Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Kigonya, alijitambulisha na kujishusha kupitia Simba

Kigonya Math Golikipa wa Azam, Mathias Kigonya

Wed, 19 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Februari 7, 2021, kipa mpya wa Azam FC aliyesajiliwa kupitia dirisha dogo kutoka Forest Rangers ya Ndola nchini Zambia, Mathias Kigonya alicheza mechi yake ya kwanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ilikuwa katika mchezo dhidi ya Simba SC iliyokuwa kwenye fomu ya hali ya juu. Kipindi cha kwanza chote Azam FC walikuwa wanafundishwa namna ya kupiga pasi, chenga na namna ya kuingia kwenye eneo la hatari la wapinzani.

Meddie Kagere, Larry Bwalwa, Louis Miquisone na Clatous Chama walikuwa wanapita na kuingia kwenye eneo la hatari la Azam FC walivyotaka. Kikwazo pekee kwao kilikuwa mtu mmoja mfupi katikati ya nguzo mbili na milingoti ya goli aliyeitwa Mathias Kigonya.

Aliokoa kila hatari hadi penati ya Clatous Chama na kuwanusuru Azam FC na kipigo cha aibu siku hiyo angalau hadi mapumziko. Dakika 45 za kwanza Simba wangeweza kuwa mbele kwa mabao sio chini ya matatu kama si uhodari uliopitiliza wa kipa huyu mpya.

Dakika ya sita tu ya mchezo, Miquisone alipata nafasi ya ana kwa ana na Kigonya, lakini jaribio lake likaishia mikononi mwa raia huyo wa Uganda, japo Miquisone alikuwa ameotea. Dakika ya saba Meddie Kagere naye akabaki ana kwa ana na Kigonya, lakini kipa huyo alifanya uokozi wa hali ya juu.

Ndani ya dakika hiyohiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akaambaa kushoto mwa uwanja na kumimina krosi ya hatari ambayo Kigonya alijinyoosha kwa umaridadi mkubwa na kuiweka salama timu yake.

Hizi ni dakika ambazo Azam FC walipigwa mafuriko ya hali ya juu. Walifanyiwa pressing ya maana na kujikuta wakipoteza kila mpira walioupata na kumpa wakati mgumu Kigonya. Safu ya ushambuliaji ya Simba ikapoteza kujiamini kutokana na hofu ambayo Kigonya aliwatia kutokana uimara wake.

Mfano halisi ni Meddie Kagere na Larry Bwalya waliopoteza nafasi za wazi kabisa dakika ya tisa. Dakika ya 20, Miquisone aliachia shuti kali nje kidogo ya 18, lakini Mathias Kigonya akafanya kazi ya ziada kulipangua.

Shuti kama hilo Miquisone alilipiga dhidi ya Al Ahly na kufunga bao kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini Kigonya akasema yeye siyo El Shenawy wa Misri. Dakika ya 23, Thadeo Lwanga aliachia shuti kali ambalo Kigonya alilidaka na kumtoka na kumkuta Meddie Kagere naye shambulio lake likaishia mikononi mwa Kigonya.

Huwezi amini, hakuna hata mtu mmoja ambaye angemlaumu Kigonya siku hiyo endapo mashambulizi yote haya yangeishia kwenye nyavu. Azam FC walianza mechi vibaya na Simba walikuwa kwenye ubora wa hali ya juu. Kilichoufanya mchezo huo kuwa sare hadi muda ule ni mikono ya Kigonya.

Kigonya alihitimisha dakika 45 za ushujaa kwa kuokoa penati iliyopigwa na Clatous Chama. Hapo ndipo akajitambulisha kwenye Ligi Kuu Bara kama mmoja wa makipa wa daraja la juu. Kigonya aliendelea kuyaishi maisha hayo ya ‘wonderful saves’ kila uchao na kuwateka Watanzania.

Lakini msimu huu wa 2021/22 haukuwa mzuri kwake tangu mwanzoni. Aliruhusu mabao rahisi kirahisi takriban katika kila mechi. Bao dhidi ya Pyramids kule Cairo, mabao yote dhidi ya Polisi Tanzania pale Moshi, bao la pili dhidi ya Yanga na mabao yote mawili dhidi ya KMC ni mfano wa udhaifu wa Kigonya msimu huu.

Lakini hatima ya yote hayo ni makosa ya mwanafunzi wa chekechea aliyoyafanya kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi. Kipa huyo ambaye alianza kuwatia hofu watu kwenye mchezo wa nusu fainali ambapo alishindwa kuokoa hata penati moja katika tisa zilizoelekezwa kwake.

Kilele ndiyo kikawa kwenye fainali. Sehemu kubwa ya mchezo alionekana kama amelazimishwa kudaka. Hakuwa na furaha kabisa golini na mara zote alikaribisha hatari kwa kupenda kuuchezea mpira pasipo sababu ya msingi.

Hakutulia golini. Mara nyingi alionekana akisogea sana mbele na kuwaweka roho juu mashabiki wake kwa hofu ya kuotewa shuti la mbali.

Lakini, kosa lake la dakika ya 56 kwa Pape Sakho ambaye hakuwa na madhara yoyote ndilo hitimisho la ushujaa alioutengeneza mwaka mmoja uliopita. Akasababaisha penati ambayo alishindwa kuikoa na kuiponza Azam FC ambayo ilikuwa timu bora uwanjani kuliko Simba siku hiyo.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz