Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MZEE WA UPUPU: Keki ya Ligi Kuu igawanywe kwa Ligi zingine

Karia, TFF President Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia

Wed, 1 Jun 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inasimamia madaraja matatu; Ligi Kuu, Championship na League One.

Kwa maana rahisi haya ndiyo madaraja ya kitaifa kwenye mpira wetu na ndiyo mada yenye mwelekeo wa soka la kulipwa.

Lakini kwa bahati mbaya pengo la kipato kwa madaraja haya ni kubwa sana kwa sababu hakuna kabisa udhamini kwenye madaraja mawili ya chini, huku kukiwa na mamilioni kwenye Ligi Kuu Bara.

Azam TV wako Ligi Kuu, NBC wako Ligi Kuu na hata GSM nao waliingia kabla ya kutoka. Pia wapo TBC.

Bodi ya Ligi ni kama baba wa hizi ligi. Ukiwa baba mwenye watoto watatu kutoka mama tofauti halafu mtoto mmoja mama yake ana kipato kizuri, hakikisha zawadi anazopewa na mama yake zisiumize hisia za hawa wengine ambao mama zao ni dhoofu-li-hali.

Tengeneza mazingira ya upendo kwake kugawana na ndugu zake au hata kwa miongozo ya malezi ya kifamilia.

Haya ndiyo majukumu ambayo ningependa kuona Bodi ya Ligi inayabeba ili kusaidia hizi ligi.

TPLB inatakiwa kupunguza idadi ya timu kwenye madaraja haya ili mgawo uwe mzuri zaidi na kuleta tija zaidi.

Ligi Kuu iwe na timu 14 na madaraja mengine yawe na timu 16 kila moja.

Udhamini wa haki za matangazo kutoka Azam TV ni wa mabilioni ya shilingi ambapo kila timu hupata zaidi ya Sh40 milioni kwa mwezi sawa na milioni 500 kwa msimu.

Zikipungua timu mbili kutoka 16 za sasa hadi 14 pendekezwa ina maana kuna Sh2 bilioni zitabaki.

Chukua pesa hizi zigawanye kwenye yale madaraja mawili; Championship - bilioni moja na League One - bilioni moja.

Hii itasaidia sana kupunguza makali ya kiuchumi kwa timu za madaraja haya ambazo haziingizi fedha yoyote kutoka kwenye viingilio, mauzo ya bidhaa wala udhamini.

Haziingizi fedha kwa sababu nyingi, lakini kubwa ni kukosa mashabiki wa kutosha ambao wangeweza kuwa wateja wa bidhaa za klabu, kuingia viwanjani au kuvutia wadhamini.

Mashabiki wanakosekana kwa sababu klabu hizi hazina mradi wa kudumu.

Klabu zimekuwa kama bendi za sikukuu ambazo huanzishwa Desemba 24 ili kuwahi Krimas na mwaka mpya na kufa Aprili baada ya Pasaka.

Klabu ya mpira ili kutengeneza mashabiki inatakiwa kuwepo kwa muda mrefu ikiwezekana kuliko hata umri wa mtu.

Watu wanatakiwa wakue wakilisikia jina la klabu tangu utotoni hadi uzeeni kwao na watoto wao na wajukuu zao hali kadhalika.

Lakini kuanzisha klabu mpya kila siku hakuna afya kwa maendeleo ya biashara ya mpira wetu.

Kila mtu anatamani kuanzisha timu ili ishiriki ligi na baada ya kukamilisha lengo lake anaachana nayo.

Anaibuka mwingine anaanzisha timu na yeye anaivunja baada ya kukamilisha lengo lake.

Timu za namna hii zinatakiwa kuanzishwa kwa ajili ya mashindano ya soka la mtaani lakini siyo ligi.

Ligi ni mradi endelevu ambao unatakiwa uwe na mpango wa muda mrefu ili kuwavutia mashabiki ambao watakuwa wateja kwenye biashara ya mpira.

Mamlaka za mpira zitengeneze mazingira magumu kwa kila mtu kuanzisha timu na badala yake aongeze nguvu kwenye timu iliyopo katika eneo lake.

Kuwe na madaraja mengi kutoka timu kuanzishwa hadi kufika Ligi Kuu.

England kwa mfano, kuna madaraja zaidi ya saba kutoka ligi ya chini kabisa hadi Ligi Kuu.

Mlolongo huu wa madaraja huwakatisha tamaa wenye malengo ya haraka haraka ya kuanzisha timu ili washiriki Ligi Kuu, hivyo kujikuta wakiungana na zilizopo.

Sasa hapo utazifanya timu zilizopo kudumu na kuzalisha mashabiki ambao zitawageuza wateja.

Na hawa mashabiki pia watakuwa kivutio cha wadhamini kwa sababu mdhamini anataka watu wa kufanya nao biashara pale anapowekeza kwenye timu.

Ndipo biashara ya mpira itakuwa kubwa na klabu zitaweza kujitegemea kiuchumi.

Lakini hiyo itachukua muda mrefu, sasa ili kuweza kufika huko lazima kuwe na mpango maalumu wa kuziwezesha klabu zilizopo kujikwamua kiuchumi.

Na mpango huo ni kuigawana hii keki ya taifa iliyopo mezani kwa sasa.

Columnist: Mwanaspoti