Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Maelekezo CAF na migogoro kwenye mpira wa Tanzania

Karia, TFF President Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia

Thu, 9 Jun 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, limetoa maelekezo kwa vyama wanachama wake ikiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwamba mwisho wa kuwasilisha majina ya klabu na wachezaji wao kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Afrika msimu ujao ni Juni 30, 2022. Baada ya hapo hakutakuwa na klabu itakayopokewa na wala wachezaji watakaoruhusiwa kushiriki mashindano ya Afrika.

Hii ina maana kwamba Tanzania inaweza kukosa wawakilishi wa mashindano ya Afrika msimu ujao kama msimu wake wa soka hautakamilika ndani ya muda huo. Hadi sasa kwa mujibu wa ratiba ya TFF, msimu wa Tanzania utakamilika Julai 2 kwa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports. Yaani fainali ya Shirikisho ambayo itamtoa mshiriki wa Kombe la Shirikisho la Afrika itafanyika nje ya tarehe rasmi ya CAF. Hii ndiyo changamoto ambayo Tanzania imeshakutana nayo huko nyuma na kusababisha mgogoro mkubwa.

Ukiacha zama za giza, 1965 na 1966 ambapo Tanzania ilishindwa kushiriki mashindano ya klabu barani Afrika kutokana na Chama cha Soka Tanzania (FAT) kukosa uzoefu kiasi cha kutojua namna ya kutuma majina ya wawakilishi kwa ajili ya misimu ya 1966 na 1967 mtawalia, kuna miaka mingine katika zama hizi za mwanga yaani karne ya 21 ambapo agizo la CAF lilileta balaa.

MGOGORO WA 2003

Desemba 2001, FAT ilifanya uchaguzi mkuu kule Arusha na Michael Wambura akamuangusha katibu mkuu, Ismail Aden Rage na kuchukua nafasi. Mwenyekiti Muhidin Ndolanga (marehemu) alitetea nafasi yake ambayo alikuwa ameikalia tangu Desemba 1991 kwenye mkutano wa halmashauri kuu ya FAT mjini Mwanza.

Wambura akaanza kazi mwaka 2002 na alitakiwa apeleke CAF majina ya wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya Afrika ya msimu wa 2003. Tarehe ya mwisho ya CAF kupokea majina hayo ilikuwa Novemba 30, na ligi yetu iliisha Novemba 26.

Wawakilishi wa Tanzania walikuwa Simba SC kama mabingwa wa Tanzania (Ligi ya Muungano) mwaka 2002 na walitakiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. JKT Ruvu ambayo sasa ni JKT Tanzania walikuwa mabingwa wa Kombe la Nyerere ambalo sasa ni Kombe la Shirikisho la Azam Sports na walitakiwa kushiriki Kombe la Washindi la CAF.

Na Mlandege ya Zanzibar ilitakiwa kushiriki Kombe la CAF kwa sababu walikuwa washindi wa pili wa Ligi ya Muungano. Lakini katibu mkuu Wambura hakupeleka hata jina moja hadi tarehe ya mwisho inafika. Sijui kwa kutonywa au kwa uzoefu wao, Simba SC walipeka wenyewe jina lao na wachezaji wao CAF hivyo kutambulika kama wawakilishi wa Tanzania.Jambo hili lilileta mtafaruku mkubwa na kuitingisha FAT.

Kamati ya utendaji ikamuita Wambura na kutaka maelezo yake kwanini hakupeleka majina ya wawakilishi. Akasema alijisahau.

Kamati ikamuwajibisha kwa kumsimamisha, lakini akaenda mahakamani kupinga na mahakama ikamrudisha kazini. Kitendo cha Wambura kwenda mahakamani 2002 kilimtesa maisha yake yote ya uongozi kwenye soka na pamoja na mambo mengine, kumgharimu nafasi yake ya makamu wa rais aliyoipata 2017.

MGOGORO WA LIGI YA MUUNGANO 2003

Vijana wengi wa sasa hawaijui Ligi ya Muungano na wengine ambao wamehadithiwa au kusoma juujuu, huitaja kama Kombe la Muungano. Kimsingi ni kwamba Kombe la Muungano na Ligi ya Muungano yalikuwa mashindano mawili tofauti. Kombe la Muungano yalikuwa mashindano kama ndondo ambayo yalikuwa yakifanyika Mufindi mkoani Iringa, chini ya uratibu wa Daud Yassin.

Ligi ya Muungano yalikuwa mashindano makubwa yaliyoandaliwa kwa pamoja na FAT na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ambayo Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) na CAF waliyatambua kama Ligi Kuu rasmi ya Tanzania. Bingwa wa Ligi ya Muungano alishiriki Klabu Bingwa Afrika ambayo kuanzia 1997 ikawa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mshindi wa pili wa Ligi ya Muungano alishiriki Kombe la Washindi Afrika - endapo msimu huo hakukuwa na Kombe Nyerere, ambalo sasa linaitwa Kombe la Shirikisho la Azam Sports. Mshindi wa tatu wa Ligi ya Muungano alishiriki Kombe la CAF la Afrika. Wakati huo Afrika ilikuwa na mashindano matatu ya ngazi ya klabu kama yalivyoanishwa hapo juu. Mwaka 2004, Kombe la Washindi na Kombe la CAF yaliunganishwa na kuzaliwa mashindano mapya ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ligi ya Muungano ilianza 1981 na kufa 2003. Sababu ya kufa kwa ligi hiyo ni CAF kuitambua Zanzibar kama mwanachama wake kivuli na kuipa nafasi za moja kwa moja kwa klabu zake kushiriki mashindano ya Afrika.

Hii ikawa na maana kuanzia 2004 Zanzibar itoe timu zake kushiriki mashindano ya CAF na Bara itoe timu kushiriki mashindano ya CAF. Kwa kuwa Ligi ya Muungano ililenga kupata wawakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mashindano ya Afrika, basi ikawa haina tena maana. Lakini hata hivyo, msimu wa mwisho yaani 2003 haukukamilika, sababu ni maagizo ya CAF kama ya mwaka huu. CAF iliagiza kwamba kufikia Desemba 24, kila nchi iwe imewasilisha majina ya klabu zitakazoshiriki. Ligi ya Muungano ilipaswa kuanza baada ya kukamilika ligi kuu za Bara na Zanzibar. Ligi ya Zanzibar iliisha Septemba tu lakini ya Bara ikaenda hadi Novemba 26.

Kwa kuhofia kuchelewa tarehe ya CAF ya kupokea wawakilishi, FAT na ZFA waka-kubaliana kwamba Ligi ya Muungano ya mwaka huo ichezwe kwa mtoano badala ya mfumo wa nyumbani na ugenini, ili imalizike mapema kuiwahi tarehe ya CAF. Mtindo kama huo ulishawahi kufanyika 1992 na hata mwaka 2002.

Ili mtoano uende vizuri walikubaliana wachukue timu nne za juu badala ya tatu kama ilivyokuwa kawaida kutoka kila upande wa Muungano, ili wapate timu nane zianzie robo fainali. Yanga iliyomaliza katika nafasi ya nne kwenye ligi ya Bara ikaangukiwa na dodo na kwa Zanzibar, timu ya nne ilikuwa Maendeleo FC. Lakini uamuzi huo ni kama ukawatokea puani FAT na ZFA kwani Yanga iliyokaribishwa ikazua mgogoro uliosababisha ligi kusambaratika.

UTATA

Ligi ya Muungano ikapangwa kuanza Desemba 10 na Yanga ikapangiwa Jamhuri ya Pemba. Wakatoka Dar es Salaam kuelekea Pemba kupitia Unguja. Walipofika Unguja, wakagoma kwenda Pemba kwa madai kwamba wamegundua hakuna ligi duniani inayochezwa kwa mtoano, hivyo wao hawapo tayari kucheza ligi ya mtoano. FAT na ZFA wakawaambia kwamba hii ni sehemu tu ya ligi ambayo imeanza tangu Januari kwa muundo wa nyumbani na ugenini, na hata baadhi ya misimu ya huko nyuma ilichezwa kwa mtindo huohuo na Yanga walishiriki, lakini wapi, Yanga waligoma!

FAT na ZFA zikaamua kuachana na Yanga na kuendelea na mashindano na timu zilizobaki mechi zikachezwa.

Yanga, kupitia katibu mkuu wao, Jamal Malinzi, wakapinga kitendo cha ligi kuendelea bila wao wakaenda kufungua kesi Mahakama ya Wilaya ya Ilala kusimamisha ligi. Ni vyema ligi yetu ikianza imalizike kwa wakati na bila kuwa na mizengwe.

Columnist: Mwanaspoti