoni. Akizungumza baada tu ya kushinda ubingwa wa dunia jijini London, Farag akahoji nini kimebadilika sasa hadi siasa zimekuwa sehemu ya michezo ilhali hapo kabla hazikuruhusiwa?

Akasema Palestina wamekuwa wakipitia matatizo haya ya Ukraine kwa miaka 74 sasa, lakini hakuna harakati kama hizi za sasa za kukemea ukandamizaji. Hili ni somo kubwa ambalo dunia imelipata kwa sasa.

Nadhani baada ya hapa inabidi ufanyike mkutano mkubwa kutathmini mwelekeo wa michezo kuhusu siasa. Kama tunaamini kwamba michezo inaweza kusaidia kufikisha ujumbe wa kisiasa kwa wahusika, basi tufanye hivyo. Tusitungiane sheria ambazo zinawaminya wengine lakini wengine wakiwa kwenye uhitaji, wanaruhusiwa kuzivunja. Afrika tumeathirika sana na vita. Libya tangu 2011 hadi sasa hakujatulia.

DRC tangu uhuru miaka ya 1960 hawajawa na utulivu wa kitaifa hadi leo. Irak tangu wavamiwe na Marekani 2003 hawajawa na utulivu hadi leo. Huko kote kuna mamilioni ya watu wasio na hatia, wanateseka. Hakuna tofauti kati ya watu wa Irak waliovamiwa na Marekani na watu wa Ukraine waliovamiwa na Urusi. Wote wanateseka, wote wanastahili huruma na wote wavamizi wao wanastahili kukosolewa. Lakini kwa Irak taasisi za kimichezo zilikaa kimya kama hakuna kilichokuwa kikitokea, ila kwa Ukraine zimeibuka!

Columnist: Mwanaspoti